• HABARI MPYA

  Friday, September 14, 2018

  AFRICAN LYON YAKAMILISHA MECHI NNE BILA USHINDI, COASTAL UNION YAOKOTA POINTI YA SITA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  TIMU ya African Lyon leo imekamilisha mechi nne bila ushindi, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Sare hiyo inayokuja baada ya kufungwa mechi moja na kutoa sare mbili awali, inawafanya wajiongezee pointi moja na kufikisha tatu, wakati wapinzani wao, Coastal Union wanafikisha pointi sita katika mechi ya nne, awali wakishinda moja na kutoa sare mbili.  
  Coastal Union walicheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi nzuri, lakini bahati mbaya wakashindwa kuzitumia ikiwemo ya dakika ya 25 pale washambuliaji waliposhindwa kumalizia krosi nzuri ya Hamisi Mustafa.

  Mshambuliaji wa Coastal Union, Hajji Ugando akimiliki mpira mbele ya beki wa African Lyon leo mjini Dar es Salaam

  Mashambulizi ya kusisimua ya African Lyon yote yalifanywa na mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 28 akipiga nje kidogo ya lango na dakika ya 39 akipiga shuti lililodakwa na kipa wa Coastal, Hussein Sharrif ‘Casillas’.
  Coastal Union nao walijibu kwa shambulizi la dakika ya 54, baada ya Issa Abushehe kupiga shuti lililogonga mwamba na dakika ya 55 Moses Kitandu anayecheza kwa mkopo kutoka Simba SC akapiga shuti ambalo kipa Douglas Kisembo alidaka.
  Mechi zaidi za Ligi Kuu zitafuatia kesho Lipuli wakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mjini Iringa Saa 8:00 mchana, Ndanda na Simba SC Uwanja wa Nangwanda SIjaona Mtwara Saa 10:00 jioni, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting Saa 10:00 jioni Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Mbao FC watamenyana na JKT Tanzania Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, KMC na Singida United Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa na Biashara United na Kagera Sugar Saa 10:00 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma mkoani Mara.
  Mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wao watateremka Uwanja wa Taifa Jumapili Saa 10:00 jioni kumenyana na Stand United, huo ukiwa mchezo wao wa pili tu baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
  Kikosi cha African Lyon kilikuwa: Douglas Kisembo, Khalfan Mbarouk, Omary Salum, Agustino Samson, Daudi Mbweni, Baraka Jaffary, Awadh Salum, Ismail Gambo, Victor Da Costa/Salum Mbowe dk64, Haruna Moshi ‘Boban’ na Gervas Bernard.
  Coastal Union: Hussein Sharrif ‘Casillas’, Adam Mohammed, Adeyum Saleh, Ibrahim Ame, Bakari Nondo, Hassan Ally, Muhsin Malima/Mtenje Albano dk80, Moses Kitandu/Andrew Albert dk80, Hamisi Mustafa, Hajji Ugando na Issa Abushehe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AFRICAN LYON YAKAMILISHA MECHI NNE BILA USHINDI, COASTAL UNION YAOKOTA POINTI YA SITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top