• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 02, 2009

  MTAGWA KUWANIA UBINGWA WA WBO

  BONDIA nyota wa Tanzania anayeishi Philadelphia nchini Marekani, Rogers Mtagwa anatarajiwa kupanda ulingoni Jumamosi (Oktoba 10, 2009) katika ukumbi wa Wamu Theater, Jijini New York, kuzipiga na bingwa wa WBO, Juan Manuel Lopez, akiwania taji hilo katika uzito wa Super Bantam.
  Katika barua pepe aliyoituma Mtagwa kwa mwandishi wa habari hizi, amewaomba Watanzania wamuombee dua atwae taji hilo la dunia lenye pesa nyingi.
  “Napigania ubingwa wa dunia wa WBO Jumamosi, napigana na bondia mmoja mkali sana, Watanzania waniombee dua nishinde, pambano hili litaonyeshwa dunia nzima, Watanzania wengine wanaweza kuliona live online (kwenye mtandao)”alisema Mtagwa.
  Mtagwa anayetumia jila la utani, The Bull kwa sasa badala ya Tiger aliloingia nalo nchini humo mwaka 2000; Machi 22, mwaka huu alitimiza miaka 30 na Jumamosi atakuwa akizipiga na bondia mwenye umri wa miaka 26 tu. Hili litakuwa pambano gumu kweli kwa Mtagwa, kwani Juan ajulikanaye kama Juanma kwa jina la utani ni bondia bora na hodari haswa, mwenye rekodi nzuri kaunzia ngumi za Ridhaa.
  Raia huyo wa Puerto Rico alicheza michuano mbalimbali mikubwa katika ngumi za Ridhaa ikiwemo Michezo ya Amerika ya Kati na Caribbean mwaka 2002, Michezo ya Amerika mwaka 2003 na Olimpiki mwaka 2004 na baada ya mafanikio hayo, ndipo akajitosa kwenye ndondi za kulipwa mwaka 2005.
  Hakuchelewa kupata mafanikio kwenye ndondi za kupigana kifua wazi, kwani Septemba 30, mwaka 2006 alimtwanga Jose Alonso na kutwaa ubingwa wa Mabara wa WBO (Latino), uzito wa Super Bantam, kabla ya Juni 7, mwaka jana kumtandika Daniel Ponce de Leon kwa Technical Knockout (TKO) na kutwaa ubingwa wa dunia wa WBO katika uzito huo.
  Mtagwa mbali na kuwa bingwa wa Baraza la Ngumi Amerika Kaskazini (NABF), pia ni bondia anayeheshimika na vyama vyote vikubwa vya ndondi duniani, WBO, WBC na IBF.
  Mtagwa ambaye yupo chini ya Meneja Joe Parella na kocha Bobby ‘Boogaloo’ Watts, bondia wa zamani wa uzito wa Middle, anapigana kwa staili ya Orthodox (anapigia mkono wa kulia) atakuwa na wakati mgumu Jumamosi, kwani mpinzani wake anapigana kwa staili ya Southpaw (anapigia mkono wa kushoto). Wataalamu wa ndondi wanasema kwamba, bondia wa Orthodox ili kumpiga Southpaw, inabidi afanye kazi sana ulingoni, kama ambavyo Floyd Mayweather Jr, amekuwa akifanya.
  Pamoja na kupigana kwa staili ya Orthodox, lakini Mayweather amekuwa akiwadunda mabondia wa Southpaw kutokana na ujanja wake wa kubadilisha badilisha mchezo ulingoni.
  Akifanikiwa kutwaa taji hilo, Mtagwa atakuwa bondia wa kwanza kabisa Mtanzania kutwaa taji la ndondi la dunia la moja kati ya vyama vitatu vikubwa- WBC, IBF na WBO.
  Rashid Matumla aliwahi kutwaa taji la WBU mwaka 1999 na akiwa na ndoto za kuwania mataji makubwa ya WBC, WBO na IBF, kampuni ya DJB Promotions iliyokuwa ikimmiliki ilimtema na huo kuwa mwanzo wa kupoteza kwake mwelekeo kwenye mchezo huo. Mbwana Matumla aliyewahi kutwaa taji la WBA International, angeweza kufika mbali naye, kama DJB ingeendelea kummiliki, lakini tangu ilipomtema, amepoteza mwelekeo pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTAGWA KUWANIA UBINGWA WA WBO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top