BODI ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba SC imeliomba Jeshi la Polisi Tanzania kuwachukulia hatua mashabiki waliomvamia Mwenyekiti wa klabu, Murtaza Ally Mangungu Abadan ya mchezo wa jana dhidi ya Esperance ya Tunisia.
Simba SC iliazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Esperance katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya jana Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Na baada ya mchezo huo kundi la mashabiki lilimvamia Manungu wakati anaondoka na kumfanyia fujo wakimtaka ajiuzulu kwa mfululizo wa matokeo mabaya ya timu.
Simba SC ilikaribia kuondoka na ushindi baada ya kuongoza 2-0 hadi mapumziko kwa mabao ya beki wa kulia, Shomari Salum Kapombe dakika ya 39 na kiungo Yusuphu Ally Kagoma dakika ya 44.
Lakini kipindi cha pili Esperance wakasawazisha mabao yote kupitia kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Mali, Aboubacar Diakité dakika ya 64 na winga Mualgeria, Kouceila Boualia dakika ya 79.
Esperance wangeweza kushinda mchezo huo kama kama si beki wa Kimataifa wa Tunisia, Hamza Jelasi kupiga juu shuti la mkwaju wa penalti dakika ya 90’+4.
Kwa matokeo hayo Simba SC inaokota pointi ya kwanza katika mchezo wa nne kufuatia kufungwa mechi zote tatu za awali wakifungwa 1-0 na Petro de Luanda ya Angola Dar ea Salaam, 2-1 na Stade Malien nchini Mali na 1-0 na Esperance nchini Tunisia.
Baada ya mchezo huo, Simba SC inasafiri kwenda Angola kuwafuata Petro de Luanda kwa mchezo wa marudiano kati ya Februari 6 na 8 Uwanja wa 11 de Novembro Jijini Luanda.
Esperance ambao kwa sare ya leo wanafikisha pointi sita — mchezo ujao watakuwa wageni wa Stade Malien Jijini Bamako kati ya Februari 6 na 8.
Ikumbukwe mechi nyingine ya Kundi D juzi Petro de Luanda walilazimishwa sare ya bila mabao na Stade Malien Uwanja wa 11 de Novembro, Luanda.
Matokeo hayo yanamaanisha Stade Malien inaendelea kuongoza Kundi D kwa pointi zake nane, ikifuafiwa na Esperance pointi sita, Petro de Luanda pointi tano na Simba SC yenye pointi moja mkiani.




.png)
0 comments:
Post a Comment