• HABARI MPYA

  Wednesday, May 28, 2014

  WAMBURA ANAONEWA? SIMBA SC WAACHWE WAFANYE UCHAGUZI HURU NA WA HAKI

  MICHAEL Richard Wambura atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari leo, kuzungumzia uamuzi wa Kamati ya Uchahuzi ya Simba SC kumuengua katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa klabu hiyo mwezi ujao.
  Wambura ameenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi mkuu wa Simba SC, kwa sababu kubwa mbili, kupeleka masuala ya soka katika mahakama za dola na pili kuwa na vielelezo tata vya ushahidi wa kurejeshewa uanachama wake.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Wakili Dk Damas Daniel Ndumbaro aliwaambia Waandishi wa Habari jana makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), makutano ya mitaa ya Ohio na Libya, Dar es Salaam Wambura ameondolewa kwa sababu kwa sasa si mwanachama halali wa klabu hiyo.

  Ikumbukwe Wambura alisimamishwa uanachama wa Klabu ya Simba tangu Mei 5 mwaka 2010 kutokana na kosa la kuipeleka klabu hiyo mahakamani akifungua kesi namba 100 ya mwaka 2010 katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
  Ndumbaro amesema kuwa Wambura aliwasilisha barua pia katika Kamati ya Uchaguzi akikiri kuipeleka Simba mahakamani na kuiomba Kamati hiyo kumaliza suala lake na kuahidi hatarudia tena kufanya kosa kama hilo. Lakini kuwa amepingana na Katiba ya klabu, TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hakunusurika.
  Mwenyekiti huyo wa Kamati amesema kwamba pia walipokea barua mbili tofauti kutoka kwa Wambura, ya kwanza ikiwa ya Novemba 6 mwaka 2012 mgombea huyo akitaka kujua uhalali wa uanachama wake na nyingine ya Septemba 15, mwaka huo huo ikijibu kuwa Simba haina tatizo lolote na yeye.
  “Kuna utata katika barua zake na pia kuna barua ya tatu ya Septemba 25 mwaka 2012 ikieleza pia  Simba hawana tatizo na Wambura,” alisema Ndumbaro.
  Aliongeza kuwa kutokana na Kamati yake kujiridhisha na maelezo hayo, imeamua kumuondoa Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
  Ndumbaro ameeleza zaidi kuwa kutokana na maamuzi ya kusimamishwa huko, Wambura hapaswi kushiriki katika shughuli za Simba kwa mujibu wa Ibara ya 12(3) ya katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2010 na ibara ya 12(3) ya 2014.
  Ndumbaro alisema endapo Wambura hataridhika na maamuzi hayo, anaruhusiwa kukata rufaa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF.
  Ndumbaro amesema pia wagombea wengine wote walioekewa pingamizi wamepitishwa na wataendelea na mchakato wa uchaguzi huo utakaofanyika Juni 29 mwaka huu.
  Kwa kuondolewa Wambura, nafasi ya wagombea Urais inabaki na watu wawili, ambao ni Evans Elieza Aveva na Andrew Peter Tupa, wakati wanaowania Umakamu wa Rais ni Jamhuri Kihwelo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Swedi Nkwabi.
  Baada ya hatua iliyochukuliwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, tutarajie mengi kutoka kwenye kinywa cha Wambura leo, lakini tayari jana wapambe wake walianza kuzungumza na kutoa vitisho vya kwenda kuuzuia uchaguzi wa klabu hiyo katika mahakama za dola, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya TFF, CAF na FIFA na ndilo kosa ambalo linamtesa mgombea huyo hivi sasa.
  Lakini, inaokenakana kama Wambura anajivunia mbeleko ya kigogo mmoja wa juu wa TFF, ambaye alikuwa naye ‘msituni’ katika harakati za kusaka uongozi wa shirikisho hilo la kandanda nchini.
  Inaonekana kabisa kigogo huyo yuko bega kwa bena na Wambura kuhakikisha swahiba wake anaruhusiwa kugombea na habari zinasema, amekwishaanza kuiingilia hadi Kamati ya Uchaguzi.
  Uzuri wa Katiba mpya za klabu zetu zinatokana na mwongozo wa TFF, ambao nao wameupokea kutoka FIFA- na lazima kufuata mfano wa Katiba za bodi hizo kubwa za mchezo huo.
  Katiba inaagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi lazima awe mwanasheria kitaaluma, na Simba SC wamempata Ndumbaro ambaye katika taarifa ya maamuzi yake jana alilisimulia kinagaubaga suala la Wambura.
  Wambura mwenyewe amekiri kosa na kuiandikia barua Kamati hiyo, akiomba msamaha na kuahidi kutorudia, lakini Kamati ya Uchaguzi ya klabu ina mamlaka ya kumsamehe mgombea huyo?
  Jibu hapana- na kwa kuheshimu taaluma yake akiwa Mwanasheria, Ndumbaro ameamua kuchukua maamuzi kwa kuyarejea maandiko ya Katiba ya klabu hiyo.
  Bado, Wambura ambaye ameiandikia barua Kamati akikiri kosa na kuomba msamaha akawasilisha barua inayosema alikwisharejeshewa uanachama wake.
  Tatizo likajitokeza pia, barua aliyoandika kuomba kurejeshewa uanachama wake, inatanguliwa na tarehe ya barua ya kukubaliwa ombi lake- hii imeitia wasiwasi Kamati labda barua hizo ni za kufoji.
  Lakini bado kwa mujibu wa Katiba, Kamati ya Uchaguzi si chombo cha mwisho katika masuala tata ya wagombea na uchaguzi, ndiyo maana Ndumbaro amemuelekeza Wambura anaweza kukata Rufaa katika Kamati ya Maadili ya TFF.
  Tuna utaratibu mzuri tuliojiwekea katika mchezo kwamba hatupaswi kwenda kwenye mahakama za dola na kufanya hivyo ni kosa ambalo hukumu yake ipo wazi.
  Wambura alifanya kosa ambalo hata yeye analitambua, lakini sasa kuwa kuwa kuna swahiba wake pale TFF- inaonekana anampa jeuri ya kuendelea kupambana.
  Lakini na huyo kigogo wa TFF pia akae akijua kwamba, anapothubutu kumbeba mtu ambaye amekwishakiuka miiko ya Katiba za soka, anakaribisha vurugu.
  Yapo maswali mengi yanaulizwa kwa sasa kuhusu Wambura, kama hakuwa mwanachama halali, ilikuwaje akateuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na hata akashiriki mikutano ya klabu.
  Wambura alisimamishwa uanachama na hakuna kikao cha Kamati ya Utendaji kilichowahi kukutana tena kumrejeshea uanachama wake- na kama alishiriki mikutano ya wanachama, alifanya hivyo kimakosa kutokana na udhaifu uliokuwapo katika klabu wakati husika.
  Kuteuliwa Kamati ya Utendaji, Rage alifanya hivyo wakati wa mgogoro na vuguvugu la kupinduliwa na si kama alikuwa hajui kama anakiuka maamuzi yake mwenyewe na Katiba pia, bali aliamua kufanya ile watoto wa mjini wanasema kumwaga ugali, baada ya wenzake kumwaga mboga.
  Daima huwa sifungamani na upande wowote, bali najitahidi sana kufuata misingi ya haki katika uandishi wangu- na ninaamini wengi wananielewa kwa misingi hiyo.
  Wambura ni mmoja kati ya watu ninaofahamiana nao vizuri na kwa muda mrefu sasa- lakini hiyo haiwezi kunizuia kuandika ukweli juu yake hata kama utamuumiza.
  Kwa sasa, kusema Wambura anaonewa wakati mwenyewe amekiri kosa ni kuishiwa hoja za kumtetea, lakini pia tahadhari kwa huyo kigogo wa TFF, bora awaache Simba SC wafanye uchaguzi huru na wa haki pasipo kutumia mamlama yake ya kimadaraka kutaka kushinikiza mambo, aache waongozwe na Katiba yao ambayo ni mfano wa katiba ya FIFA. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAMBURA ANAONEWA? SIMBA SC WAACHWE WAFANYE UCHAGUZI HURU NA WA HAKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top