WENYEJI, Pyramids wamefanikiwa kwenda Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka nyuma mara mbili na kushinda 3-2 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini usiku huu Uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 Jijini Cairo.
Shujaa wa Pyramids leo ni mshambuliaji wa Kimataifa was Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele aliyefunga mabao mawili leo.
Mayele, nyota wa zamani wa Yanga ya Tanzania — alifunga mabao yake dakika ya 45’+1 na 84, huku bao lingine la Pyramids likifungwa na kiungo Mmisri, Ramadan Sobhi dakika ya 57.
Mabao ya Oralndo Pirates yamefungwa na mshambuliaji Relebohile Mofokeng dakika ya 41 na kiungo, Mohau Nkota dakika ya 52 na Pyramids wanakwenda Fainali kwa ushindi huo wa mbinde nyumbani kufuatia sare ya bila mabao kwenye mchezo wa kwanza Aprili 19 Uwanja wa FNB (Soccer City) Jijini Johannesburg.
Pyramids sasa watakutana na wapinzani wengine kutoka Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ambao mapema leo wamewatoa mabingwa watetezi, Al Ahly.
Mamelodi Sundowns wamekwenda Fainali kwa faida ya mabao ya ugenini kufuatia baada ya sare ya 1-1 leo Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo nchini Misri kufuatia sare ya bila mabao katika mchezo wa kwanza Aprili 19 Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria.
Katika mchezo wa marudiniano leo, mshambuliaji Taher Mohamed alianza kuwafungia Ahly dakika ya 24, kabla ya Yasser Ibrahim kujifunga dakika ya 90 kuitemesha tonge kinywani timu yake na kuipeleka Fainali Mamelodi.
Hii inakuwa mara ya kwanza Pyramids kuingia Fainali ya michuano hiyo, wakati Mamelodi Sundowns wanakwenda Fainali kwa mara ya tatu baada ya mwaka 2001 walipofungwa na Al Ahly 3-0 ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani na 2016 walipotwaa taji leo pekee kwa ushindi wa 3-0 nyumbani na kipigo cha 1-0 ugenini.
0 comments:
Post a Comment