• HABARI MPYA

  Sunday, May 25, 2014

  AL AHLY BENGHAZI, ZAMALEK ZAANZA KUSHINDA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA

  Na Princess Asia, TUNIS
  TIMU za Ahly Benghazi na Zamalek zimepata ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana na kufufua matumaini ya kunyakuwa ubingwa mwisho wa mashindano hayo.
  Ahly Benghazi ya Libya imeifunga Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia mabao 3-2 katika mchezo wa Kundi B mjini Sfax, Tunisia hicho kikiwa kipigo cha pili mfululizo kwa timu hiyo ya Tunisia katika hatua hii ya makundi, wakati Zamalek imeilaza 2-1 Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa Kundi A mjini Cairo.

  Matokeo hayo yanaipeleka Esperance mkiani mwa kundi hilo baada ya kushindwa kupata japo pointi moja katika mechi mbili na kipigo hicho kinazidi kumuweka pabaya kocha Mholanzi, Ruud Krol.
  Walibya walipata bao la kwanza dakika ya tano kupitia kwa nyota wake Mzimbabwe, Edward Sadomba kabla ya Farag Mbarak kufunga la pili dakika saba baadaye.
  Mabingwa mara mbili Afrika, Esperance walirudisha bao moja kupitia kwa Ahmed Akaichi, lakini Mnigeria Moses Orkuma akaifungia bao la tatu timu ya Libya kabla ya mapumziko. Esperance ilipata bao la pili kupitia kwa Oussama Darragi dakika ya 78.
  Ahly Benghazi sasa ina pointi tatu sawa na CS Sfaxien ambayo leo inacheza Setif.
  Mjini Cairo, Mohamed Abdel Shafy alifunga  ao la dakika za jioni kuihakikishia ushindi wa kwanza Zamalek katika hatua ya makundi. 
  Dominique da Silva aliwafungia ‘White Knights’ dakika ya tano bao la kwanza kabla ya mshambuliaji wa Hilal, Mudathir Eltaieb ‘Careca’ kutumia vizuri makosa ya Yasser Ibrahim kumzunguka Abdel Wahed na kusukuma mpora nyabuni.
  Zamalek ilipata bao lake la ushindi dakika ya 81 kupitia kwa Abdel Shafy  na sasa inalingana kwa pointi na Hilal na AS Vita Club, ambayo leo baadaye itamenyana na ndugu zao, TP Mazembe mjini Lubumbashi.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AL AHLY BENGHAZI, ZAMALEK ZAANZA KUSHINDA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top