• HABARI MPYA

  Thursday, September 20, 2018

  HUYU NDIYE ALEX KITENGE WA STAND UNITED, MFUNGAJI WA HAT TRICK YA KWANZA YA MSIMU LIGI KUU

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Alex Kitenge raia wa Burundi anayechezea Stand United katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (TPL) mwishoni wa wiki iliyopita amekuwa gumzo baada ya kuifungia timu yake mabao matatu (hat trick) dhidi ya Yanga katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam licha ya kufungwa mabao 4-3.
  Kitenge pia amewahi kucheza ligi mbalimbali Afrika Mashariki ikiwemo Ligi Kuu za Burundi na Kenya ambapo katika Ligi ya Burundi amechezea timu za Lydia Ludic, Royal FC na Atletico Olympique huku Kenya akiichezea timu ya AFC Leopards.
  Kabla ya kucheza ligi kuu, Kitenge amechezea timu ya Taifa ya Burundi ya vijana wenye umri chini ya miaka ishirini (U20) akiwa chini ya Kocha Masoud Djuma ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa Simba SC.

  Alex Kitenge mfungaji wa hat trick ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu akikabidhiwa mpira 

  Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame ndiyo iliyomleta Tanzania akiwa na timu ya Lydia Ludic ya Burundi. 
  Michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ilifanyika Tanzania Juni hadi Julai, mwaka huu ikizihusisha timu kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.
  Moja kati ya vitu vilivyomfanya Kitenge kuwa gumzo, ni kitendo chake cha kufunga hat trick, lakini siyo tu hat trick ni kuweza kurudisha mabao matatu kwa timu ya Yanga iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 4-2 hadi dakika za mwishoni.
  Yawezekana jina la Kitenge limenogesha zaidi ushindi huo kutokana na Kitenge ni aina ya nguo inayovaliwa zaidi na wanawake pia wanaume kwa kiasi fulani lakini ngoja nikwambie kitu, kabla ya hat trick ya wikiendi iliyopita, mshambuliaji huyu ana hat trick nyingine tano ambazo amewahi kuzipiga awali akiwa anacheza ligi za Burundi na Kenya.
  Akiwa katika ligi hizo, Kitenge amewahi kufunga hat trick dhidi ya timu za Muzinga, Olympique Star, Lelier, Musongati na Sonny Sugar na juzi mbele ya Yanga amekamilisha hat trick yake ya sita ambayo pia ni ya kwanza katika msimu huu wa 2018/19  katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Kama kuna vitu anavyovifurahia katika mchezo dhidi ya Yanga ni kuweza kuifunga timu hiyo, Kitenge anasema licha ya kuibuka mchezaji bora alitakata zaidi katika mchezo huo amefurahi zaidi kuweza kuifunga Yanga ambayo ni timu kubwa yenye ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.
  Matamanio makubwa ya Kitenge ni kucheza soka la kulipwa barani Ulaya hivyo hata mkataba wake aliosaini na Stand United ni kwa muda wa mwaka mmoja tu. Lakini aliomba muda wowote timu nyingine ikimuhitaji basi aruhusiwe kuondoka klabuni hapo kwani bado anahitaji kusonga mbele zaidi.
  Ukiachana na kutamani kucheza Ulaya, mshambuliaji huyu anasema iwapo atatoka Stand United kama si kwenda Ulaya basi anatamani kucheza Simba, maana ndiyo timu anayoipenda na anaona ina kiwango kikubwa kuliko timu nyingine za Tanzania.
  Licha ya kuichezea Stand United Kitenge anasema anafahamiana na wachezaji wanaocheza na waliocheza Ligi ya Tanzania ambao miongoni mwao ni Paul Bukaba na Laudit Mavugo.
  Kitenge ni shabiki wa Klabu ya Liverpool ya England na Barcelona ya Hispania lakini mchezaji anayemkubali zaidi katika soka duniani ni  Luiz Suarez wa Barcelona, vilevile bado anatambua viwango vizuri vya Lionel Messi wa Barcelona na Christiano Ronaldo wa Juventus ambao yeye huwaita ‘mafundi’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HUYU NDIYE ALEX KITENGE WA STAND UNITED, MFUNGAJI WA HAT TRICK YA KWANZA YA MSIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top