Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
KIINGILIO katika mchezo kati ya Nigeria ‘Flying Eagles’ na
Tanzania, Ngorongoro kuwania tiketi ya Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri
chini ya miaka 20 Jumapili hii (Mei 11
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa Sh. 2,000.
Flying Eagles imewasili usiku wa kuamkia leo na msafara wa watu 32
kwa ndege ya Ethiopian Airlines ambapo imefikia hoteli ya Sapphire. Mechi hiyo
ya kwanza ya raundi ya pili itafanyika kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nigeria inayofundishwa na kocha Manu Garba itafanya mazoezi leo
(Mei 8 mwaka huu) saa 10 jioni itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa ambao
ndiyo utakaotumika kwa mechi siku ya Jumapili.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 kwa sehemu zote
wakati upande wa VIP itakuwa ni sh. 5,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya
mechi katika magari maalumu.
Ngorongoro Heroes ambayo katika raundi ya kwanza iliitoa Kenya kwa
jumla ya mabao 4-3 inaendelea kujinoa jijini Dar es Salaam chini ya Kocha wake
John Simkoko na Msaidizi wake Mohamed Ayoub kujiweka sawa kwa mechi hiyo
inayosubiriwa kwa hamu na washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Nigeria kama ilivyo kwa nchi nyingine 12 imeanzia moja kwa moja
raundi ya pili kutokana na ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF). Nchi hizo ni Afrika Kusini, Angola, Benin, Burkina Faso,
Cameroon, Gabon, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mali, Misri,
Morocco na Zambia.



.png)
0 comments:
Post a Comment