Na Prince Akbar, Dar es Salaam
TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Nigeria, Flying Eagles
imewasili usiku wa manane jana nchini tayari kwa mchezo dhidi ya Tanzania,
Ngorongoro Heroes Jumapili hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya
Fainali za Afrika mwakani nchini Senegal.
Eagles imewasili na msafara wa watu 30, wakiwemo wachezaji 18,
miongoni mwao wanacheza Ulaya na kufikia katika hoteli ya kimataifa ya Sapphire
Court, iliyopo makutano ya mitaa ya Lindi na Sikukuu, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Sapphire Court, Abdulfatah Salim Saleh ameiambia BIN
ZUBEIRY Flying Eagles wamefika salama na kupatiwa huduma nzuri tayari kwa
mchezo wa mwishoni mwa wiki.
![]() |
Manu Garba, kocha wa Flying Eagles |
Flying Eagles kwa sasa inafundishwa na kocha aliyeipa Nigeria
Kombe la nne la Dunia la U-17 mwaka jana, katika mashindano yaliyofanyika Falme
za Kiarabu, Manu Garba.
Garba ni kocha mwenye mafanikio Nigeria akiwa amewahi kuwa
Msaidizi wa Yemi Tella wakati Golden Eaglets inatwaa taji la U17 Afrika mwaka 2007
mjini Lome, Togo kabla ya kutwaa na Kombe la Dunia pia nchini Korea.
Aliiongoza pia timu ya jimbo la nyumbani kwao, Gombe Youth Team kutwaa
ubingwa wa michuano ya U-18 ya Umbro mjini Manchester mwaka 2005.
Mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, enzi zake
alichezea klabu za El-Kanemi Warriors (1987-1993); Kano Pillars (1994); Gombe
United (1995) na BCC Lions (1996).
Alianza ukocha mara tu baada ya kustaafu kama mwalimu Msaidizi
Gombe United kuanzia 1997 hadi 2008 kabla ya kuwa Mshauri wa Ufundi mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment