• HABARI MPYA

    Friday, September 21, 2018

    CAF, TFF YATOA POLE AJALI YA KIVUKO CHA MV NYERERE KILICHOZAMA KATIKATI YA BUGORARA NA UKARA JANA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) na la Tanzania (TFF), wametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere kinachofanya safari zake kati ya Bugorara na kisiwa cha Ukara katika ziwa Victoria kilichozama jana.
    Taarifa ya TFF pia imewatakia afya njema majeruhi wote waliounusurika kwenye ajali hiyo iliyotokea jana mchana. 
    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jonathan Shana alisema jana jioni kwamba kivuko hicho kilizama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara. Kiliondoka Saa 6:00 mchana na ilipofika Saa 8:00 mchana kilipinduka.
    Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda alikiri kuzama kwa kivuko hicho na yuko njiani kulekea huko na watatoa taarifa baadaye.

    Miili ya watu zaidi ya 44 iliokolewa jana kabla ya zoezi la uokoaji kusitishwa hadi leo

    Kivuko cha MV. Nyerere kilinunuliwa na kuanza kutoa huduma mwaka 2004 na Julai mwaka huu kilifungwa injini mbili mpya zenye thamani ya Shilingi Milioni 19. 
    Kivuko hicho cha MV. Nyerere kina uwezo wa kubeba tani 25, sawa na abiria 100 na magari matatu kwa wakati mmoja.
    Miili ya watu zaidi ya 44 iliokolewa jana kabla ya zoezi la uokoaji kusitishwa hadi leo na watu wengine 37 waliokolewa wakiwa na hali mbaya.
    Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella anatarajiwa kuendelea kuongoza zoezi la uokoaji leo.
    Wakati huo huo: Rais CAF, Ahmad kupitia Rais wa TFF, Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi msiba wa waliofariki kwenye ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichozama jana kati ya Ukara na Bugorara,Ukerewe.
    Ahmad ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Muheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania kiujumla.
    Ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo mzito uliosababisha majonzi makubwa kwa Watanzania.
    “Naungana na Watanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Muheshimiwa John Magufuli kwa msiba huo mzito kwa Tanzania” alisema Ahmad.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAF, TFF YATOA POLE AJALI YA KIVUKO CHA MV NYERERE KILICHOZAMA KATIKATI YA BUGORARA NA UKARA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top