Na Dina Ismail, Dar es Salaam
KAMPUNI Smart Sports imejitolea kuratibu safari ya mashabiki wanaotaka kwenda Harare, kuishangilia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mchezo wa marudiano na wenyeji Zimbabwe Juni 1, mwaka huu.
Tanzania ilishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Jumapili na wiki ijayo timu hizo zitarudiana Harare.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeikabidhi Smart Sports chini ya Mkurugenzi wake, George Wakuganda jukumu la kuratibu safari ya njia ya barabara kwa ajili ya mashabiki wanaotaka kwenda kuisapoti timu katika mchezo wa marudiano.
Wakuganda ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba mashabiki wataondoka na usafiri wa mabasi maalum ambayo yatawasili Harare Jumapili siku ya mechi na baada ya mchezo wataanza safari ya kurejea Dar es Salaam.
Wakuganda amewataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu yao ya taifa kwa kwenda kuishangilia ikicheza nchini Zimbabwe.
![]() |
Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' akiwaongoza wenzake kuingia uwanjani kwenye mchezo na Zimbabwe Jumapili |
Kuhusu gharama za safari, Wakuganda amesema kila shabiki atawajibika kulipa kiasi cha Sh 300,000 kwa ajili ya nauli ya kwenda Harare na kurudi Dar es Salaam.
Amewataka mashabiki wenye nia ya kusafiri kwenda kuishangilia Stars ikicheza ugenini kuwasiliana naye kwa nambari ya simu +255 715 995 111.
0 comments:
Post a Comment