• HABARI MPYA

  Sunday, July 31, 2016

  SIMBA WASIKURUPUKE, WAITAFAKARI KWA MAPANA MAREFU OFA YA DEWJI

  SIMBA SC inatarajiwa kufanya Mkutano wake Mkuu wa mwaka leo katika Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysteraby, Dar es Salaam.
  Na katika Mkutano wa leo, mjadala mkuu unatarajiwa kuwa ofa ya mfanyabiashara Mohamed Gulam Dewji anayetaka kuwekeza Sh. Bilioni 20 katika klabu hiyo ili auziwe asilimia 51 ya hisa za klabu.
  Mbunge huyo wa zamaani wa Singida Mjini, alikutana na Waandishi wa Habari juzi ofisini kwake, jengo la Golden Jubilee Towers, Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam na kuwaeleza mikakati mizuri iwapo atauziwa Simba SC, mojawapo ikiwa ni kutumia bajeti ya Sh. Bilioni 5.5 kwa msimu ili kuwapiku wapinzani Azam na Yanga.
  Rais huyo wa Kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) alisema atayafanya hayo iwapo Simba SC watakubali kumuuzia asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20.
  Alisema akiuziwa asilimia 51 ya hisa na kuwa mmiliki wa Simba, atawawezesha wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo kupewa hisa bure, ambazo wataamua wenyewe kuuza, au kununua hisa zaidi. 
  Na kwa kuwa Ofa hiyo ya tajiri huyo kijana zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes, inakuja wakati Simba SC inafanya Mkutano wake Mkuu wa mwaka leo, tuseme imekuja wakati mwafaka.
  “Shabaha yangu ni kuitoa klabu kwenye Bajeti ya Bilioni 1.2 hadi Bilioni 5.5, mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka, lazima tusajili vizuri, tuajiri kocha mzuri. Ukitenga Bilioni 4 kwa mwaka, tayari umewazidi wapinzani Azam na Yanga,”. 
  Na kuhusu Bilioni 1.5 inayobaki, Mo Dewji amesema Simba inatimiza miaka 80 tangu ianzishwe mwaka 1936, lakini haina Uwanja japo wa mazoezi tu.
  “Mimi kama mpenzi wa Simba inaniuma,
  wenzetu (Azam) wameanza juzi, lakini wana Uwanja. Mimi nitaweka Bilioni 1.5 kila mwaka ili kukamilisha ujenzi wa Uwanja ndani ya miaka mitatu ambao utakuwa wa kisasa utakaotupa fursa ya kuanzisha na miradi ya soka ya vijana,”. 
  Amesema lengo lake ni kuifanya Simba itwae ubingwa wa Afrika kwa kushindana na timu kama TP Mazembe zinazotumia Bajeti ya Sh. Bilioni 20 kwa mwaka.
  “Mimi ninaondoka, ninakwenda zangu Singida kupumzika, wao watakuwa na Mkutano Jumapili, wakikubali wasipokubali sina shida. Nitakubali kwa roho safi,”alisema Mo Dewji na kuongeza; “Wabadilishe katiba tusaini mkataba, baada ya hapo kuna taratibu ambazo zinaweza kuchukua miezi sita hadi mwaka, lakini hapa katikati kwa kuwa ntakuwa nimeridhika na mwenendo wa uendeshwaji wa klabu, na mimi pia kama mshabiki nitasaidia kwenye usajili, nasikia wanahangaika kumpata mchezaji mmoja kutoka Ivory Coast, nitawasaidia,”alisema.
  Mo amesema kwa sasa Simba inazidiwa na Yanga na Azam kwa sababu tu ya kutokuwa na fedha za kutengeneza bajeti kubwa ya uendeshwaji.
  “Kwenye usajili Simba inaweka hela ndogo, Yanga na Azam inaweka kubwa, pia hatuna uwezo wa kumlipa mshahara mzuri mchezaji, ndiyo maana baada ya kutafakari kwa kuwa mimi ni shabiki na mwanachama ningependa kuwekeza Simba ili tubadili mfumo wetu,”alisema.
  Mo Dewji alisema kwa kuwa Simba ina majengo pacha mawili Mtaa wa Msimbazi na kiwanja wa Bunju, atatumia Sh. Bilioni 5 kujenga Uwanja wa kisasa ndani ya miaka mitatu.
  “Shabaha yangu, nikichukua Bilioni 20 tukubaliane hakuna mtu ataruhusiwa kuchukua hiyo fedha. Twende tukaiweke katika akaunti maalum benki kwa miaka mitano tutapata faida ya asilimia 17.5 ambayo ni sawa Sh. Bilioni 3.5,” amesema.
  “Lakini kwa kuwa mimi ni mfanyabiashara, nina uhusiano na wafanyabiashara wenzangu, kama utakumbuka nilipokuwa mdhamini (1999 -2005) niliwaleta pia Simba Cement na benki ya NBC kudhamini Simba,”
  Mo amesema ni muhimu Simba SC kukubali ofa yake, kwa sababu amesikia wadhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wanasita kusaini Mkataba mpya na mpango wa kuishawishi benki ya NMB kudhamini unasuasua.
  “Maana yake bajeti ya klabu itashuka zaidi hadi kurudi kwenye Sh Milioni 500 au 600, hii itakuwa hatari sana kwa klabu. Hatuwezi kushindana siyo tu Afrika, bali hata Tanzania,”alisema.
  Mo Dewji ni mpenzi na mwanachama wa Simba SC, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.
  Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon kwa muda, kabla ya kuiuza kwa mfanyabishara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi.
  Ukweli ni kwamba Simba SC inahitaji fedha ili kujiinua tena na kurudisha makali yake katika soka ya Tanzania, ambayo yamepotea kwa sasa.
  Na sababu anazozitaja Mo ndiyo hizo hizo, kwamba timu imezidiwa nguvu ya kiuchumi na wapinzani Azam na Yanga matokeo yake wamejitoa kwenye mbio za mataji nchini.
  Ni kweli Simba SC inahitaji nguvu mpya – tena aina ya nguvu ambayo anataka kuileta Mo Dewji.
  Sipingani na wazo la Dewji, lakini tu kuna tatizo naliona hapa, wengi wametekwa na ofa ya uwekezaji wa Bilioni 20 na hawataki kutazama kwa undani kama itakuwa sahihi kufanya hivyo, au la.
  Kuuza asilimia 51 za hisa za klabu kwa mtu mmoja ni kuitoa kabisa Simba mikononi mwa wana Simba na kuifanya iwe mali ya mtu mmoja – hapa unazungumzia hadi sheria za uwekezaji wa aina hiyo maana yake hili si jambo la kukurupuka au kulichukulia kijuu juu.
  Tusiangalie matatizo ya leo ya Simba na tukataka kuyatatua kwa namna na gharama yoyote bila kuzingatia mustakabali mzima wa klabu.
  Mo kuwekeza Simba, au mfanyabiashara yoyote ni vizuri, lakini – lakini tu hili si suala la kulichukulia kijuu juu, linahitaji umakini wa hali ya juu, ili siku moja historia ya klabu isije ikawahukumu viongozi waliopo madarakani leo, chini ya Rais Evans Aveva. 
  Maamuzi mazito ya aina hii husababisha hadi historia ya klabu kuandikwa upya – hivyo wana Simba wanapaswa kutuliza vichwa vyao na kuamua bila shinikizo, bali kwa kuzingatia maslahi na mustakabali wa klabu yao. Nawatakia mkutano mwema Simba SC.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WASIKURUPUKE, WAITAFAKARI KWA MAPANA MAREFU OFA YA DEWJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top