• HABARI MPYA

  Sunday, May 25, 2014

  NIMEWAELEWA SANA HANS POPPE NA JULIO, NANI MWENYE MAPENZI YA DHATI NA SIMBA SC?

  JAMHURI Mussa Kihwelo alisema amechukua fomu za kugombea nafasi ya Makamu wa Rais wa Simba SC kwa sababu ya kuwania uongozi ni sawa na kutongoza mwanamke, kuna kukubaliwa na kukataliwa.
  Nilimuelewa sana, beki huyo na kocha wa zamani wa Simba SC maarufu kwa jina la utani Julio- na wala haikuwa kauli ya dhalili, bali aliwasilisha mfano mzuri akiwasimamisha wanachama wa Simba SC upande wa mwanamke anayetongozwa na mgombea upande wa mwanaume mtongozaji.

  Ni mfano tu, naamini hata wanachama na wapenzi wa Simba SC wanajua Julio hakulenga kuwadhalilisha wala kuwakashifu, bali alikuwa anatoa mfano kulingana na hali halisi.
  Mwanaume anayetongoza mwanamke, kuna mawili ama kukubaliwa au kukataliwa na Julio alikuwa anamaanisha yuko tayari kwa lolote, kupata au kuukosa uongozi.
  Lakini pia, katika dunia ya leo kuna wanaume wa tofauti ambao wote humuhitaji mwanamke, kundi moja la wanaume ambao hupenda tu kuwachezea wanawake, na lingine ni lile yenye mapenzi ya dhati.
  Huu ni mtihani mzito mbele ya wanachama wa Simba SC kuelekea uchaguzi wa klabu yao mwishoni mwa mwei ujao, kuweza kuwabaini wagomba wenye mapenzi ya kweli na klabu yao.
  Kuna watu hawana mapenzi ya dhati na Simba SC ila wanataka kuingia madarakani kutimiza malengo ya maslahi binafsi.
  Hawa hawana alama mwili, ila historia zao na klabu vinaweza kuwa vielelezo tosha vya ukweli juu yao.
   Mwenyekiti wa Friends Of Simba (F.O.S.), Zacharia Hans Poppe aliwaasa wanachama wa Simba SC wahakikishe wanachagua viongozi wazuri katika uchaguzi wa klabu hiyo Juni 29, mwaka huu, vinginevyo hatakuwa tayari kushirikia na viongozi wasiofaa.
  “Na siyo mimi tu, kuna wafadhili wengine sita nimewapata ambao wamekubali kuisaidia Simba SC, iwapo tu uchaguzi wa mwezi ujao utazalisha viongozi bora wenye kuaminika,” amesema Hans Poppe akizungumza na BIN ZUBEIRY  wiki hii.
  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kwamba baada ya miaka minne ya kuvumilia kufanya chini ya uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage, hatakuwa tayari kupoteza muda na fedha zake kwa mara nyingine kwa kuwasaidia viongozi wengine bomu iwapo watachaguliwa.
  “Tunapoteza muda wetu, tunajitolea kwa hali na mali kuisaidia Simba SC, lakini inapotokea klabu inakuwa na viongozi wa ovyo, yote hayo yanakuwa kazi bure.
  Sasa napenda nichukue fursa hii kuwaasa, wanachama wenzangu wa Simba SC, wawe makini safari hii kuhakikisha wanachagua viongozi bora, ili tuweze kurudisha zama za heshima ndani ya klabu yetu,”amesema.
  Poppe amesema kwamba kuanzia msimu ujao ushindani utaongezeka katika soka ya Tanzania kutokana na timu nyingi kuja juu, hivyo Simba SC inapaswa kuwa imara sana chini ya viongozi bora ili kuweza kuhimili vishindo vya ushindani.
  “Hatutakiwi kufanya mzaha hata kidogo, tuweke mbele maslahi ya Simba SC na wote tuamue kwa manufaa ya Simba SC, tuonyeshe mapenzi yetu ya dhati kwa klabu kwa kuchagua viongozi bora, watakaoirudishia klabu hadhi yake,”amesema. 
  Poppe amewataka Simba SC watumie kura zao vizuri kwa kuchagua viongozi makini kuanzia nafasi za Ujumbe, Makamu wa Rais na Rais ili kuhakikisha klabu inakuwa katika mikono salama.
  “Achaguliwe mtu ambaye ana sapoti, anakubalika, ana historia na Simba SC, huko nyuma amewahi kuisaidia timu, siyo mtu ambaye anaibuka tu kuja kuomba uongozi, wakati hana rekodi za kusaidia timu.
  Lazima sana tuwe makini na tuwatathmini watu wanaokuja kutuomba uongozi, historia zao, siyo watu wa migogoro, hawana kashfa za ubadhirifu, wanashirikiana vizuri na wenzao na wana mapenzi ya dhati na Simba,”amesema Poppe.
  Kwa sasa Poppe mbali na kuwa Mwenyekiti wa F.O.S., pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo chini ya uongozi wa sasa wa Alhaj Rage unaomaliza muda wake.
  Poppe amekuwa mhimili muhimu mno ndani ya Simba SC kwa zaidi ya miaka mitano sasa akiisaidia kwa hali na mali klabu hiyo na wazi iwapo atarudisha mkono wake nyuma, klabu hiyo itayumba.
  Naamini kwa wenye mapenzi ya dhati na Simba SC  watakuwa wamewaelewa  Julio na Poppe kuelekea mchezo huo.
  Ukweli ni kwamba wanachama wa Simba SC wanatakiwa kuwa makini mno katika uchgauzi, ili kuhakikisha wanachgua viongozi bora na si bora vongozi. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NIMEWAELEWA SANA HANS POPPE NA JULIO, NANI MWENYE MAPENZI YA DHATI NA SIMBA SC? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top