• HABARI MPYA

    Thursday, July 12, 2012

    NDOO NNE ZA KAGAME ZILIVYOTUA YANGA, JE WATABEBA YA TANO 2012?


    Kikosin cha mwisho Yanga kutwaa Kagame mwaka jana; Kutoka kulia waliosimama ni Yaw Berko, Davies Mwape, Chacha Marwa, Juma Kijiko, Jerry Tegete na Nadir Cannavaro. Walioinama ni kutoka kulia Oscar Joshua, Nsajigwa Shadrack, Godfrey Taita, Hamisi Kiiza na Nurdin Bakari.
    Na Prince Akbar
    MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, inatarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu yaani Jumamosi ijayo, kwa mabingwa watetezi, Yanga kufungua dimba na Athletico ya Burundi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, wanaingia kwenye michuano hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kutetea taji lao, baada ya kusajili wachezaji wapya nyota na kuajiri kocha mpya kutoka Ubelgiji, Thom Saintfiet.
    Miongoni mwa wachezaji nyota waliosajiliwa Yanga ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Kelvin Yondan kutoka Simba SC, Simon Msuva kutoka Moro United, Said Bahanuzi kutoka Mtibwa Sugar, Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Ladisalus Mbogo kutoka Toto African na Nizar Khalfan aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa Marekani.
    Hao wanaungana na nyota wengine wa Yanga waliowezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mwaka jana kama kipa Yaw Berko kutoka Ghana, Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’, Nahodha Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Godfrey Taita, Rashid Gumbo, Jerry Tegete na Shamte Ally.
    Lakini kikosini kuna Yanga kuna nyota wengine wa msimu uliopita, lakini hawakucheza Kombe la Kagame kama viungo Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Athumani Iddi ‘Chuji’. 

    SIRI YA JEURI YA YANGA
    Yanga inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa kampuni ya Shivacom.
    Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
    Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
    Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya kmaribuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano (2008, 2009 na 2011) sambamba na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.


    ZANZIBAR MWAKA 1975:
    Iliingia kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa michuano.
    Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
    Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba SC.
    Mabao ya Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.

    KAMPALA, UGANDA MWAKA 1993:
    Ilikwenda kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
    Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
    Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
    Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba  na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la pili la michuano hiyo.
    Marehemu Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

    KAMPALA, UGANDA MWAKA 1999:
    Ilikwenda kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka 1993.
    Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
    Naadiga Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji Express  na SC Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
    Kwa matokeo hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na mabingwa watetezi.
    Mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao ya
    Sekilojo Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
    Katika Robo Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa penalti.
    Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya 90.
    Hivyo kwa mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya mchezo huo.
    Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Peter akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.

    DAR ES SALAAM 2011:
    Yanga ilifanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Simba bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah aliyefunga bao hilo, pekee dakika ya 108, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kitaalamu na kiungo Rashid Gumbo.
    Kabla ya taji hilo walilotwaa Jumapili sambamba na dola za Kimarekani 30, 000, sawa na Sh. Milioni 45 za Tanzania, Yanga walitwaa tena Kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakiifunga Simba mabao 2-0 na baadaye mara mbili mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 na 1999, mara zote wakiifunga SC Villa ya huko.
    Ulikuwa mchezo mgumu ambao ulidumu kwa dakika 120, timu zikionyesha kucheza tahadhari, kabla ya Asamoah kumaliza kazi.
    Kikosi kilichoipa Yanga kombe la nne la Kagame kilikuwa; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid Gumbo, Godfrey Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari, Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
    Yanga iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.
    Katika Robo Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
    Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza Simba SC katika fainali.
    Ikumbukwe katika michuano ya mwaka huu, Yanga iliingia kama ‘viti maalumu’, kwani Simba SC ndio walikuwa wawakilishi halisi kama mabingwa wa Bara.
    Ili kushiriki mashindano ya mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe CECAFA dola za Kimarekani 20,000 kama faini ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu wa michuano hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es Salaam.
    Yanga ilitakiwa kucheza na Simba mwaka huo kuwania nafasi ya tatu, ikiwa chini ya Mwenyekiti aliyekuwa na misimamo mikali, Wakili Imani Omar Madega, Yanga iligoma kwa sababu hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa mapato ya milangoni. 
    Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa mataji yake manne ya Kombe la Kagame- na Jumamosi wanaanza changamoto ya kuifukuza rekodi ya watani wao wa jadi, Simba SC waliotwaa taji hilo mara sita, je wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NDOO NNE ZA KAGAME ZILIVYOTUA YANGA, JE WATABEBA YA TANO 2012? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top