• HABARI MPYA

  Wednesday, May 28, 2014

  NDUMBARO ALITAJA JINA LANGU MARA 16 NDANI YA DAKIKA 40, ALIKUWA ANA HASIRA NA MIMI- WAMBURA

  Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM 
  MICHAEL Wambura, mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Simba aliyeondolewa kugombea na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, amesema atakata rufaa katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupinga maamuzi ya kuenguliwa kwake.
  Wambura, katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF) jana aliondolewa kushiriki uchaguzi na kamati hiyo inayooongozwa na daktari wa sheria, Damas Ndumbaro kwa kuwa si mwanachama kwa maelezo kuwa alisimamishwa rasmi uanachama na Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jijini Dar es Salaam Mei 5, 2010 baada ya kupeleka kesi ya soka katika mahakama za kiraia.
  Michael Wambura amejibu mapigo ya Ndumbaro

  Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mchana, Wambura amesema kesho saa 5 asubuhi atatinga kwenye Ofisi za TFF zilizopo katika ghorofa ya 3 ya jengo la PPF, Posta jijini Dar es Salaam kuwasilisha rufaa yake kwa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya shirikisho hilo kupinga maamuzi yote ya kamati ya Ndumbaro dhidi yake.
  "Nimeenguliwa kugombea kwa sababu ambazo si za kweli. Mimi ni mwanachama halali wa Simba kwa sababu tangu 2010 wanayodai nilisimamisha uanachama, sijawhi kupata barua ya kusimamishwa na nimekuwa nikishiriki mikutano yote ya wanachama wa Simba na kulipia ada ya uanachama wangu," amesema Wambura.
  "Nimeshangazwa sana na maamuzi ya kamati ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, mtu anapoteza uanachama wa klabu baada ya kushindwa kulipa ada ya uanachama, kifo au kufukuzwa na mkutano mkuu wa klabu.
  Wambura 16; Dk Ndumbaro kulia akizungumza jana wakati wa kuelezea kuondolewa kwa Wambura uchaguzi wa Simba

  "Inashangaza kuona daktari ya sheria anahukumu kesi kwa kutamka jina la mtuhumiwa mara 16. Jina langu limetajwa mara 16 ndani ya dakika 40. Michael Wambura... Michael Wambura... Hii inaonyesha kwamba alikuwa na hasira nyingi dhidi yangu.
  "Hata walioniwekea pingamizi, wengi wao wanatoka Tawi la Mpira Pesa ambalo limeshafutiwa uanachama. Kuna watu wanataka waweke mtu wao ili awafichie mambo yao. Wameuza gazeti la Simba, wametujengea jengo bovu.
  "Mkutano unaosemwa ulinifukuza uanachama, ulikuwa batili kwa sababu haukuitishwa na mwenyekiti wa Simba na wajumbe saba akiwamo Mwenyekiti Hassan Dalali hakuhudhuria lakini saini za wajumbe hao ziligushiwa kwamba walihudhuria.
  "Mimi nimeshiriki kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba na kuteua wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi kama mjumbe wa Kamati ya Utendaji. Wanaposema mimi si mwanachama halali, basi waukatae hata uteuzi wao kuwa wajumbe wa kamati ya uchaguzi kwa sababu umefanywa na watu ambao si halali.
  "Nilitegemea wajumbe wa kamati hiyo wangelikataa uteuzi au kujiuzulu baada ya kubaini hilo. Inakuwaje unakataa kula nyama lakini mchuzi wake unakula?" Alihoji Wambura.
  Kuhusu barua zenye utata ambazo Ndumbaro alizieleza kwa waandishi wa habari jana, Wambura amesema aliandika barua nyingi za kuomba ufafanuzi juu ya uhalali wake wakati akienguliwa katika chaguzi mbalimbali zikiwamo za Simba, TFF na Mara lakini akasisitiza kuwa 'suala hilo litaelezwa kwa kina kwenye rufaa inayopelekwa TFF."
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDUMBARO ALITAJA JINA LANGU MARA 16 NDANI YA DAKIKA 40, ALIKUWA ANA HASIRA NA MIMI- WAMBURA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top