• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 16, 2009

  KIPA MZUNGU AREJEA YANGA LEO

  Hapa nipo na Obren baada ya kuwasili nchini tumkizungumza Uwanja wa ndege wa mwalimu Nyerere.


  KIPA Mzungu wa klabu bingwa ya soka Tanzania, Yanga, Obren Curkovic amewasili leo mjini Dar es Salaam, majira ya saa 9:30 Alasiri kwa ndege ya Shirika la Emirates, akitokea kwao, Serbia alipokwenda tangu Aprili mwaka huu.
  Akizungumza na bongostaz baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Obren alisema amerejea kwenye klabu yake kuendelea kuitumikia.
  “Nimechoka sana, nimesafiri saa nyingi, nataka niende kupumzika, kwa ufupi nimerudi Yanga,”alisema kipa huyo anayefananishwa na mlinda wa Chelsea, Petr Cech raia wa Jamhuri ya Czech kwa ushujaa wake langoni.
  Obren amewasili ili kuwahi kusaini mkataba wa kuendelea kuichezea klabu hiyo, baada ya tofauti zilizokuwapo baina yake na klabu hiyo kumalizwa.
  Mara baada ya kuwasili, Obren alilakiwa na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Emmanuel Mpangala na kupakiwa kwenye gari dogo la klabu hiyo waliyopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
  Kipa huyo aliyekwenda moja kwa moja kwenye Hotel ya Tamal, Mwenge, aliidakia Yanga mechi 10 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kufungwa bao moja tu na Shaaban Kisiga ‘Malone’ katika mechi ambayo timu yake ilishinda 3-1.
  Yanga walimheshimu zaidi kwa umahiri aliounyesha kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya watani wa jadi, Simba ambao timu hiyo ilishinda 1-0 kwa bao pekee la Ben Mwalala aliyepokea pasi ya Boniphace Ambani.
  Obren aliondoka nchini baada ya kukerwa na tuhuma za baadhi ya watu kwamba aliihujumu timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Ahly nchini Misri hadi ikafungwa 3-0.
  Mara tu baada ya mchezo wa marudiano na Waarabu hao, ambao Yanga ilitandikwa tena 1-0, langoni akiwa Juma Kaseja, Obren aliamua kutimkia nyumbani kwao.
  Tuhuma ambazo ziliwahusisha pia makocha wa klabu hiyo, akiwemo Kondic, baadaye zilipuuzwa baada ya kubainika zilipandikizwa na watani wao wa jadi, Simba waliokuwa na lengo la kuwavuruga kisaikolojia kabla ya mchezo baina yao, Aprili 19, mwaka huu.
  Viongozi wawili wa Simba (majina tunayahifadhi) walidaiwa kusafiri na Yanga kwenda Cairo huku kukiwa na madai kwamba wanakwenda kusaidai timu hiyo mbinu za kuwafunga Waarabu, lakini habari nyingine zilidai kwamba walikwenda kufanya hila hizo chafu.
  Uimara wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Wakili Imani Madega kupuuza tuhuma hizo akitaka kwanza uthibitisho ndio azifanyie kazi, ulisaidia kutochafua hali ya hewa ndani ya Yanga.
  Baadhi ya wapenzi na wanachama maarufu wa Yanga walikuwa wakimpigia simu Madega kumshinikiza amuwajibishe Kondic kutokana na tuhuma hizo za kupika, lakini Wakili huyo wa kujitegemea aliweka msisitizo kwamba waliotoa tuhuma hizo watoe uthibitisho.
  Lakini baadaye ilibainika kuwa zilikuwa ni tuhuma za kupika, ambazo zilitengenezwa ili kuwafanya Yanga wavurugane na hadi kufikia mechi ya watano wa jadi, Aprili 19, wawe dhaifu na kufungwa na Simba.
  Baada ya kuona Yanga wameendelea kuwa pamoja, zilianza mbinu nyingine za kuwapigia simu makocha wa klabu hiyo na Obren kuwapa vitisho na kuwataka waondoke kwenye klabu hiyo.
  Kondic alivumilia vitisho hivyo, lakini Obren na kocha kijana Civojnov Serdan walishindwa kuhimili na kuamua kuondoka.
  Hata hivyo, baada ya Kondic kuwapa somo wawili hao, wameamua kwa pamoja kurejea kuendelea na kazi Jangwani.
  Wakati Obren anarejea Yanga, tayari kuna uwezekano mkubwa, makipa wengine walioidakia klabu hiyo msimu huu Juma Kaseja na Stephen Malashi wakaachwa waondoke, kwani wote mikataba yao imekwisha.
  Huenda nafasi za Kaseja na Malashi zikazibwa na makipa kutoka Cameroon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao wanaendelea na majaribio kwenye klabu hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA MZUNGU AREJEA YANGA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top