• HABARI MPYA

    Wednesday, May 28, 2014

    MALINZI AAPA KWA JINA LA MUNGU; “NIKIMGUNDUA MTU ANATOA RUSHWA, WALLAHI ATANITAMBUA MIMI NANI”

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameapa kwa jina la Mungu, kwamba akimgundua mtu anatoa rushwa kupanga matokeo katika mashindano yoyote chini ya utawala wake, ajuta kuzaliwa.
    Akizungumza usiku wa jana ukumbi wa Golden Jubilee Tower, Mtaa wa Ohiao, Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa tuzo na zawadi washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Malinzi alisema ligi hiyo imetawaliwa rushwa.
    Malinzi aliwashutumu marefa kwamba wanahongwa mno na wamejisahau kiasi kwamba msimu unapoanza wanaanza kupanga bajeti za matumizi makubwa kwa kutegemea rushwa.
    Wallahi atanitambua; Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza jana katika tuzo za washindi wa Ligi Kuu

    Hata hivyo, Malinzi amesema; “Ila nasema, siku nikimgundua mtu anayetoa rushwa katika soka ya nchi hii, wallahi (haki ya Mungu) atanitambua mimi ni nani, nasema atajuta kunifahamu,”.
    Malinzi amewaasa viongozi wa klabu baada ya kusajili wachezaji wa gharama kubwa, basi waachane na desturi ya kuhonga marefa, kwani inaharibu soka ya Tanzania.
    Malinzi aliwapongeza mabingwa wapya wa Ligi Kuu, Azam FC waliowapiku waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili msimu huu.
    Pamoja na hayo, Malinzi ametoa changamoto kwa wadhamini wa ligi hiyo, Vodacom Tanzania kuboresha udhamini wao na akasema anafurahi atakuwa na kikao nao hivi karibuni kuzungumzia suala hilo.
    Katika sherehe za utoaji wa tuzo hizo usiku wa jana, mshambulaji wa Azam FC kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 akiwapiku Anthony Matogolo wa Mbeya City na Lugano Mwangama wa Prisons.
    Kwa ushindi huo, Kipre amezawadiwa kitita cha Sh. Milioni 5.2, wakati kipa wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Sharrif ‘Cassilas’ ameshinda tuzo ya mlinda mlango bora wa Ligi Kuu akiwapiku David Burhan wa Mbeya City na Beno Kakolanya. 
    Juma Mwambusi Mwambusi wa Mbeya City, alishinda tuzo kocha bora, akiwaangusha Charles Boniface Mkwasa wa Yanga SC na Mecky Mexime wa Mtibwa Sugar na kupewa Sh. Milioni 5.2. 
    Refa Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam ameibuka mwamuzi bora akilamba Sh. milioni 7.8 baada ya kuwabwaga Isihaka Shirikisho wa Tanga na Jonasia Rukia wa Kagera walioingia kwenye kipengele hicho.  
    Tuzo ya Mfungaji bora wa msimu ilikwenda kwa mshambuliaji wa Simba, Mrundi Amisi Tambwe.
    Tambwe aliyefunga magoli 19, alizawadiwa Sh. milioni 5.2.
    Tambwe aliwashinda Elias Maguri wa Ruvu Shooting, Kipre Tchetce wa Azam FC wote mabao 13, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza wote wa Yanga SC ambao wote walifunga mabao 12 kila mmoja. 
    Yanga SC imeibuka timu yenye nidhamu kwa mara nyingine baada ya kutwaa tuzo hiyo pia msimu wa 2012/13 wa Ligi Kuu na kuzawadiwa Sh. Milioni 16 ikizipiku Azam FC na JKT Oljoro.
    Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na Sh. milioni 75 iliyokwenda kwa Azam FC waliotwaa ubingwa, Yanga SC Sh. milioni 35, Mbeya City Sh. milioni 26 na Simba SC Sh. 21.
    Hakukuwa na mchezaji hata mmoja kati ya walioshinda tuzo zao kutokana na wachezaji hao kuwa mapumzikoni baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu na wote walipokelewa tuzo zao.
    Juma Mwambusi yuko Sudan na timu yake wakishirki michuano ya Nile Basin, naye alipokelewa tuzo yake na Katibu Mkuu wake, Emmanuel Kimbe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI AAPA KWA JINA LA MUNGU; “NIKIMGUNDUA MTU ANATOA RUSHWA, WALLAHI ATANITAMBUA MIMI NANI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top