• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 16, 2009

  MAJIBU YA KUYUNGA KUHUSU SHUTUMA ZAKE KWA KOCHA WA YANGA...

  Profesa Kondic ni zaidi ya kocha…

  na mahmoud zubeiry
  NIMESOMA gazeti la BINGWA toleo la jana, na makala moja ikaniteka zaidi ya nyingine nikaamua kuisoma kuanzia mwanzo hadi mwisho. Makala hiyo iliandikwa na mwandishi Mohammed Kuyunga akimchambua kocha wa Yanga, Profesa Dusan Kondic, chini ya kichwa cha habari; Kondic kocha, wakala au muua vipaji?
  Kuyunga ameanza kwa kusimulia historia zake binafsi alipokuwa anasafiri kwenda Kigamboni ambako alikutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ramadhani Nassib.
  Kuyumba amesimulia kwamba Nassib alimwaga sifa nyingi kwa Kondic, akiwa na imani kwamba ataifikisha mbali klabu hiyo.
  Baada ya kuelezea kwa muhtasari wasifu wa Kondic kulingana na ufahamu wake, Kuyunga sasa akaanza kumchambua kocha huyo bora wa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara. Kwa faida ya wasomaji wetu, ningependa kuweka sawia baadhi ya mambo aliyoyaandika mwandishi huyo.

  Ugomvi na Maximo:
  “Ikumbukwe kuwa Kondic ameachiwa uhuru wa kusajili wachezaji katika Yanga na ana uwezo wa kumleta mchezaji yeyote katika timu hiyo, kwa hiyo mbali ya kutofautiana na Maximo kuhusu muda unaotumiwa na wachezaji wake kuwa Stars, Kondic pia aliwahi kulalamika Maximo anachukua wachezaji wengi kutoka Yanga.
  Lakini labda kocha huyu alikuwa amesahau, kuwa ni yeye aliyesajili wachezaji wengi baada ya kuwaona wakiwa na timu ya taifa, akina Jerson Tegete, Geoffrey Boniphace, Vincent Barnabas na Kiggi Makasy. Wote hawa amewatoa Stars,”.
  Naam, hicho ndio kipengele cha kwanza Kuyunga.
  Awali ya yote Kuyunga, anapaswa kufahamu kwamba, kocha yeyote mtaalamu, hatapenda kuingiliwa katika kuunda timu yake, lazima atasajili mwenyewe kwa matakwa yake. Hivyo uhuru aliopewa Kondic ni sahihi.
  Kuyunga amemsingizia Kondic kwamba aliwahi kugombana na Maximo, siyo kweli, kocha wa Yanga aliyewahi kugombana na kocha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni Milutin Sredojevic ‘Micho’ wakigombea wachezaji.
  Micho aligombana na Maximo mbele ya Sunday Kayuni, Mserbia huyo akiwataka wachezaji wa Yanga waliopo Stars aende nao kambini Afrika Kusini na kocha wa timu ya taifa akisitiza wabaki kambini kujiandaa na wenzao.
  Ukweli ni kwamba Kondic aliwahi kulalamikia mfumo wa Maximo kuwahodhi wachezaji wa klabu kwa muda mrefu, akimtaka afuate kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambazo zinaelekeza kuwa mchezaji anapaswa kujiunga na timu ya taifa saa 48 kabla ya mchezo, ambao wa kirafiki unatambuliwa na FIFA.
  Mechi za kuwania kufuzu mchezaji anatakiwa aruhusiwe siku nne kabla, ikiwemo siku ya mchezo wenyewe na inaweza ikawa siku tano, iwapo mchezaji atalazimika kusafiri kutoka bara moja hadi lingine.
  Aidha, kuelekea fainali za michuano mikubwa kama CAN, Kombe la Dunia, Mabara klabu inapaswa kumuachia mchezaji anagalau wiki mbili kabla ya kuanza kwa michuano.
  Lakini Maximo amekuwa akikatisha programu za klabu za kuwachukua wachezaji kwa programu za timu ya taifa wakati mwingine mwezi mzima.
  Kwa sababu ninafahamu sababu za Maximo kufanya hivyo, kubwa ni kwamba klabu nyingi nchini hazina walimu wenye utaalamu wa kutosha kuwapika wachezaji, siwezi kuwa mpinzani katika hili, lakini pia haiondoi ukweli kwamba anakiuka utaratibu.
  Kwa hivyo ninamuambia Kuyunga, Kondic alikuwa sahihi kulalamika juu ya hilo, kwa sababu naye ana majukumu ambayo anahitaji kuyafanya kwa ufanisi.
  Kuhusu kusajili wachezaji kutoka timu ya taifa, Kuyunga anapaswa kufahamu kocha yeyote bora nchini atahitaji wachezaji bora ambao wengi wao tayari wamekwishapata nafasi kwenye timu zao za taifa.
  Arsene Wenger alivutiwa na Kolo Toure alipomuona kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2002 zilizofanyika Mali, wakati huo anachezea ASEC Abidjan ya nyumbani kwao Ivory Coast.
  Ingawa alimsajili kutoka timu ya taifa, lakini leo kocha yeyote wa Ivory Coast anapomuhitaji mchezaji huyo kutoka Arsenal, lazima afuate utaratibu uliowekwa na FIFA, vinginevyo ataingia tu kwenye malumbano na Mfaransa huyo. Hivyo ninambuambia bwana Kuyunga, Kondic yuko sahihi kuchukua wachezaji kutoka timu ya taifa.
  USAJILI WA NJE:
  Kuyunga anasema kwamba baada ya TFF kupitisha kanuni ya klabu kusajili wachezaji 10 wa kigeni kwa ajili ya Ligi Kuu, Kondic alitumia vyema fursa hiyo kwa kusajili wachezaji kama Maurice Sunguti, Boniphace Ambani, Ben Mwalala, George Owino na Mike Barasa, lakini akashindwa kuwapata Joseph Shikokoti na John Njoroge.
  Kuyunga anauliza: “Sijui nani aliyemuambia Kondic kuwa Tanzania kuna tatizo la fullback (mabeki wa pembeni) hadi kuwataka Shikokoti na Njoroge.
  “Hivi hawa jamaa hawaji kuchukua nafasi ya Watanzania wengine kweli katika Yanga? Je, Kondic hayupo pale kwa ajili ya kuua kipaji cha Mtanzania mwenzangu, mdogo wangu Amir Maftah na kummaliza kabisa Shadrack Nsajigwa kweli?”.
  Hakika katika kipengele hiki Kuyunga amechekesha mno, kwanza Sunguti ni mchezaji ambaye kocha huyo alimkuta kikosini na kumaliza msimu kabla ya kuanza msimu mpya. Kuhusu Shikokoti, Yanga walichelewa kuwasilisha usajili wa wachezaji hao TFF na huo ulikuwa uzembe wa kiongozi mmoja, aliyeamua kuweka hati za usajili wa wachezaji kwenye kabati la ofisini kwake badala ya kuzipeleka panapohusika.
  Lakini hao ni wachezaji wa Yanga tangu Desemba mwaka jana, ambao waliachwa wacheze Tusker kwa mkopo.
  Kuhusu mabeki wa pembeni, Kuyunga anaonekana ni mtu ambaye yuko mbali kabisa na soka ya nchi hii, tangu kuondoka kwa Alphonce Modest, Tanzania haijapata tena beki halisi wa kushoto, zaidi makocha wamekuwa wakitoa wachezaji kwenye nafasi nyingine na kuwalazimisha kucheza sehemu hiyo.
  Amir Maftah ni kiungo aliyeanza kurudishwa kwenye nafasi hiyo na Maximo, wakati Mecky Mexime anaeleka kutundika daluga zake. Alipopatikana Juma Jabu, Amir akawa hachezeshwi tena nafasi hiyo Stars.
  Kabla ya hapo, alikuwapo Kassim Issa ‘Bedwi’, wakati wa kocha Mjerumani Burkhad Pape, naye alirudishwa kutoka kiungo hadi beki wa kushoto. Tena aliyeanza kumpanga nafasi hiyo, alikuwa kocha maarufu zamani, Mansour Magram (sasa marehemu), wakati huo akiinoa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
  Tanzania kuna tatizo la mabeki wa pembeni, tena hadi kulia pia, ndio maana hata Freddy Mbuna alitolewa kwenye ushambuliaji hadi beki katika klabu hiyo hiyo ya Yanga, Nassor Masoud ‘Cholo’ na Said Sued, wote hawa walitolewa kwenye nafasi zao za kiungo na kufanywa mabeki Simba.
  Hata huyo Nsajigwa Shadrack, nafasi yake halisi uwanjani ilikuwa ni kiungo na mwaka 2004, aliwahi kuitwa timu ya taifa kama kiungo chini ya Salum Madadi. Hivyo Kuyunga anapaswa kufahamu, nchi ina tatizo la mabeki wa pembeni na Kondic yuko sahihi kuleta mabeki kutoka nje. Ramadhan Wasso, Simba ilimsajili kutoka Burundi, kama ilijua hapa kuna mabeki wa kumwaga, kwa nini ilikubali kuingia gharama za ziada?
  Katika kipengele kingine, Kuyunga anamshutumu Kondic kuwa ameua kipaji cha Mwaikimba kwa kutompa nafasi kabisa kwenye kikosi chake.
  Kuyunga anapaswa kufahamu kwamba, Mwaikimba ni mchezaji ambaye amejimaliza mwenyewe kuanzia timu ya taifa chini ya Maximo na Yanga yenyewe chini ya Micho.
  Kondic ndiye aliyemkingia kifua mchezaji huyo abaki kwenye kikosi cha msimu uliopita baada ya viongozi kutaka kumtupia virago, lakini naye pia ilifika wakati yakamshinda.
  Kwa kumkumbusha Kuyunga, wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, Kondic alithubutu kutomsajili Ben Mwalala na kumpa nafasi Mwaikimba, uamuzi ambao baadaye aliujutia kwani mchezaji huyo aliishia kuchekesha tu.
  Kuyunga anaendelea kusema wachezaji kama Hamisi Yussuf na Vincent Barnabas waliokuwa wakitisha sana waqlipokuwa Kagera Sugar, wote hawa Kondic ameua vipaji vyao.
  Kwanza namsahihisha, Hamisi Yussuf hajawahi kucheza Kagera Sugar, alitokea Rwanda kujiunga na Yanga mwaka 2006. Nianze na Hamisi, huyu ni mchezaji ambaye kutokana na kushuka kiwango chake, alianza kutemwa kwanza na Maximo timu ya taifa.
  Yanga nako, ameshindwa kuwapiku mabeki wengine akina Nadir Haroub ‘Cananvaro’, Wisdom Ndhlovu na George Owino kwa ubora, hivyo kujikuta akiwa mchezaji wa benchi. Hata alipopewa nafasi kwenye mechi mbili tatu, alionekana kabisa kucheza chini ya kiwango.
  Kocha haangalii sura ya mtu, anaangalia soka, ndio maana leo Cannavaro aliyekuwa akiwekwa benchi na Hamisi mwanzoni kuanzia timu ya taifa hadi Yanga, ndiye chaguo la kwanza kote huko.
  Barnabas aliingia Yanga na mguu mbaya, kwanza alianza kuandamwa na majeraha lakini mwishoni mwa msimu uliopita alipona na kuanza kuonyesha cheche zake. Alicheza vizuri na kung’ara kwenye mechi dhidi ya watani wa jadi, Simba.
  Kuyunga anaendelea kusema Credo Mwaipopo aliamua kuondoka Yanga baada ya kuona wageni tu ndio wanapewa nafasi. Credo ambaye ni kiungo, aliondoka Yanga baada ya kuona hawezi kugombea namba na Athumani Iddi ‘Chuji’, Castory Mumbara, Shamte Ally, Abdi Kassim ‘Babbi’, Mrisho Ngassa, Geoffrey Bonny na Kiggi Makasy, wote hawa viungo wenzake wazawa.
  Kwa ufupi, Credo alisoma ishara za nyakati na kuamua kutafuta ustaarabu mwingine.Kwa bahati nzuri au mbaya, msimu uliopita Yanga haikuwa na kiungo mgeni. Sasa hao wageni aliowakimbia Credo ni akina nani?

  KONDIC ANAKUZA VIPAJI:
  Inawezekana hili Kuyunga hajaliona, lakini ukweli ni kwamba Kondic amesaidia vipaji vya wachezaji wengi wa Yanga kupanda kwa mfano Nurdin Bakari aliyekuwa ametemwa na klabu yake Simba, amempandisha hadi amerejeshwa timu ya taifa.
  Razack Khalfan mchezaji wa kikosi cha pili, aliyepandishwa kikosi cha kwanza, naye ameitwa timu ya taifa na Maximo kutoka benchi la wachezaji wa akiba wa Yanga.
  Ambani na Ben Mwalala, wote walikutana na Kondic wakiwa wamefungiwa vioo kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, lakini sasa wamekuwa wakiitwa baada ya soka ya kupanda.
  Kuyunga anasema Kondic anamuweka benchi Jerry Tegete wakati ndiye mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa, si kweli anachofanya Kondic hataki kumchosha mchezaji huyo kwa kumpanga acheze dakika 90 za kila mechi ya Yanga kutokana na umri wake mdogo, anamkomaza taratibu.
  Kuyunga anasema Kondic ni wakala kwa sababu anawatafutia wachezaji wa Yanga nafasi za kucheza nje, hiki nacho ni kichekesho.
  Kondic anachotaka ni kuinufaisha Yanga, unapofikia msimu wa usajili hakuna haja ya klabu kufungua akaunti, bali zitumike fedha ambazo zimepatikana kutokana na kuuza wachezaji na huo mfumo wa kisasa wa uendeshwaji soka duniani kote.
  Leo Ferguson anamuuza Ronaldo, wakati anapiga hesabu za kumnunua Torres. Kama Kondic alitaka kumuuza Laurent Kabanda Ulaya akagoma, basi hiyo ni hasara yake (Kabanda) kwa sababu leo kila mchezaji wa Afrika anaota kucheza Ulaya.
  Kuyunga anasema Kondic anaomba mkataba Yanga kabla huu wa sasa haujamalizika, kwanza habari hizo si za kweli, Yanga na Kondic wamekwishamaliza na ndio maana klabu hiyo imemkabidhi kocha huyo jukumu la kusajili kikosi mcha msimu ujao.
  Kuna habari nyingine zinaibuka kwenye magazeti ni za uzushi mtupu, kama hizi za Kondic kudai mkataba mpya. Kondic ameondoka nchini ameenda Afrika Kusini kushuhudia michuano ya Kombe la Mabara, Juni 22, mwaka huu atakuwa hapa kuendelea na progamu zake.
  Mara nyingi nimekuwa nikizungumza na Profesa Kondic, ni kocha mwenye mipango mingi mizuri inayohusu mfumo mzima wa klabu, ambayo baadaye itainufaisha mno Yanga.
  Hivyo kwa ujumla makala ya Kuyunga haikumtendea haki kocha huyo, ambaye mara nyingi amekuwa akilalamikia baadhi ya waandishi wa habari nchini, kumnukuu wakati hakuzungumza nao na au kwenda kuandika tofauti na alivyozungumza nao.
  Napenda kumkumbusha Kuyunga juu ya funguo za kuwa mwandishi bora kuwa ni;
  Pata uthibitisho wa uhakika kadiri utakavyoweza kupata (kuhusu habari unayotaka kuandika).
  Wahabarishe wasomaji wako vyanzo vya habari ulipopata habari yako.
  Kuwa mkweli kwa jambo ambalo hufahamu kuhusu habari hiyo.
  Usijaribu kuandika kwa kuongeza chumvi kwenye habari yako, la msingi na kuweka wazi. Daima hakikisha unaandika ukweli.
  Naamini, akifuata mwongozo huu, atakuwa mwandishi bora na ataisaidia jamii kupitia taaluma yake, kwani kwa makala yake ya kwenye gazeti la BINGWA jana, dhahiri ameipotosha jamii kwa kumshushia tuhuma zisizo za ukweli Kondic na kueleza mambo bila ya kuwa na uhakika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAJIBU YA KUYUNGA KUHUSU SHUTUMA ZAKE KWA KOCHA WA YANGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top