• HABARI MPYA

  Friday, May 30, 2014

  RAGE AFUNGUKA MAMBO MAZITO BUNGENI, MENGI YA MAANA, MTU MZIMA YUKO SAWA!

  Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ameikosoa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kutaka ifanyiwe marekebisho ili iendane na mabadiliko ya ulimwengu wa michezo.
  Akichangia Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyowasilishwa Bungeni mjini Dodoma jana asubuhi, Rage alisema Sheria ya BMT imepitwa na wakati kwa sababu ina vitu vingi ambavyo vinavyozungumzia enzi za ujima ambazo kwa sasa havipo.
  "Ipo Sheria ya BMT ya mwaka 1967 ambayo kwa mara ya mwisho ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 1971. Vitu vingi vilivyomo kwenye Sheria hiyo vimepitwa na wakati. Mfano, inazungumzia kuwania uongozi lazima uwe mwanachama wa TANU, chama ambacho kwa sasa hakipo," amesema Rage.
  Aidha, Rage ametumiwa fursa hiyo kuwaomba wanachama na wapenzi wa Simba watulie kipindi hiki ambacho klabu hiyo iko katika mchakato wa uchaguzi mkuu.
  "Ninawaomba wanachama wa Simba watulie katika kipindi hiki cha kusaka viongozi wapya ili masuala yote yanayohusu  mchakato wa uchaguzi mkuu yashughulikiwe kwa misingi na taratibu zilizopo za mpira wa miguu," amesema Rage.
  Mtu mzima yuko sawa; Muheshimiwa Rage amefunguka mambo mazito Bungeni

  WANAOPELEKA SOKA MAHAKAMANI WASIRUHUSIWE KUGOMBEA
  Katika hatua nyingine, Rage, ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini (CCM) amelitaka BMT kuhakikisha linakuwa na kipengele katika Katiba yake inayokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia.
  "Ukiangalia Katiba za TFF, CAF na FIFA zinakataza masuala ya soka kuingiliwa na serikali na kupelekwa katika mahakama za kiraia. BMT iwe na kifungu cha sheria kinachokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia ili iende sanjari na Katiba za mashirikisho hayo," amesema Rage.  Huyu vipi? Mgombea Urais wa Simba SC, Michael Wambura akikabidhi fedha za kukata rufaa kwa Danny Msangi, Mkurugenzi wa Fedha wa TFF kwenye ofisi za shirikisho hilo leo baada ya kuenguliwa katika uchaguzi kwa sababu aliipeleka klabu hiyo mahakamani.

  ZANZIBAR WASAHAU UANACHAMA FIFA 
  Rage, ambaye anamaliza muda wake wa miaka minne wa kuiongoza Simba Juni 29, mwaka huu tangu aingie rasmi madarakani Mei 10, 2010, amewataka Wazanzibar kutopoteza muda wa kusaka uanachama FIFA kwa vile suala hilo ni sawa na ndoto za mchana.
  "Wanachama wote wa FIFA, isipokuwa zile nchi maalum kisoka za Scoatland na Wales, ni wanachama wa UN (Umoja wa Mataifa). Zanzibar si mwanachama wa UN, hivyo hawezi kuwa mwanachama wa FIFA. Nimeamua kulisema hili mapema ili Waziri asisumbuke kuulizwa maswali juu ya hatua iliyofikiwa ya Zanzibar kusaka uanachama katika shirikisho hilo la soka la kimataifa," amesema zaidi Rage.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAGE AFUNGUKA MAMBO MAZITO BUNGENI, MENGI YA MAANA, MTU MZIMA YUKO SAWA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top