• HABARI MPYA

    Sunday, July 24, 2016

    NGASSA NJIA PANDA SAUZI, MPANGO WA FREE STATE KUUZWA KAMA UMEBUMA HIVI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa bado hajui atachezea timu gani msimu ujao katikaLigi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, kufuatia mopango wa kuuzwa kwa klabu yake, Free State Stars kwa klabu ya Moroka Swallows kukwama.
    Free State Stars ya Bathlehem ilifikia makubaliano ya kuwauzia timu Moroka Swallows ya Johannesburg, lakini Bodi ya Ligi ya PSL inadaiwa kuzuia mpango huo baada ya baadhi ya taratibu kutokamilishwa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kutoka Bethlehem, Afrika Kusini, Ngassa alisema kwamba kwa sasa wachezaji wote wa Free State Stars wapo njia panda na hawajui mustakabali wao.

    “Tupo tu hapa, ila Jumatatu tumeitwa kwenye kikao na uongozi wa Free State Stars, tunatarajia kwenda kujua hatima yetu siku hiyo,”alisema Ngassa.
    Nyota huyo wa zamani wa Toto Africans, Kagera Suga, Azam FC, Simba SC na Yanga SC alisema kwamba uongozi wa Moroka Swallows ulituma basi Bethlehem wachezaji wapande waende Johannesburg wiki hii, lakini wakazuiwa na uongozi wa Free State wakiambiwa inawezekana mpango wa kuuzwa timu ukafa.
    “Sisi tunapenda zaidi kubaki katika timu tuliyoizoea. Ila kama itauzwa sawa, tutaangalia ustaarabu mwingine, lakini ukweli ni kwamba wachezaji wengi hawakufurahia mpango huo,”alisema Ngassa. 
    Baada ya kushuka daraja kwa mara ya pili ndani ya misimu miwili, mwishoni mwa msimu wa 2015/2016, Swallows imefanikiwa kurejea Ligi Kuu kwa kuinunua Free State. 
    Stars itakuwa timu ya pili kuuzwa tangu mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya Mpumalanga Black Aces kuuzwa kutoka kwa Mario na George Morfou kwenda kwa John Comitis - na sasa inajulikana kama Cape Town City FC chini ya mmiliki mpya. 
    Ngassa alijiunga na Free State Stars msimu uliopita kama mchezaji huru baada ya kumaliza Mkataba wake Yanga na wakati anajiandaa kuingia katika msimu wake wa pili kwenye mkataba wa miaka minne, timu hiyo inataka kuuzwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA NJIA PANDA SAUZI, MPANGO WA FREE STATE KUUZWA KAMA UMEBUMA HIVI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top