• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 22, 2009

  ULIKUWA MWAKA WA SIMBA SC...


  UNAPOANZA kuzungumzia makali ya klabu za soka Tanzania, basi Simba itatajwa kama hodari namba moja, kutokana vitu vyake ilivyowahi kufanya kihistoria, kuanzia mwaka 1974.
  Mwaka 1974, kwanza Simba ilianza kwa kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, katika michuano iliyofanyika mjini Dar es Salaam.
  Kama wahenga walisema nyota njema huonekana asubuhi, basi hizo zilikuwa dalili njema kwa Simba kutikisa soka ya Afrika mwaka huo.
  Mwisho wa msimu, Simba iliingia kwenye orodha ya klabu nne bora zaidi barani Afrika, kutokana na kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huo 1974.
  Mwaka huo, Wekundu hao wa Msimbazi walianza Raundi ya Kwanza kwa kumenyana na Linare ya Lesotho na katika mchezo wa kwanza ugenini, waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 kabla na ushindi wa 2-1 nyumbani, hivyo kusonga mbele kwa ujumla ya ushindi wa mabao 5-2.
  Katika Raundi ya pili, Simba ilimenyana na Zambia Army na katika mchezo wa kwanza mjini Lusaka, iliibuka na ushindi wa 2-1 kabla ya kumalizia na ushindi wa 1-0 nyumbani, Dar es Salaam, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.
  Hatimaye Simba ikaingia Robo Fainali ambako ilikutana na Hearts of Oak ya Ghana na kwenye mchezo wa kwanza ugenini Wekundu wa Msimbazi waliustaajabisha ulimwengu kwa kuibuka na ushindi wa 2-1, mabao yakifungwa na Adam Sabu (sasa marehemu) na Abdallah Kibadeni na kwenye marudiano, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana mjini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Simba ilikata tiketi ya kuinga Nusu Fainali, ambako ilikutana na Mehallal El Kubra ya Misri na kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi walishinda bao 1-0 na kwenye marudiano, Waarabu walilipa kisasi cha ushindi wa 1-0.
  Kwa matokeo hayo, mchezo huo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na ndipo Simba ilipong’olewa kwa penalti 3-0. Tena siku hiyo, aliyekuwa kipa wa Simba, Athumani Mambosasa (sasa marehemu) alilalamikwa kupigwa na vitu akiwa langoni, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kuelekeza akili yake vyema kwenye kuokoa michomo ya Waarabu.
  Huu ni kati ya miaka miwili ya kihistoria kwa Simba kwenye soka ya Afrika, mwingine ukiwa ni mwaka 1993, timu hiyo ilipofika fainali ya Kombe la CAF na kufungwa na Stella Abidjan mjini Dar es Salaam 2-0, baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini.
  Kwa nini nimekumbuka vitu hivyo vya Simba mwaka 1974? Ni baada ya kusoma makala moja iliyoandikwa kwenye gazeti la BINGWA toleo la Juni 20, mwaka huu na Mwandishi Mohamed Kuyunga.
  Makala hiyo yenye kichwa cha habari; Tuwalinganishe Tambwe, Victor, Santos na Kondic hakika ilisheheni utumbo mtupu, ni kama mwandishi wa makala hiyo ana jukumu la kuandika kujaza kurasa tu na si kwa minajili ya kitaaluma.
  Ameanza kwa kuikoroga historia ya Dk. Victor Stanslescu alipokuwa nchini miaka ya 1970 katika klabu ya Yanga, lakini amechekesha zaidi aliposema mwaka 1974 Yanga ilicheza na Enugu Rangers katika Klabu Bingwa Afrika.
  Jamani kwa mpenzi wa soka wa Tanzania ambaye hajui hata hili la vitu vya Simba SC katika michuano hiyo ya Afrika mwaka 1974 awekwe kwenye kundi gani?
  Namkumbusha mwandishi wa makala hiyo, funguo za kuwa mwandishi bora kuwa ni; Pata uthibitisho wa uhakika kadiri utakavyoweza kupata (kuhusu habari unayotaka kuandika).
  Wahabarishe wasomaji wako vyanzo vya habari ulipopata habari yako. Kuwa mkweli kwa jambo ambalo hufahamu kuhusu habari hiyo. Usijaribu kuandika kwa kuongeza chumvi kwenye habari yako, la msingi ni kuweka wazi. Daima hakikisha unaandika ukweli,”.
  Hivyo kwa hili la kusema Yanga ilicheza Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974, mwandishi amesema uongo. Kama hajakusudia kusema uongo, basi amefanya hivyo kwa sababu hajui, kama alikuwa hajui alikuwa ana sababu gani ya kuandika?
  Sasa namuelimisha Kuyunga, Yanga ilicheza na Enugu Rangers International ya Nigeria Mei mwaka 1975, ukiwa ni mchezo wa pili wa raundi ya Pili wa Klabu Bingwa Afrika.
  Katika mchezo wa kwanza nchini Nigeria, Yanga ilipigana kiume na kupata sare ya bila kufungana na wenyeji, lakini kwenye marudiano ikiwa inahitaji angalau sare ya bila kufungana ili isonge mbele, ilijikuta ikilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani na kuwaachia simanzi mashabiki wake.
  Kwa kumuelimisha zaidi Kuyunga, Yanga ilifuzu moja kwa moja kucheza na Enugu, baada ya kukosa mpinzani kwenye Raundi ya Kwanza.
  Kila siku nimekuwa nikiwaambia waandishi wenzangu kwenye chumba cha habari (New Habari), waachane na mtindo wa kuandika ili mradi wajaze kurasa, kwani kufanya hivyo ni kuwakosea wasomaji wetu, ambao wengi yao wanajua kuliko sisi.
  Kwa Certificate, Stashahada na Shahada zetu za Uandishi wa Habari, tunawaandikia Wanafalsafa, Maprofesa na Madaktari, dhahiri hawa watu wanajua kuliko sisi, ndio maana Waandishi wa Habari tunahimizwa kusoma zaidi na zaidi, ili kupanua uelewa wetu.
  Najua hakuna malaika miongoni mwetu, hivyo kukosea mara moja moja si jambo la ajabu, lakini inapotokea kukosea ikawa ni kawaida, basi huo udhaifu, hivyo waandishi wa namna hiyo si mfano wa kuigwa hata kidogo.
  Hivyo Kuyunga anapaswa kufahamu nini wajibu wake kama Mwandishi Habari, ili jamii imheshimu na kumuenzi daima.
  Elimu ya darasani ni suala moja, lakini pia kuna uelewa kuhusu michezo yenyewe, hasa soka ambayo Kuyunga anaizungumzia, hali ya kuwa anaonekana mbumbumbu mno katika hilo.
  Kuna magwiji wa historia za soka kuanzia enzi za Gossage na Sunlight Cup kama Kitwana Manara, enzi zake akiitwa Popat, ambaye alianza kama kipa baadaye mshambuliaji na kwa nafasi zote hizo alichezea timu ya taifa ya Tanzania.
  Sijui kati ya Kuyunga na Kitwana Manara nani anajua zaidi kuhusu Dk. Victor na Yanga. Manara alikuwamo kwenye kikosi cha Yanga kilichocheza na Enugu Rangers mwaka 1975.
  Kwa hivyo, Kuyunga anapaswa kujua fika, kabla ya kuandika chochote kwanza vema akafanya utafiti na awe wazi kwa mambo asiyoyajua, vinginevyo ataendelea kujiaibisha kwa wasomaji wenye kuelewa na kuwapotosha wale wasioelewa.
  Mimi sina uelewa wa kutosha kuhusu muziki wa nyumbani wa enzi hizo na historia yake, kwa sababu sikupenda kuifuatilia wakati wa makuzi yangu, nilitekwa na muziki wa Wamarekani hususan Hip hop, hivyo siwezi kuchambua chochote kuhusu Sikinde, Msondo au OSS.
  Lakini kwa soka, mchezo ambao nimeucheza tangu nikiwa shule ya Msingi Mgulani, Dar es Salaam, ndondi mchezo ambao pia nimeucheza tangu shuleni hapo nikiwa na akina Hassan Matumla na mdogo wake, Mbwana Matumla ambao waliendelea nao wakati mimi niliishia njiani, wakati wowote naweza kuuchambua.
  Nimekuwa mpenzi mkubwa wa ndondi na soka katika maisha yangu yote hadi sasa, najua juu ya michezo hiyo na ninaendelea kujifunza kila siku na ndiyo maana makala na habari zangu kuhusu michezo hiyo ni sahihi na hazina mushkeli.
  Lakini kikubwa ninapenda kufanyia kazi iwe habari au makala ninayotaka kuandika, kabla ya kufanya hivyo, ndio maana mara nyingi ninapoteza muda wangu mwingi Makataba Kuu ya Taifa kusoma habari zilizoandikwa miaka ya nyuma kuhusu soka na michezo mingine ninayotaka kuandika kwa undani.
  Labda iwe Kuyunga ana ajenda ya kutaka kumchafua tu Kondic, tu kwa sababu hataki awe kocha wa Yanga au ametumwa na watu wasiomtaka kocha huyo, lakini kwa kuandikwa kwa sababu ya hoja, Kuyunga hana lolote. Ndiyo maana namuambia mwaka 1974 ni Simba SC iliyoshiriki Klabu Bingwa Afrika hadi kufika Nusu Fainali na kutolewa kwa penalti na Mehalla El Kubra.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIKUWA MWAKA WA SIMBA SC... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top