• HABARI MPYA

    Tuesday, April 22, 2025

    KOMBE LA MUUNGANO SASA MECHI ZOTE NI DIMBA LA GOMBANI KISIWANI PEMBA


    MICHUANO maalum ya kuazimisha sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania tukufu Aprili 26, mwaka 1964 sasa itafanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba kuanzia Aprili 24 hadi Mei 1, mwaka huu (2024).
    Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imelazimika kuiondoa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambako ilipangwa kufanyika kati ya 
    Aprili 23 na Aprili 30 baada ya kupokea taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ikielekeza Uwanja huo kutotumiwa mfululizo ili kulinda ubora wake.
    Na hiyo kwa sababu Uwanja huo utatumika kwa Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee zinazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda zitakazofanyika Agosti mwaka huu.
    Nchi hizo tatu za Afrika Mashariki pia ni wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 zitakazofanyika Kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huo.
    Katika ratiba mpya ya Kombe la Muungano, michuano inayoanzia hatua ya Robo Fainali, wenyeji, JKU watamenyana na Singida Back Stars ya Singida Aprili 24 kuanzia Saa 11:00 jioni, kabla ya wenyeji wengine, Zimamoto  kuumana na Coastal Union ya Tanga Aprili 25 kuanzia Saa 10:00 jioni — na Saa 1:15 usiku wenyeji wengine, KMKM watacheza Azam FC ya Dar es Salaam.
    Vigogo, Yanga watakamilisha hatua hiyo ya Robo Fainali kwa kumenyana na wenyeji wengine, KVZ kuanzia Saa 1:15 usiku.
    Mechi za Nusu Fainali zitafuatia Aprili 28 na 29, wakati Fainali itachezwa Mei 1 hapo hapo Uwanja wa Gombani.
    Mabingwa watetezi, Simba wameshindwa kushiriki michuano ya mwaka huu kwa sababu wanakabiliwa na mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini Aprili Aprili 27 Jijini Durban.
    Simba SC ilitwaa taji la michuano hiyo iliyoanza mwaka jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, bao pekee la kiungo Msenegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
    Sarr alifunga bao hilo akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Israel Patrick Mwenda kufuatia mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana kuangushwa nje kidogo ya boksi.
    Simba SC ilizawadiwa Sh. Milioni 50, wakati washindi wa pili, Azam FC walipata Sh. Milioni 30. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOMBE LA MUUNGANO SASA MECHI ZOTE NI DIMBA LA GOMBANI KISIWANI PEMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top