• HABARI MPYA

    Saturday, May 24, 2014

    NI REAL AU ATLETICO KUPELEKA MWALI WA LIGI YA MABINGWA MADRID?

    Na Juma Pinto, LISBON
    ‘MWALI’ wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu anatarajiwa kumpata mwenyewe usiku wa leo katika fainali itakayopigwa Uwanja wa Luz mjini Lisbon, Ureno baina ya Real Madrid na Atletico Madrid za Hispania.
    Huo ni mchezo wa kuhitimisha msimu wa 59 wa michuano hiyo mikubwa zaidi ya klabu Ulaya na msimu wa 22 tangu michuano hiyo ianze kutumia jina hilo kutoka Klabu Bingwa ya Ulaya.
    Hii itakuwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo kukutanisha timu kutoka Jiji moja, Madrid.
    Uwanja wa Luz anbao utapokea Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo

    Ikumbukwe mshindi wa mechi hiyo atakutana na  Sevilla, pia ya Hispania mabingwa wa michuano ya pili kwa ukubwa ya UEFA, Europa League katika mechi ya Super Cup ya UEFA.
    Na pia ataingia moja kwa moja Nusu Fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA mwaka huu.
    Real Madrid ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi katika Ligi ya Mabingwa, ikiwa imetwaa mataji tisa. 
    Hispania kwa ujumla ndiyo inaongoza kutoa mabingwa wengi wa michuano hiyo, hadi sasa ikitoa mabingwa 13, ikifuatiwa na England na Italia ambazo kila moja imetoa mabingwa 12. 
    Jumla ya klabu 22 tofauti zimekwishatwaa taji hilo, kati ya hizo 12 zimeshinda Kombe hilo zaidi ya mara moja na tangu michuano hiyo ibadilishwe jina na muundo wake mwaka 1992, hakuna timu iliyoweza kubeba ‘mwali’ mfululizo.
    AC Milan ndiyo ilikuwa timu ya mwisho kutetea taji hilo msimu wa 1989–1990 na Bayern Munich, waliokuwa mabingwa watetezi baada ya kuifunga Borussia Dortmund 2-1 katika fainali mwaka jana, walitolewa katika Nusu Fainali na Real Madrid mwaka huu.
    Bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kujinyakulia kitita cha Euro Milioni 10.5 na mshindi wa pili Euro Milioni 6.5 wakati timu zilizotolewa katika Nusu Fainali, Beyern na Barcelona kila moja itapata Euro Milioni 4.9.
    Shaka hakuna; Cristiano Ronaldo ametua na Real mjini Lisbon akiwa fiti kwa asilimia 100

    Ready? Diego Costa takes part in Atletico Madrid's final training session before the Champions League final
    Yuko tayari? Diego Costa alishiriki mazoezi ya Atletico Madrid jana, ingawa alifanya mazoezi mepesi tu

    UEFA pia hutoa Euro Miloni 2.1 kwa kila timu inayofuzu kwenye Raundi ya awali ya michuano hiyo, Euro Milioni 8.6 kwa zinazoingia hatua ya makundi, wakati timu inayoshinda mechi katika hatua hiyo inapata Euro Milioni 1 na sare Euro 500,000. 
    Timu zinazongia kwenye hatua ya 16 Bora inapata Euro Milioni 3.5 wakati kwa zinazofuzu Robo Fainali zinapata Euro Milioni 3.9. 
    Wakati Real ina mataji tisa iliyoyatwaa misimu ya 
    1956, 1957, 1958, 1959, 1960, 1966, 1998, 2000 na 2002 pamoja na kushika nafasi ya pili mara tatu 1962, 1964 na 1981, Atletico Madrid iliingia fainali mara moja tu mwaka 1974 na kufungwa na Bayern Munich.
    Nyota wa Real, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale waliokuwa majeruhi wote wamepona na wamekuja na timu yao Lisbon tayari kwa kuipigania kupata taji la 10 la michuaho hiyo.
    Mshambuliaji tegemeo wa Atletico Madrid, Diego Costa ambaye ni majeruhi pia mapema wiki hii alipelekwa Serbia kutibiwa na mganga wa kienyeji ili aweze kupona haraka na kucheza.     
    Atletico tayari wameshinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu ikiwazidi kete vigogo wa nchi hiyo Barcelona siku ya mwisho walipotoa nao sare ya 1-1 na Real baada ya kukosa taji la La Liga watakuwa wanajaribu kurejesha heshima katika Ligi ya Mabingwa.  
    Tangu juzi, Jiji la Lisbon limetawaliwa na shamrashamra za mashabiki wa Real na Atletico waliosafiri kutoka Madrid kuja kuzisapoti timu zao.
    Gwiji wa zamani wa Real, Mreno Luis Figo ndiye balozi wa mchezo huo ambaye baadaye anatarajiwa kuwamo katika kikosi cha magwiji wa timu hiyo kitakachofanya ziara Tanzania Agosti mwaka huu.
    Wapenzi wa soka kutoka nchi mbalimbali duniani nao pia wapo hapa wakiwemo Watanzania. Je, ni Real au Atletico atampandisha ndege mwali wa Ligi ya Mabingwa kurejea naye Madrid? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI REAL AU ATLETICO KUPELEKA MWALI WA LIGI YA MABINGWA MADRID? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top