• HABARI MPYA

    Tuesday, May 05, 2009

    NSAJIGWA: SINA CHANGU YANGA


    BEKI wa kimataifa wa klabu ya Yanga, Nsajigwa Shadrack, amesema kwamba mkataba wake na klabu hiyo umemalizika na ameomba asitafutiwe sababu, hasa kupakaziwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
    Akizungumza na bongostaz Jumapili alisema: “Sijui haya yanatoka wapi, mimi nimekuwa mfano bora wa wachezaji wenye nidhamu, mara nyingi nimekuwa nikiwaongoza wachezaji wenzangu, kwa mfano, wakitaka kugoma hivi nawaambia hapana, msifanye hivyo.
    Lakini leo naambiwa mimi nitaachwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu upi? Napenda kusema mimi si mtovu wa nidhamu hata kidogo, nawaheshimu viongozi wa Yanga na makocha wote na wala sijawahi kukwaruzana nao.
    Ila kuna kiongozi mmoja tu, huyo tuliwahi kupishana kauli, tangu siku hiyo amekuwa kama ananipiga mizengwe, ila mimi nasema hii Yanga bwana, wamekwishapita wengi, Yanga imekwishaacha wachezaji wengi wazuri mno. Hata mimi najua siku moja nitaondoka, hapa tunapita na hata hawa viongozi nao wakati wao utafika, wataondoka, kwa hiyo mimi ninaomba tusichafuliane majina,” alisema Nsajigwa.
    Kauli hiyo ya Nsajigwa inafuatia habari kwamba yeye na George Owino watauzwa klabu ya Red Star Belgrade ya Serbia, ambayo hivi sasa inadaiwa kuyumba kiuchumi kiasi cha kukimbiwa na baadhi ya wachezaji wake.
    Klabu hiyo pekee ya Ulaya Mashariki kuwahi kuchukua ubingwa wa Ulaya mwaka 1991, hivi sasa ipo katika hali mbaya mno kiuchumi na wachezaji wake walikaririwa mwezi uliopita wakisema hawana fedha kwa ajili ya chakula wala kulipia nyumba wanazoishi.
    Kiungo wake mahiri, Mirnes Sisic, raia wa Slovenia, aliwawakilisha wachezaji wenzake kwa kueleza kilio chao alipozungumza na Reuters.
    Alisema alifukuzwa kwenye nyumba baada ya Red Star kushindwa kulipia pango, wakati wachezaji wengine wa Afrika Kusini walikamatwa uwanja wa ndege wakiwa wanataka kutoroka na kurejeshwa Belgrade.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSAJIGWA: SINA CHANGU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top