• HABARI MPYA

    Sunday, May 25, 2014

    DIDA: SIJUI HATIMA YANGU YANGA SC

    Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
    KIPA chaguo la kwanza kwa Yanga kwa sasa Deogratius Munishi 'Dida' amesema hana uhakika wa kuendelea kubaki Yanga baada ya mkataba wake kumalizika kutokana na kasumba iliyoibuka ya kutokuwa na imani na wachezaji pindi timu inapofanya vibaya.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu leo mchana akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa (Taifa Stas) iliyopo Tukuyu jijini Mbeya, Dida aliyejiunga na Yanga mwaka jana akitokea Azam FC, alisema hana uhakika wa kuendelea kuvaa uzi wa njano na kijani wa Yanga baada ya mkataba wake wa miaka miwili na 'watoto wa Jangwani' kumalizika.
    Sijui hatima yangu; Kipa Deo Munishi 'Dida' amesema hana uhakika wa kubaki Yanga SC baada ya kumaliza Mkataba wake

    "Kwa sasa bado nina mwaka mmoja wa kuitumikia Yanga lakini baada ya hapo sijui nitakakokuwa. Nitakuwa katika kipindi kizuri zaidi cha kuzungumzia hatma yangu baada ya kumalizika kwa mkataba," amesema Dida na kuongeza:
    "Kuna mambo mengi yanayojiri ndani ya klabu na sina uhakika kama Wanayanga watakuwa na hamu na mimi baada ya msimu ujao maana siku hizi ukiharibu mara moja wanakuhukumu na kusahau mazuri yote uliyofanya."
    Licha ya kufanya vizuri ligi kuu na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Dida amesema hakuna kiongozi hata mmoja wa Yanga ambaye amemfuata kwa lengo la kuzungumza juu ya kuongeza mkataba mwingine.
    Dida, akiwa ni mchezaji huru baada ya kumalizana na Azam FC waliomsimamisha kwa tuhuma za rushwa msimu wa 2012/13, alijiunga na Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili Juni 27, mwaka jana kwa mapendekezo ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mholanzi Ernie Brandts.
    Akiwa na kikosi cha Yanga, kipa huyo hata hivyo, alilazimika kusugua benchi kwa muda mrefu hadi kipa mwenzake Ali Mustafa 'Barthez' alipoharibu baada ya kufungwa magoli matatu katika sare ya maajabu ya 3-3 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 20 mwaka jana.
    Baada ya Barthez kufanya kile ambacho kimetafsiriwa na Wanayanga kwamba ni kucheza chini ya kiwango, uongozi wa Yanga uliamua kumsajili kipa mkongwe Juma Kaseja aliyetokea Simba SC.
    Dida amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Yanga akimpiku Kaseja aliyesajiliwa katika kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu huu.
    Kipa huyo mwenye umri wa miaka 25 pia ni mlinda mlango chaguo la kwanza kwa benchi la ufundi la Stars. Aishi Manula wa Azam FC ndiye kipa chaguo la pili kwa benchi hilo linaloongozwa na kocha mpya Mholanzi Mart Nooij.
    Dida aliyezaliwa Aprili 6, mwaka 1989, awali akipiga kazi Manyema Rangers, Simba SC, Mtibwa Sugar na Azam na pia amewahi kucheza soka ya kulipwa Oman.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DIDA: SIJUI HATIMA YANGU YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top