• HABARI MPYA

    Tuesday, May 27, 2014

    TP MAZEMBE WAIKAUSHIA TFF KUHUSU SAMATTA NA ULIMWENGU KUJA KUCHEZA MECHI YA MARUDIANO NA ZIMBABWE

    Na Mahmoud ZubeIry, DAR ES SALAAM
    WASHAMBULIAJI wawili wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu huenda wasipatikane kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Zimbabwe Juni 1 mjini Harare hatua za awali Kombe la Mataifa ya Afrika.
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wametuma barua kwa klabu yao, TP Mazembe kuwaomba kwa ajili ya mchezo huo, lakini hawajajibiwa.
    Hatihati; Thomas Ulimwengu na mwenzake Mbwana Samatta chini huenda wasipatikanate kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Zimbabwe

    “Tulituma barua, lakini tunasikitika hadi sasa hatujajibiwa na hatujui hatima ya wachezaji hao, ila kwa vyovyote tunajipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo hata bila ya wao,”alisema Malinzi.
    Wachezaji hao wa Tout Puissant Mazembe ya DRC walikuja katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kugombea tiketi ya AFCON 2015 nchini Morocco Taifa Stars ikishinda 1-0 wiki iliyopita.
    Juzi walikuwa wana mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika nyumbani Lubumbashi dhidi ya AS Vita ya Kinshasa na Samatta akafunga bao pekee la ushindi.
    Mazembe watakuwa na mchezo mwingine Juni 7 dhidi ya Zamalek ya Misri wakicheza nyumbani tena, Lubumbashi na wikiendi hii hawatakuwa na mchezo- maana yake hawataathirika kuwaruhusu nyota hao kuja kuitumikia nchi yao.
    Lakini baada ya kufungwa mechi moja na kushinda moja katika Kundi lake A Ligi ya Mabingwa Afrika, Mazembe inaweza kuhitaji kuwa na maandalizi mazuri ya pamoja na wachezaji wake wote kwa ajili ya mechi na Zamalek.
    Kama itakuwa hivyo, basi Taifa Stars itawakosa wachezaji wake hao muhimu katika mchezo huo mgumu, ambao watakuwa na jukumu la kulinda ushindi mwembamba wa 1-0 ulitokana na bao la John Bocco wa Azam FC. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TP MAZEMBE WAIKAUSHIA TFF KUHUSU SAMATTA NA ULIMWENGU KUJA KUCHEZA MECHI YA MARUDIANO NA ZIMBABWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top