• HABARI MPYA

    Wednesday, May 07, 2014

    TUNATAKA UTITIRI WA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU, JE SASA TUKO TAYARI?

    NI klabu tatu ndizo zinajua umuhimu wa kuwa na wachezaji wengi wa kigeni katika vikosi vyao, kati ya Klabu zote zaidi ya 30 za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
    Klabu hizo, ni Azam FC, Simba SC na Yanga SC, zote za Dar es Salaam ambazo ndizo zimekuwa washindani wa ubingwa wa Ligi Kuu, inayodhaminiwa na Vodacom.
    Kwa pamoja, Azam FC, Simba na Yanga SC zinaamini haziwezi kufanya vizuri katika michuano ya Afrika bila ya kuwa na wachezaji wengi wa kigeni, zikitazama timu nyingine zinazofanya vizuri huko mfano TP Mazembe ya DRC, zinaundwa na wachezaji wengi wa kigeni.

    Kama DRC ni moja ya nchi zinazoaminika kuwa na wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kucheza soka, lakini klabu yake inayofanya vizuri katika michuano ya Afrika ina wachezaji zaidi ya 10 wa kigeni kikosini, vipi kwa Tanzania?
    Bila shaka huo ndio mtazamo wa wababe wa soka ya nchi hii, Azam, Simba na Yanga SC- lakini ikumbukwe msimu wa 2008-2009 ilipitishwa kanuni ya kusajili wachezaji 10 katika Ligi Kuu na kuwatumia watano kwa wakati mmoja uwanjani, wakati kwenye michuano ya Afrika hakukuwa na kikomo.
    Hata hivyo, Azimio la Bagamoyo mwaka 2007 lilipitisha kwamba kuanzia msimu uliopita idadi ya wachezaji wa kigeni kwa kila klabu iwe wachezaji watatu na kuanzia msimu wa 2009/2010 idadi ilipungua kutoka wachezaji 10 hadi watano.
    Chini ya Rais Leodegar Tenga- Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliona klabu zimeshindwa kutumia vyema fursa ya kusajili wachezaji wengi wa kigeni, kwa kuleta wachezaji wenye uwezo mkubwa, badala yake waliletwa wachezaji ambao walikuwa wanazidiwa uwezo kwa mbali kabisa na wachezaji wa hapa.
    TFF ikaona klabu hazijawa tayari kwa wachezaji wengi wa kigeni na kuamua kupunguza hadi kutoka 10 hadi watano- pia kutilia mkazo kwamba kuanzia msimu uliopita watabaki watatu. Kanuni ya wachezaji watatu ikapigwa teke hadi msimu ujao, lakini sasa kuna mchakato unaendelea ama, wachezaji wabaki watano, au waongezwe hadi saba.
    Taarifa ya TFF wiki iliyopita imesema kwamba idadi ya wachezaji wa kigeni Ligi Kuu itafanyiwa uamuzi na Kamati ya Utendaji, baada ya kupata maoni ya klabu za ligi hiyo na Ligi Daraja la Kwanza katika cha pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, Mei 11 mwaka huu.
    Taarifa ilisema mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee kuwa watano kama ilivyo katika kanuni za sasa, lakini kikao cha klabu na Malinzi kitatoa jibu.
    Shinikizo la klabu kubwa, Azam FC, Simba na Yanga ndilo linatarajiwa kubeba hatima ya idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi yetu kuanzia msimu ujao- kubaki watano au kuongezeka hadi saba.
    Ikumbukwe tayari Ligi Kuu imekwishapanuliwa na kuanzia msimu ujao wa 2015/2016 itakuwa na timu 16 badala ya 14 za sasa.
    Mabadiliko hayo yamepitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Mei 3, mwaka huu mjini Dar es Salaam baada ya kupokea mapendekezo ya kuongeza idadi ya timu kutoka kwenye Kamati ya Mashindano.
    TFF imesema uamuzi huo umefanywa kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo, na kuwezesha wachezaji kupata mechi nyingi zaidi za mashindano. Kwa mabadiliko hayo maana yake ni kuwa Ligi ya msimu wa 2015/2016 itakuwa na mechi 240 wakati kwa sasa ina mechi 182.
    Tutarajie kwa kiasi kikubwa, timu kubwa zitafanikiwa kuzishawishi timu zisizo na maslahi na wachezaji wa kigeni, kukubali idadi kubwa ya wachezaji wa nje- lakini tujiulize tuko tayari kwa hilo?
    Tulikwishapewa fursa ya kuwa na wachezaji 10 wa kigeni, lakini matokeo yake tukasajili wachezaji ambao hata kutuliza mpira hawajui- hadi TFF ikaamua kubadilisha kanuni hiyo.
    Hilo ni jambo la msingi kutazama, lazima ufike wakati klabu ziache utaratibu wa kuletewa letewa wachezaji na mawakala, zifuatilie zenyewe wachezaji jambo ambalo ni rahisi.
    Klabu lazima ziwe na vitengo maalum vya kufuatilia wachezaji, ambavyo watu wake watakuwa wanatazama Televisheni zinapochezwa mechi za Ligi za nje, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ili kutazama wachezaji wakali.
    Rahisi tu, Televisheni ya SuperSport inaonyesha ligi nyingi za Afrika pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho- huko watu wanaweza kupata wachezaji bora badala ya wale tuliokuwa tunaletewa akina Kanu Mbiyavanga na Jama Mba.
    Lakini pia maskauti wa klabu wanaweza kwenda kwenye fainali za mashindano mbalimbali ya Afrika yakiwemo ya vijana, kusaka vijana wenye vipaji na kuleta ambao wataleta changamoto ya kweli kwenye soka yetu.
    Tazama wale vijana wawili kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche na Kipre Balou- wote Azam FC iliwatoa katika timu ya vijana ya nchi hiyo iliyokuja kucheza michuano ya CECAFA Challenge mwaka 2010 hapa Dar es Salaam na wamethibitisha wao ni wachezaji kweli.
    Didier Kavumbangu aliyenyakuliwa na Azam FC kutoka Yanga SC, alikuja hapa na klabu yake, Atletico ya Burundi na kwa kiasi fulani ameonyesha ni mchezaji wa ukweli- kama ilivyo kwa mwenzake Amisi Tambwe.
    Tatizo huwa ni kwa hawa wachezaji wa kuletewa na mawala, sijui akina Akuffo na Asamoah- ila kama zinafanyika taratibu nzuri za kutafuta wachezaji wazuri wa kigeni, nchi itafurahia kanuni hiyo. Ndiyo maana ninauliza, tunalilia wachezaji kibao wa kigeni, je sasa tuko tayari? Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNATAKA UTITIRI WA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU, JE SASA TUKO TAYARI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top