Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
KINDA anayecheza soka ya kulipwa Ujerumani, Charles Mishetto
ameomba kuitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars aisaidie katika
kampeni za kuing’oa Zimbabwe.
Hatua hiyo inakuja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)
kuikubalia TP Mazembe ya DRC ambayo imegoma kuwaachia Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu kuitumikia Taifa Stars katika mechi ya kuwania kushiriki fainali
zijazo za Afrika (AFCON) dhidi ya Zimbabwe.
FIFA imesema klabu hazitashurutishwa kuwaachilia wachezaji wao ili
washiriki mechi za kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika Morocco mwakani, kwa
sababu ipo nje kalenda ya mechi za shirikisho hilo.
![]() |
Nipeni mikoba; Charles Mishetto kushoto akicheza Ujerumani |
Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mwasiliano wa TFF alisema jana mchana kuwa wawili hao
hawatakuwamo kwenye kikosi cha kovha mpya Mholanzi Mart Nooij kitakachoivaa
Zimbabwe mwishoni mwa wiki ijayo kwa vile wanahitajika kwenye klabu yao.
Lakini Mishetto anayechezea klabu ya SPBGG 1914 Selbitz ya
Ujerumani ameiambia BIN ZUBEIRY jana kutoka nchini humo; “Kama TFF wataweza
kuandika barua kwa klabu yangu inaweza kuniruhusu waje wanione, wakiona
nitawafaa, sawa wakiona siwezi nitarudi, ila naamini ninaweza kuisaidia timu
yangu,”.
Charles Mishetto ameendelea kung’ara katika Ligi Daraja la Nne
Ujerumani baada ya mwishoni mwa wiki kufunga bao moja timu yake ikilala 2-1
mbele ya SVO 1912 ugenini.
Katika mchezo huo Ligi Daraja la Nne, iitwayo Bayernliga 4,
Michael Johnson aliwafungia wenyeji dakika ya 10 na Ricko Muller akafunga la
pili dakika ya 26, kabla ya Mishetto kuifungia Selbitz dakika ya 62.
Mishetto aliangushwa kwenye eneo la hatari siku hiyo na timu yake
ikapewa penalti, lakini bahati mbaya yeye mwenyewe akakosa.
Mechi za kuwania kufuzu AFCON zitafanyika Mei 16-18, tarehe ambayo
haipo kwenye ratiba ya FIFA na kwa hivyo haitakuwa lazima wachezaji wa klabu
kuruhusiwa kuondoka.
Hata hivyo, michuano ya makundi itakayoshirikisha Ghana, Nigeria
na Cameroon, zitakuwa katika tarehe iliyoidhinishwa na FIFA , ikimaanisha kuwa
klabu vya soka kote duniani lazima ziwaruhusu wachezaji wao kushiriki mechi
hizo.
Mbali na Samata na Ulimwengu, wachezaji kama Edward Sadomba,
wataathiriwa na mgongano wa tarehe zilizo kati ya mechi za kufuzu
zitakazofanyika 2015 na michuano ya klabu. Sadomba atahitajika kwa wakati mmoja
na klabu yake ya Al Ahli Benghazi pamoja na timu yake ya taifa Zimbabwe
itakayokipiga dhidi ya Taifa Stars.
Lakini FIFA lilikaririwa na BBC juzi likieleza kuwa wachezaji
wanaweza tu kuondoka ikiwa maafisa wa klabu na mashirikisho ya nchi husika
wanaweza kukubaliana.
0 comments:
Post a Comment