• HABARI MPYA

  Saturday, July 09, 2016

  RASMI, MAYANGA AREJESHWA MTIBWA SUGAR, MECKY AENDA KAGERA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Mtibwa Sugar imeingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Salum Mayanga kwa ajili ya kukinoa kikosi chake kama kocha mkuu kwa misimu ya 2016/17 na 2017/18. Mwalimu Mayanga anachukua nafasi ya Mecky Maxime aliyekuwa kocha mkuu wa Mtibwa na ambaye msimu huu ameingia mkataba wa kuifundisha klabu ya Kagera Sugar. Kwenye majukukumu yake mapya, Mayanga atasaidiwa na Patrick Mwangata pamoja na Zuberi Katwila ambao tokea awali walikuwemo kwenye benchi la ufundi la Mtibwa kama walimu wasaidizi.
  Mwalimu Mayanga ambaye msimu uliopita aliifundisha klabu ya Prisons ya Mbeya na kuiwezesha kumaliza katika nafasi ya nne, ni mmoja wa makocha wenye ujuzi mkubwa na uzoefu hapa nchini. 
  Salum Mayanga amerejeshwa Mtibwa Sugar kuchukua nafasi ya Mecky Mexime 

  Kocha Mayanga ana leseni ya ukocha ya daraja A inayotambuliwa na CAF, na pia aliwahi kuhudhuria kozi ya kimataifa ya ukocha wa mpira wa miguu iliyofanyika kwa wiki tatu nchini Ujerumani mwaka 2009.
  Hii ni mara ya pili kwa Mwalimu Mayanga kuifundisha klabu ya Mtibwa Sugar kama mwalimu mkuu. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2008/09 na 2009/10 ambapo aliweza kuipatia klabu ya Mtibwa mafanikio makubwa kwa kuiwezesha kutwaa kombe la Tusker, Kombe la Mapinduzi na pia kutwaa ngao ya jamii. Aidha kabla ya kuwa mwalimu mkuu, Mayanga alikuwa kocha msaidizi wa klabu ya Mtibwa kwa kipindi kirefu chini ya makocha kadhaa wakiwemo Twahir Muhidin, Tom Olaba, James Sianga na Abdallah Kibaden.
  Mwalimu Mayanga ambaye pia ni mwajiriwa wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, kabla hajawa kocha alikuwa ni mchezaji wa klabu ya Mtibwa katika miaka ya tisini na ni miongoni mwa wachezaji waliyoipandisha daraja klabu ya Mtibwa kwenda ligi daraja la kwanza ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuwa ligi kuu.
  Klabu ya Mtibwa inachukua fursa hii kuwahakikishia wapenzi wake kuwa ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha inafanya vizuri zaidi msimu ujao. Aidha inachukua fursa hii kumshukuru Mecky Maxime kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi chake kama kocha mkuu wa Mtibwa.
  Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser alisema kuwa Mecky ni kocha mzuri sana mwenye kuipenda kazi yake na mwenye malengo. “kwa umri wake naamini atafika mbali sana na ni hazina kubwa kwa taifa”. Alisema Bayser na kuongeza kuwa Mecky aliuomba uongozi kujaribu changamoto mpya na uongozi ukamkubalia bila kinyongo wakiamini kuwa Mtibwa ni nyumbani kwake na siku yoyote atarudi tena.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RASMI, MAYANGA AREJESHWA MTIBWA SUGAR, MECKY AENDA KAGERA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top