• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 15, 2009

  TBL: HATUNA MPANGO WA KUJITOA SIMBA SC

  Meneja wa Kilimanjaro Beer, Oscar Shelukindo


  KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imesema kwamba haina mpango wa kuacha kuidhamini Simba ya Dar es Salaam, eti kwa sababu ya malumbano yanayoendelea kwenye klabu hiyo, kwani walipoamua kujitosa kwenye klabu hiyo, walikwishajua kila kitu.
  Akizungumza na bongostaz ofisini kwake jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Oscar Shelukindo alisema kwamba malumbano yanayoendelea kwenye klabu hiyo hayaisumbui kwa chochote TBL na wala hawawezi kuyaingilia.
  “Sisi tuna mkataba na Simba, tunachotazama je, masharti yaliyomo kwenye mkataba wetu yanatekelezwa, mambo mengine tunawaachia wao, hatuwezi kuyaingilia, wakati mwingine malumbano ni demokrasia,”alisema Shelukindo.
  Bosi huyo wa TBL, inayoidhamini Simba kupitia bia ya Kilimanjaro, alisema kwamba wakati wanafikiria kuidhamini klabu hiyo, walijua fika kuna wakati itatokea migogoro jambo ambalo linatokana na mifumo ya uendeshwaji wa klabu zenyewe.
  Alisema kwa sababu hiyo, wao watabakia kufanya shughuli zao kwa kushirikiana na watu wenye dhamana ya klabu hiyo, akimaanisha viongozi waliochaguliwa kihalali kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.
  Hata hivyo, Shelukindo alisistiza kwamba suala la kuajiri Katibu Mtendaji na Mkurugenzi wa Fedha ni muhimu na juu ya hilo watahakikisha wanakula sahani moja na viongozi wa Simba hadi walikamilishe.
  “Hilo suala la hao watendaji wa kuajiriwa ni muhimu, kwa kushirikiana na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) tutahakikisha siyo Simba, hata wapinzani wao wa jadi, Yanga ambao pia tunawadhamini kupitia bia hii (Kilimanjaro Premium Lager), nao wanalitekeleza,”alisema Oscar.
  Tangu kumpoteza mdhamini wake aliyewatoa gizani mwaka 1999 kampuni ya, Mohamed Enterprises Limited (MeTL), klabu kongwe ya soka nchini, Simba imekuwa ikisota kupata wadhamini wengine kabla ya Agosti 18, mwaka 2008 TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro kujitokeza kuokoa jahazi.
  TBL iliingia mkataba na Simba wenye thamani ya Sh. Bilioni 3, utakaodumu kwa miaka mitatu, ikiwa kila mwaka Kilimanjaro itakuwa ikitoa Sh. Bilioni 1, kwa klabu hiyo kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu.
  Mapema tu wakati wa hafla ya uzinduzi wa mkataba huo, iliyofanyika Agosti 18, mwaka 2008 kwenye hoteli ya Movenpick, mjini Dar es Salasam, Kilimanjaro Premium Lager ilitoa hundi ya sh. 25,000,000 kwa klabu hiyo, ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wake.
  Kilimanjaro Premium Lager, pia imetoa udhamini kama huo kwa klabu ya Yanga. Katika mkataba huo, ambao Simba imepewa mabasi mawili Hiece na Coaster, pia inavuna sh. Milioni 16, kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya wachezaji, hiyo ikiwa ni mbali na kupatiwa basi dogo la kusafiria wachezaji.
  Msimu huu pia Simba, kutokana na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, imevuna Sh. Milioni 15 kulingana na mkataba huo, wakati watani wao wa jadi, Yanga waliokuwa mabingwa wamepata Sh. Milioni 25.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TBL: HATUNA MPANGO WA KUJITOA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top