CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Kimelipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuiwezesha timu ya taifa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2025 nchini Morocco.
Kaimu Katibu Mkuu wa TASWA, Imani Makongoro amesema pongezi hizo zinakwenda kwa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, wasaidizi wake na wachezaji wa Taifa Stars.
“Pia tunawapongeza wananchi waliofurika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuiunga mkono Taifa Stars kwa dhati na kuwapa hamasa wachezaji wetu mwanzo hadi mwisho wa mchezo mgumu tulipopambana na Guinea na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 Novemba 19, 2024,” amesema.
Imani Makongoro amesema TASWA inawasihi Watanzania waendelee kuiunga mkono Taifa Stars, kwani safari bado ni ngumu na ndefu.
“Ni vizuri kwa mshikamano ambao tumeonesha hadi tukafanikiwa kuvuka kizingiti na kupata tiketi ya kwenda Morocco tukauendeleza kwa kasi zaidi,”.
“Tunaomba matayarisho kwa fainali za mwakani yaanze mara moja na kila mwenye uwezo ajitokeze kuisaidia Taifa Stars, kwani ushindi wao ni wa kulijengea heshima Taifa letu. Kwa pamoja tutashinda. Heko Taifa Stars,”amesema.
0 comments:
Post a Comment