• HABARI MPYA

  Friday, September 14, 2018

  WAZIRI MKUU, MAJALIWA AMPONGEZA MWAKINYO KWA USHINDI WA UINGEREZA

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amempongeza bondia Hassan Mwakinyo kwa ushindi wake wa TKO dhidi ya Muingereza, Sam Eggington Uwanja wa Arena Birmingham, zamani Barclaycard Arena mjini Birmingham, England Jumamosi iliyopita.
  Mwakinyo aliushitua ulimwengu baada ya kummaliza Eggington kwa TKO katika raundi ya pili kuelekea pambano kuu jana kati ya Muingereza, Amir Khan na Samuel Vargas Colombia anayeishi Canada. Khan alishinda kwa pointi za majaji wote.
  “Na nimpongeze pia mwanamasumbiwi wa Kitanzania, Hassan Mwakinyo kwa kumchapa bondia Muingereza, Sam Eggington kwenye raundi ya pili ya pambano lao la masumbwi lililofanyika huko Birmingham nchini Unigereza,".
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) amempongeza bondia Hassan Mwakinyo (kushoto) kwa ushindi wake wa TKO Uingereza 

  "Hongereni sana wanamichezo wetu na endelezeni moyo huo wa kizalendo mliouonyesha katika kulitangaza taifa letu,”alisema Waziri Mkuu.
  Baada ya maelezo hayo, Spika wa Bunge Job Ndugai akamtambulisha Mwakinyo aliyealikwa Bungeni kwa ajili ya pongezi na Wabunge wote wakakubali kumchangia Sh. 20,000 kila mmoja kwa ajili ya pongezi.
  Baaada ya ushindi huo, Mwakinyo atapanda tena ulingoni Oktoba 20, kuzipiga na mwenyeji Wanik Awdijan ukumbi wa Alex Sportcentrum mjini Nuremberg, Ujerumani katika pambano la kuwania taji la vijana la IBF uzito wa Middle.

  Hassan Mwakinyo (kulia) akimuadhibu Sam Eggington (kulia) Jumamosi Uwanja wa Arena Birmingham 

  Litakuwa pambano lake la nne kupigana nje ya Tanzania, kwani kabla ya kumpiga Eggington alimshinda pia kwa TKO Anthony Jarmann wa Namibia Agosti 8, mwaka jana ukumbi wa Grand Palm Hotel mjini Gaborone nchini Botswana kabla ya Desemba 2, mwaka jana Mwakinyo kupoteza kwa pointi mbele ya mwenyeji, Lendrush Akopian ukumbi wa Krylia Sovetov mjini Moscow, Urusi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI MKUU, MAJALIWA AMPONGEZA MWAKINYO KWA USHINDI WA UINGEREZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top