• HABARI MPYA

    Friday, December 12, 2025

    HAMZA AKAMILISHA MATIBABU YAKE NCHINI MOROCCO


    BEKI wa kati wa SimbaSC, Abdulrazack Mohamed Hamza amekamilisha matibabu ya upasuaji ambayo yamefanyika nchini Morocco. 
    Hatua hiyo inampa Hamza matumaini mapya ya kurejea uwanjani baada ya kipindi kirefu cha kuwa nje ya majukumu ya timu.
    Uongozi wa Simba umethibitisha kuwa mchezaji huyo anaendelea vizuri na kwamba taratibu za mwisho za matibabu wa jeraha lake zinaendelea kufuatiliwa kwa karibu.
    Hamza alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha yaliyomsumbua msimu huu, hali iliyoathiri mchango wake ndani ya kikosi cha wekundu wa Msimbazi.
    Majeraha hayo yaliyokuwa yakijirudia yalimlazimu kufanyiwa vipimo vya kina ambavyo vilionyesha kuwa upasuaji ulikuwa hatua sahihi zaidi ili kurejesha ubora wake.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio nchini Morocco, eneo ambalo klabu hiyo imekuwa ikitumia kwa wachezaji wake kupata huduma bora za kitabibu kutokana na ubobezi wa wataalamu wao.
    Madaktari wamethibitisha kuwa beki huyo yupo katika hali nzuri na mwitikio wa mwili wake baada ya upasuaji unaridhisha.
    Klabu imesema awamu inayofuata kwa mchezaji huyo ni kuanza programu maalumu ya itakayodumu kwa muda maalumu kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye mazoezi mepesi.
    Ratiba yake ya kurejea dimbani itategemea mwendelezo wa maendeleo yake katika kipindi hiki cha kuimarika upya.
    Hamza ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitegemewa kwenye eneo la ulinzi kutokana na uthabiti, nguvu na utulivu wake katika kuongoza safu ya nyuma. Kutokuwepo kwake kumeifanya Simba kujaribu mbinu na muunganiko tofauti kwenye ulinzi msimu huu.
    Kwa sasa mashabiki wa Simba wanapewa matumaini kuwa kurejea kwa Hamza kutaleta nguvu mpya, hasa katika kipindi ambacho timu inajiandaa na mechi ngumu za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
    Beki huyo aliumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii wa kariakoo dabi uliochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa Septemba 16  mwaka huu.
    Next
    This is the most recent post.
    Older Post
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAMZA AKAMILISHA MATIBABU YAKE NCHINI MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top