Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
HANS Van Der Pluijm, kocha mkuu wa Yanga amesema kwamba alikuwa
anapita njia tu katika klabu hiyo, kwani muda mrefu alikuwa ana dili la kazi Uarabuni.
Pluijm amewaaga rasmi wachezaji wake, viongozi, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo baada ya kumaliza
mkataba wake wa miezi sita na sasa anakwenda kujiunga na timu Al Shoalah FC
iliyoshiriki Ligi Kuu nchini Saudi Arabia.
Kocha huyo raia wa Uholanzi ambaye ameiongoza Yanga kwa kipindi
cha miezi mitano amesema anashukuru kwa sapoti aliyokuwa akiipata kutoka kwa
wachezaji, viongozi, wapenzi na wanachama wa timu hii kwa kipindi chote
alipokuwa nchini Tanzania tangu Januari mwaka huu.
![]() |
Nilikuwa napita tu; Kocha Hans van der Pluijm amesema alikuwa ana dili la kwenda Uarabuni kabla ya kutua Jangwani |
"Najua wengi itawashangaza kuona ninaondoka lakini ukweli ni
kwamba nilikuwa na hiyo dili hata kabla ya kuja Yanga, nilikuwa na makubaliano
na timu ya Al Shoalah FC, makubaliano ambayo yanaanza mwezi ujao hivyo
nilikubaliana na viongozi wa Yanga kuja kufanya kazi kwa kipindi cha miezi sita
tu, ninashukuru tumefanya kazi salama na baada ya mkataba huo kuisha nipo
tayari kurudi kuja kufanya kazi Tanzania," amesema Pluijm katika mkutano
na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya Yanga jijini Dar es
Salaam leo mchana.
Aidha, Pluijm aliyechukua jukumu la kuinoa Yanga akichukua mikoba
ya Mholanzi mwenzake Ernie Brandts aliyetimuliwa baada ya kufungwa 3-1 katika
mechi ya 'ndondo' ya 'Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba' Desemba 21 mwaka jana,
amesema anaipenda Yanga na amejaza fomu kuomba uanachama.
Kocha huyo anaondoka leo kwenda Ghana kisha kwenda nchini Saudi
Arabia tayari kwa kujiandaa na maandalizi ya msimu ujao katika timu hiyo ambayo
ataitumikia kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kuhusu usajili, kocha huyo amesema ameshakabidhi ripoti yake ya
kiufundi tangu juzi ambayo viongozi wanaifanyia kazi kisha kabla ya kuwekwa
wazi.
Kwa upande wake, Beno Njovu, katibu mkuu wa Yanga aliyekuwa
amefuatana na kocha huyo katika mkutano huo, amesema wameipokea ripoti ya
Pluijm na itajadiliwa na Kamti ya Utendaji ya klabu hiyo kabla ya kuanza kufanyiwa
kazi huku akieleza kuwa wataifanyia kazi ripoti hiyo ili kumrahisishia kocha
mpya ajaye.
“Tunamshukuru kwa msaada
wake ndani ya Yanga. Kwa kiasi kikubwa tutaifanyia kazi ripoti ya Pluijm, kwani
ameiona Yanga na anajua upungufu wake na hii itamrahisishia kocha ajaye ambaye
haifahamu
Yanga,” amesema Njovu.
0 comments:
Post a Comment