• HABARI MPYA

    Saturday, October 31, 2009

    HIZI NI SALAMU ZANGU KWAKO MH MKUCHIKA...




    NIANZE kwa kumpongeza Waziri Habari Utamaduni na Michezo, Mh. George Huruma Mkuchika na watendaji wote wa wizara wafanyao kazi kwa uadilifu, kwani mabadiliko makubwa yenye kuashiria ufanisi yameonekana kwa kipindi chake tangu apewe wizara hiyo.
    Kwa mwelekeo huu, bila shaka kama Mkuchika atabakia kwenye wizara hiyo kwa miaka mitano ijayo, yapo matarajio makubwa kwamba; sekta ya sanaa, michezo na utamaduni wetu vitaimarika kwa kiasi kikubwa.
    Miongoni mwa mambo ya hivi karibuni aliyowahi kufanya Mkuchika ambayo yaliwafurahisha Watanzania wengi ni tamko lake la kupiga marufuku maonyesho yote ya filamu kwenye hadhara ya watu, majumba yasiyo rasmi, vibanda, kumbi ndogondogo, hoteli na maeneo ya baa bila kufuata masharti ya jumba la sinema- kwa mujibu wa sheria na 4 ya mwaka 1974 inayotumika nchini.
    Katika agizo lake alililitoa mjini Dar es salaam, wakati akizindua Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini ambayo itakuwa na jukumu la kukagua na kusimamia maonyesho na shughuli za filamu nchini, Mkuchika alisema sehemu nyingi zinazotumiwa kuonyesha filamu hazina leseni halali za kuonyeshea filamu na kuongeza kuwa siyo salama kwa mali na afya za watu.
    Alisema athari nyingi tayari zimekwishajitokeza katika jamii yetu na filamu nyingi zimechangia kubomoa na kudumisha Utamaduni wa taifa- na hata kuchangia kwa kiasi kikubwa kubomoa misingi ya amani, upendo, uadilifu, heshima, uaminifu na utu ambao ni utambulisho wa Mtanzania jinsi ulivyokuwa umejijenga na kuenea katika jamii yetu.
    Kweli tamko hili limeonekana kupokewa vizuri na wahusika wote waliotajwa wameanza kufuata taratibu- kwani wale ambao wameendelea kufanya mambo kinyume wamekuwa wakikutana na mikono ya sheria.
    Hata hivyo, kuna jambo moja tu ambalo pengine wakati ule Mkuchika ama alisahau au alikuwa hajapewa taarifa kabisa kuhusu suala hilo- nalo ni hizi kampuni ndogondogo za hapa nyumbani za kutoa huduma za Televisheni za kulipa, maarufu kama Cable Televisheni, nazo sasa zinatishia amani ya utamaduni na maadili ya Mtanzania.
    Kana kwamba hiyo haitoshi, kampuni hizi (siyo zote) pia zimekuwa zikihujumu kwa kiasi kikubwa kazi za wasanii wa Tanzania, kutokana na kuthubutu kuonyesha filamu za wasanii wa nje na ndani bila ya kufuata utaratibu.
    Ingawa wakati anatoa tamko lake la kupiga marufuku maonyesho yote ya filamu kwenye hadhara ya watu, majumba yasiyo rasmi, vibanda, kumbi ndogondogo, hoteli na maeneo ya baa bila kufuata masharti ya jumba la sinema- kwa mujibu wa sheria na 4 ya mwaka 1974, hakuwataja watu wa Cable Televisheni, lakini ukweli ni kwamba sheria hii inawahusu na wao pia.
    Ila kwa sababu hawakutajwa moja kwa moja, basi wamejihisi wako huru kuwaonyesha filamu wateja wao bila ya kuzingatia sheria namba 4 ya mwaka 1974, lakini ukweli unabaki pale pale- kwa sababu wao wanafanya biashara, kutokana na kupokea ada za kila mwezi kutoka kwa wananchi na kuwapa huduma- basi sheria hii inawahusu.
    Juzi nilikuwa nazungumza na msanii mmoja anaitwa Check Budi, akaniambia alikwenda Kahama mkoani Shinyanga na Nzega mkoani Tabora kwa shughuli zake binafasi, huko alikutana na mambo ambayo yapo kinyume na tamko la Mkuchika.
    Alisema kuna kampuni za Cable TV zinaonyesha filamu za wasanii wa Tanzania, lakini kwa sababu wanajua huo ni vunjaji wa sheria- inapofia wakati wa kuonyesha filamu hizo- hawatoi nembo ya TV yao.
    Kwa nini hawatoi? Nilimuuliza Check, ambaye aliniambia hivi; “Wanajua wakitoa watu watarekodi na kwenda kushitaki, kwa hivyo wanafanya wakijua kabisa wanavunja sheria, watu hawa ni hatari sana, wanaweza kuwa wanaonyesha hata picha za ngono na watu watashindwa kuwachukulia hatua, kwa sababu utapeleka mahakamani ushahidi ambao hauonyeshi ni Cable TV gani? si itakuwa kichekesho,”.
    Hivyo ndivyo alivyoniambia Check kuhusu watu hao wanaomiliki Cable TV- namna ambavyo wanamcheza shere Waziri Mkuchika kwa kufanya kile ambacho alikataza lakini kwa kutumia ujanja ujanja.
    Kwa kuzingatia kwamba sanaa imeajiri vijana wengi wa taifa hili, ambao pengine bila ya hivyo leo baadhi yao wangekuwa waporaji mitaani, au wafanya uhalifu wa namna yoyote- kwanza hiyo pekee ni sababu tosha ya watu hawa kuchukuliwa hatua.
    Kwani kufanya hivyo kunasababisha wateja wao wasinunue tena filamu za wasanii wa nyumbani baada ya kuziona bure kwenye Cable TV- na kama msanii atakuwa hapati mauzo mazuri kwenye kazi yake, je sanaa itakuwa na faida tena kwake?
    Na akiachana sanaa akafanye gani- kama ambavyo tunafahamu wasanii walio wengi Tanzania (siyo wote) ni wale ambao elimu zao ni ndogo- katika kuhakikisha wanatafuta sehemu za kujiegesha waweze kuendesha maisha yao wamegundua sanaa.
    Mbali na sababu hiyo, kikubwa ni kwamba mfanyabiashara ambaye yupo tayari kuvunuja sheria ili biashara yake iende vizuri, huyo ni hatari sana kwa taifa- kwani anaweza kufanya jambo lolote ili avune zaidi.
    Kuna hatari kubwa hawa watu wanaweza kweli kuwa wanaonyesha hata sinema za ngono- wakiamini kwa hivyo ndiyo watavutiua wateja wengi kwenye biashara yao. Ni kwa sababu hiyo namtumia salamu hizi Waziri Mkuchika, ajue kwamba kuna watu wanamcheza shere. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIZI NI SALAMU ZANGU KWAKO MH MKUCHIKA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top