// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); WAJUAJI WENGI, WATAALAMU ‘NJAA NJAA’ MAJANGA KWA SOKA YETU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE WAJUAJI WENGI, WATAALAMU ‘NJAA NJAA’ MAJANGA KWA SOKA YETU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, May 18, 2014

    WAJUAJI WENGI, WATAALAMU ‘NJAA NJAA’ MAJANGA KWA SOKA YETU

    TANZANIA ilikosa tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee baada ya kufungwa nyumbani na ugenini na Uganda mwaka jana.
    Ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen, Taifa Stars ilifungwa 1-0 na The Cranes Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 3-1 Kampala na kutolewa.
    Kikosi kilihusisha wachezaji wote wa timu pendwa nchini, Azam, Simba na Yanga, lakini ilikuwa vigumu kuvuka mbele ya Waganda.
    Hakika matokeo yale yalikatisha tamaa mno mashabiki wa soka nchini na wengi wakapendekeza timu ivunjwe na kuundwa upya.

    Hayo yalikuwa maoni ya wadau wakati ule baada ya kutolewa na Uganda- na zaidi yalitokana na hasira za kipigo.
    Tuna matatizo mengi mno katika soka yetu na tunahitaji suluhisho la kudumu ambalo litatokana na tathmini za kitaalamu zinazotakiwa kufanywa na wataalamu. 
    Lakini inakuwa vigumu kufuata njia hiyo kwa sababu ya kasumba moja kubwa tuliyonayo, ujuaji na ubinafsi.
    Viongozi wetu wa siku hizi wanajifanya wajuaji sana, hawashauriki, hawataki kuwaachia wataalamu wafanye kazi zao- bali kila kitu wanajua wao, wanaweza wao.
    Kiongozi anamuagiza mtaalamu afanye jambo hata kama si sahihi kitaalamu, lakini mtaalamu naye kwa nidhamu ya woga, kuogopa akikataa ataondolewa kazini- basi anakubali tu.
    Hili ni tatizo kubwa- viongozi wanaamka na mipango yao kwenye ndoto zao wanakuja kuwaagiza wataalamu wafanye- na kwa bahati mbaya wataalamu wetu wengi ni ‘njaa njaa’ wanakubali, matokeo yake wanazidi kuipotezea muda wa kusonga mbele soka yetu.
    Tumekuwa mahiri wa kuimba ‘programu programu’, lakini namna ya kutekeleza linakuwa tatizo- badala yake tumeendelea kufanya mambo kwa hisia zaidi kuliko uhalisia.
    Uwekezaji wa soka ya vijana ni jambo la msingi sana katika maendeleo ya mchezo huo, lakini bado tumeendelea kulifanya hilo kwa mzaha mzaha, bila kujua athari zake ni zipi.
    Yapata miaka mitano sasa tangu klabu zimetakiwa kuwa na timu za vijana na ni msimu wa nne sasa mfululizo katika kanuni za Ligi Kuu, imeambatanishwa na ligi ya vijana pia, ambayo huwa na usajili wake maalumu.
    Lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshindwa kuisimamia ligi hiyo ipasavyo, matokeo yake umagumashi mwingi unafanyika.
    Timu zinatumia wachezaji waliozidi umri, kwa sababu hazijui umuhimu wa kutumia wachezaji vijana halisi. Mashindano ya vijana ni maalum kuandaa wachezaji bora wa baadaye, lakini pamoja na dhana hiyo, timu zinafikiria ushindi zaidi na kuamua kuchomekea wachezaji waliozidi umri.
    TFF imeshindwa kusimamia vyema hilo na matokeo yake timu nazo zinatumia mwanya huo kufanya upumbavu mbaya sana kwa soka yetu.
    Upande wa pili, bado ligi ya vijana ya Ligi Kuu haina sifa, kwa sababu haieleweki na haipo katika mpangilio wenye kueleweka.
    Timu hazisafiri kwenda kwenye mechi za ugenini, maana yake kama Dar es Salaam wana timu sita, basi zitamenyana baina yao tu.
    Mtibwa Sugar ambayo msimu uliopita ilikuwa timu pekee pale Morogoro haikucheza na timu nyingine yoyote ya vijana ya Ligi Kuu kadhalika Kagera Sugar ya Bukoba, Rhino Rangers ya Tabora, Ruvu Shooting ya Pwani na JKT Oljoro ya Arusha.
    Tanga Coastal Union na Mgambo JKT zilimenyana zenyewe tu. Zaidi ya hapo, timu za vijana za Ligi Kuu hukutanishwa katika mashindano ya wiki mbili, Kombe la Uhai mjini Dar es Salaam.
    Sasa unaweza kujiuliza, hivi hawa watu wa TFF wanajua umuhimu wa kuwa na timu za vijana, au tunapokea maagizo ya FIFA na CAF na kuyatekeleza ili mradi tuonekane tumeyatekeleza tu, bila kujua faida yake? 
    Soka ya leo ni mchezo wa kisayansi, unahitaji elimu na wenye soka yao, FIFA kila siku wamekuwa wakitoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya uendeshaji wa mchezo huo.
    Lakini inakuwa tabu kama tu pale TFF hakuna waatalamu wenye elimu ya mpira wa miguu- maana yake hata hao viongozi wa klabu hawawezi kuelimishwa.
    Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi ameingia na mikakati mingi ambayo kwa bahati mbaya anataka kuitekeleza yote kwa wakati mmoja- ni jambo gumu.
    Kwa weledi wake, Malinzi aliingia na mpango wa kutengeneza Taifa Stars mpya, akaunda jopo la makocha kuzunguka nchi nzima kusaka vipaji.
    Ulitumika muda na gharama katika zoezi hilo, lakini mwisho wa siku baada ya ujio wa kocha mpya, Mholanzi Mart Nooij aliyeishuhudia timu mpya ikicheza soka mbovu na kufungwa 3-0 na Burundi katika mchezo wa kirafiki, akabadilisha mambo.
    Nooij alirudisha wakongwe wote waliokuwa wakiitumikia timu kabla yake kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa katika makundi ya kugombea tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco dhidi ya Zimbabwe.   
    Ni wachezaji wale wale, ambao baadhi yao wamekuwa wakiichezea timu hiyo tangu enzi za kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambao walishindwa kufurukuta mbele ya Uganda.
    Naamini, ubora wa mwalimu mpya unaweza kubadilisha timu yetu na ikafanya vizuri sasa, lakini bado tunatakiwa kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo ya soka yetu.
    Lazima tuwe na msingi bora na imara wa kuanzia kuibua vipaji, kuvilea na kuviendeleza, ili baadaye tuje kuwa na timu bora ya taifa.
    Tuna mashindano mengi ya kuibua vipaji kama Airtel Rising Stars, Copa Coca Cola na mengine, lakini tujiulize vijana wanapotoka hapo wanakwenda kulelewa wapi, wanakwenda kuendelezwa wapi?
    Lazima klabu zetu ziwe hatua ya pili ya vijana hao kuelelewa na kuendelezwa, lakini kwa bahati mbaya, ukiondoa Azam FC, sehemu nyingne kwenye fursa hiyo ipo labda ni kwenye timu za majeshi pekee.
    Lazima TFF ihakikishe klabu zinakuwa na timu rasmi na halisi za vijana na ambazo zinahudumiwa vizuri na kucheza mashindano.
    Pili, lazima TFF ihakikishe ligi ya vijana inakuwa ligi kamili, ambayo vijana wancheza ligi yao sawa na sambamba na ligi ya wakubwa.
    Tukifanya hivyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana katika kujenga msingi imara wa uzalishaji vipaji- ambavyo baadaye vitakuja kulisaidia taifa letu.  Lakini tukiendelea na usanii, basi daima milele soka yetu haitafika popote. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAJUAJI WENGI, WATAALAMU ‘NJAA NJAA’ MAJANGA KWA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top