• HABARI MPYA

  Friday, September 14, 2018

  MWADUI CHUPUCHUPU KUPIGWA NA AZAM FC, YASAWAZISHA BAO DAKIKA ZA JIONI KUPATA SARE 1-1

  Na Mwandishi Wetu, MWADUI
  AZAM FC imepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mwadui Complex, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga mchana wa leo.
  Sare hiyo inawafanya Azam FC wafikishe pointi saba baada ya awali kushinda mechi mbili nyumbani, 2-0 na Mbeya City na 3-0 Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Katika mchezo wa leo, wageni, Azam FC ndiyo walioanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 55, kabla ya Innocent Edwin kuwasawazishia wenyeji, Mwadui FC dakika ya 71.

  Mshambuliaji wa Azam FC, Daniel Lyanga akilalamika baada ya refa kukataa bao lake 

  Katika mchezo huo, refa aliingia lawamani kwa kukataa bao la mapema la Azam FC lililofungwa na mshambuliaji wake, Daniel Lyanga akidai alikuwa ameotea.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unaendelea hivi sasa Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kati ya African Lyon na Coastal Union. 
  Mechi zaidi za Ligi Kuu zitafuatia kesho Lipuli wakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mjini Iringa Saa 8:00 mchana, Ndanda na Simba SC Uwanja wa Nangwanda SIjaona Mtwara Saa 10:00 jioni, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting Saa 10:00 jioni Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbao FC na JKT Tanzania Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, KMC na Singida United Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa na Biashara United na Kagera Sugar Saa 10:00 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma mkoani Mara.
  Mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wao watateremka Uwanja wa Taifa Jumapili Saa 10:00 jioni kumenyana na Stand United, huo ukiwa mchezo wao wa pili tu baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWADUI CHUPUCHUPU KUPIGWA NA AZAM FC, YASAWAZISHA BAO DAKIKA ZA JIONI KUPATA SARE 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top