• HABARI MPYA

  Friday, May 30, 2014

  SIMBA YANGA ZALA DILI LA BENKI, SERIKALI YAONYA WAHUNI WALETA VURUMAI KLABUNI

  Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
  SERIKALI imetoa onyo kali kwa wapenzi na wanachama wa klabu kongwe nchini Simba na Yanga wanaoendekeza fujo na uhuni wakati huu ambao klabu hizo ziko katika michakato ya kuapata viongozi wapya.
  Aidha, serikali imewataka viongozi wa klabu hizo zilizoanzishwa 1935 na 1936 kuhakikisha wanamaliza migogoro inayoendelea kwa sasa ili kurejesha amani ya michezo nchini.
  Mwenyekiti wa Simba SC, Ahaj Ismail Aden Rage kushoto akipokwa Mkataba wa makubaliano yao na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi. katikati ni Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia.

  Katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa hafla ya uzinduzi wa akaunti maalum kwa ajili ya mashabiki na wanachama wa Simba na Yanga kwenye ukumbi wa Hyatt Regency, Dar es Salaam muda mfupi uliopita, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, ameonya tabia za vurugu na uhuni unaofanywa na baadhi ya wapenzi wa klabu hizo huku akitaka kufanyike jitihada shadidi kurejesha utulivu.
  "Moja ya vitu vinavyokera kwenye tasnia ya michezo ni migogoro ya klabu. Na migogoro hii haifanywi na wachezaji bali viongozi wa klabu kwa manufaa yao binafsi," amesema Nkamia.
  "Kuna desturi imejengeka kwamba kuwa kiongozi wa Simba au Yanga kwa sasa ni dili. Simba sasa wameanza vurugu katika mchakato wa uchaguzi wao. Wamefunga mlango wa ofisi zao. Kwa niaba ya serikali, ninawaomba viongozi wahakikishe wa Simba warejesha utulivu kipindi hiki cha uchaguzi.
  "Simba na Yanga ni timu kongwe nchini na zimekuwa zikitoa wachezaji wengi wa timu ya taifa. Kuibuka kwa migogoro na fujo ndani ya klabu hizo kuna athari kubwa hata kwa timu ya taifa na soka la Tanzania kwa ujumla," amesema zaidi kiongozi huyo.
  Nkamia pia ameipongeza Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kuwa anaamini maamuzi hayo ni hatua kubwa katika kuzisaidia klabu hizo kimapato na kurahisha kazi ya kutambua idadi ya wanachama wa klabu hizo na michango yao.
  Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TPB, Sabasaba Moshingi amesema lengo kuu la kuanzisha akaunti hizo ni kuziwezesha klabu hizo mbili kuongeza kipato na kurahisisha kazi ya viongozi wa klabu hiyo kuwafahamu wanachama walio hai na mashabiki wao.
  Amesema kadi hizo zitawawezesha wanachama kuingia katika mikutano yote ya klabu hizo na kwamba zitakuwa za aina mbili; za wanachama wa kawaida na wanachama wakubwa (VIP).
  "Simba na Yanga ni klabu kongwe nchini kwa maana zipo tangu miaka ya 1930 lakini bado zinakabiliwa na changamoto ya kiuchumi. Tumeona tuanzishe utaratibu huu kujitegemea kifedha kupitia michango ya wanachama wake," amesema Moshingi.
  Ismail Aden Rage, Rais wa Simba, amesema kuanzishwa kwa akaunti hizo kutaisaidia klabu yake kujiendesha pasipo kutegemea wanachama wake wenye majina makubwa.
  "TPB kwa kuanzisha akaunti hii watatusaidia kuondoka na utaratibu wa kutegemea fedha za watu wanaojigeuza miunguwatu ili waabudiwe," amesema Rage.
  "Kama nilivyoahidi katika uongozi wangu, nitaachia Simba uwanja. Juni 21 nitakadhiwa uwanja wenye magoli na wenzetu wa TPB wametuahidi kutujengea hosteli ili wachezaji wetu waondokane na utaratibu wa kuweka kambi kwenye hoteli. 
  "Kadi hizi za uanachama za Simba zinazotolewa na TPB zitarahisha usajili wa wanacha wetu kwa sababu watajisajili kwa siku moja na kupewa kadi yao muda huo huo. Hakuna mkombozi wa Simba kwa sasa zaidi ya Benki ya Posta Tanzania." amesema zaidi Rage.
  Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga naye akipokea Mkataba

  Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amesema upinzani uliopo kati yao na Simba ni wa uwanjani tu na wataendelea kushirikiana katika masuala mengine yote ya nje ya uwanja likiwamo la kujikwamua kiuchumi.
  Baadhi ya viongozi wa michezo waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Michael Wambura, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu na Katibu wa Simba, Ezekiel Kamwaga. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YANGA ZALA DILI LA BENKI, SERIKALI YAONYA WAHUNI WALETA VURUMAI KLABUNI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top