• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 30, 2009

  KONDIC: BADO NIPO SAAANA YANGA

  KOCHA wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Savo Kondic amesema kwamba hafikirii kuiacha klabu hiyo kwa sasa, kwani ana mipango yake anayotaka kuikamilisha kwanza ili siku akiondoka akumbukwe daima.
  Akizungumza na bongostaz jana mjini Dar es Salaam, Kondic alisema kwamba amepata ofa kutoka klabu za Afrika Kusini na Angola, zikimtaka akafundishe lakini hajazikubali na ameamua kuendelea na Yanga.
  "Siku nitakapotaka kuondoka Yanga, nitasema, asanteni, inatosha, kwaherini. Mimi ni kocha mwenye taaluma,"alisema Kondic.
  Mtalaamu huyo kutoka Serbia, alisema kwamba si kweli kuwa Mkataba wake umemalizika Yanga kama inavyoelezwa na vyombo vya habari nchini, bali utamalizika Desemba mwaka huu.
  Alisema tayari amekubaliana na Yanga kuongeza mkataba baada ya huu wa sasa kumalizika na hawezi kuwa kigeugeu katika hilo. "Nimemua kuendelea kufanya kazi Yanga kwa sababu ninawaheshimu mashabiki, hii ni timu kubwa yenye mashabiki wengi zaidi.
  Ninamuheshimu mfadhili (Yussuf Manji), amekuwa akitumia fedha nyingi kwa ajili ya timu, ananipa sapoti kubwa kufanikisha mambo yangu hapa, nawaheshimu viongozi na kila mtu katika Yanga,"alisema.
  Kondic alisema kwa sasa anasubiri kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa jengo la klabu hiyo, lililopo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam, ili aanze rasmi programu yake endelevu ndani ya klabu hiyo.
  "Kwa kiasi kikubwa mambo yamekamilika, gym iko tayari sehemu ya kuchezea mpira inatengenezwa sasa, vyumba viko tayari, yaani kama mambo yataendelea hivi sidhani kama itachukua muda mrefu zaidi ya mwezi kabla haijakamilika kabisa,"alisema.
  Alisema katika mikakati yake endelevu, atakuwa na timu za vijana kuanzia chini ya umri wa miaka 12, 17 na 22 ambao anaamini miaka ijayo watakuwa tegemeo la taifa.
  "Sisi wote, mimi na wenzangu, Spaso (Sokolovoski) na (Civojnov) Serdan tunaendelea na kazi hapa.
  Lengo letu kubwa lilikuwa kwanza ujenzi wa jengo pale na Uwanja ukamilike ndio tuanze kazi rasmi, sasa kama hilo limekamilika iweje tuondoke, bado hatujafanya kazi tuliyokusudia hapa,"alisema.
  Kondic aliwasili mjini Dar es Salaam juzi usiku akitokea Afrika Kusini alikokwenda kushuhudia mechi kadhaa za michuano ya Kombe la FIFA la Mabara. Akiwa nchini humo ambako pia anaishi na familia yake, kuliibuka habari kwamba hatarejea nchini ameamua kuachana na Yanga.
  Kondic alianza kuifundisha Yanga Desemba 2007 na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mara mbili mfululizo. Msimu huu alipewa tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kwa kushinda tuzo hiyo, Kondic ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza mgeni kutunukiwa tuzo hiyo, ambayo awali ilikuwa inachukuliwa kama tuzo maalum kwa ajili ya makocha wazalendo.

  Boniphace Ambani kupima afya China

  MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Kenya, anaicheza klabu ya Yanga, Boniphace Ngairah Ambani ameitwa na klabu ya Hangzhou Greentwon ya Zhejiang China ili kuchukuliwa vipimo vya Kiafaya, mtihani ambao akifuzu atapatiwa mkataba na klabu hiyo, iliyomfanyia majaribio Machi mwaka huu.
  Akizungumza jana kwa simu mjini Dar es Salaam, Ambani alisema kwamba amepokea mwaliko wa kuitwa China kwenye klabu iliyomfanyia majaribio, ili aende kufanyiwa uchunguzi wa afya yake kabla ya kusaini mkataba.
  Ambani aliyewasili jana mjini Dar es Salaam, akitokea kwao Nairobi, alisema kwamba anafanya mpango wa kupata Visa, kutoka Ubalozi wa China ili aende haraka kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
  Awali kulikuwa na habari kwamba, baada ya Greentwon kumpata Moses Sakyi wa Ghana, iliamua kuachana na Ambani, lakini sasa imemgeukia tena mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mapema juzi, kocha wa Yanga, Profesa Dusan Savo Kondic alisema kwamba ni kweli Ambani ameitwa tena China na kwamba mbali na mpachika mabao wake huyo hatari, pia wachezaji wengine George Owino na John Njoroge nao wanatakiwa kwenda kufanya majaribio Ujerumani.
  "Owino na Njoroge wote kwanza walikuwa wanatakiwa Iran, lakini sisi tuliikataa hiyo ofa kwa sababu haitawasaidia wachezaji wetu, sasa tumeamua tuangalie hii ya Ujerumani,"alisema Kondic.
  Ambani alijiunga na Yanga msimu huu akitokea India, alikokuwa akichezea na tangu amejiunga na klabu hiyo, ametokea kuwa mfungaji tegemeo wa klabu hiyo.


  Kocha wa Nancy ya Ufaransa
  amfuata Mrisho Ngassa Dar

  KOCHA wa klabu ya AS Nancy inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, Pablo Correa anatarajiwa kuwasili nchini wiki hii kwa ajili ya kufanya mpango wa kumchukua, winga wa klabu ya Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa ili akaendeleze kipaji chake kwenye klabu hiyo.
  Kocha huyo raia wa Uruguay, amevutiwa na kipaji cha Ngassa aliyewahi kufanyiwa majaribio na klabu ya West Ham United ya England Aprili mwaka huu na ameiarifu klabu ya Yanga anakuja kuonana ana kwa ana na winga huyo mwenye kasi uwanjani.
  "Kocha wa Nancy anakuja wiki hii kuonana na Ngassa, anamtaka. Hii inakuwa ofa ya pili kwa Ngassa baada ya ile ya Urusi, huyu ni mchezaji mwenye kipaji, nina imani atafanikiwa,"alisema Kocha wa Yanga, Profesa Dusan Savo Kondic alipozungumza na bongostaz juzi jioni mjini Dar es Salaam.
  Kondic alisema kwamba kipaji cha Ngassa kinawavutia makocha wengi Ulaya na wengi wameonyesha nia ya kumhitaji kijana huyo, hivyo hata kama atashindana na Correa wa Nancy, bado nyota huyo ana nafasi nyingine kadhaa za kwenda kujaribu bahati yake.
  Kwa kipindi hiki ambacho Ligi imesimama na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars haipo kambini, Ngassa amekuwa akijifua mwenyewe kwenye Uwanja wa Saba Saba, Mtoni asubuhi na usiku ili kujiweka fiti.
  "Ninafanya mazoezi kwenye Uwanja mmoja wa mchanga huku Saba Saba, lengo ni kujiweka fiti, ili wakati wowote nikiitwa kwa majaribio niwe fiti, nafanya asubuhi na usiku,"alisema Ngassa alipozungumza na DIMBA juzi jioni.
  Ngassa ilikuwa aondoke nchini Ijumaa kwenda Urusi kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu moja ya huko, lakini kutokana na wakala wake Yussuf Bakhresa kushindwa kumpatia viza ya kuingia nchini humo, safari hiyo ilishindikana.
  AS Nancy-Lorraine ni klabu iliyoanzishwa mwaka 1967 ikitokana na klabu ya FC Nancy, iliyokufa mwaka 1965 na ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Ufaransa, inayojulikana kama Ligue 1 msimu wa 2005-2006.
  Hiyo ni timu ambayo hata nyota wa zamani wa Ufaransa, Michel Platini aliichezea kuanzia msimu wa 1973 hadi 1979.
  Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Stade Marcel Picot, msimu wa 2005-2006 ilitwaa Kombe la Ligi Ufaransa, (Coupe de la Ligue), hivyo kupata tiketi ya kucheza Kombe la UEFA.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KONDIC: BADO NIPO SAAANA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top