• HABARI MPYA

  Sunday, July 24, 2016

  AZAM VETERANS WAWANIA NUSU FAINALI KOMBE LA FRESCO LEO

  MICHUANO ya timu za maveterani ya Azam Fresco Cup, inatarajia kuendelea leo, wenyeji Azam Veteran wakisaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali kwa kukipiga na Mbagala Veteran Saa 9.30 Alasiri Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mchezo huo wa Kundi A utafuatiwa na mwingine kati ya TFF Veteran na Binslum Tyres utakaoanza kutimua vumbi kuanzia saa 11.00 jioni na ule wa funga dimba utawahusisha Yanga Veteran na Chamazi Veteran (saa 12.30 jioni).
  Kikosi cha Azam Veterans ambacho kinashuka dimbani leo Chamazi
  Tegemeo la mabao la Azam Veterans, Abdulkarim Amin 'Popat'

  Huo utakuwa ni mchezo wa pili wa Azam Veteran kwenye michuano hiyo, ambapo katika fungua dimba iliichapa Simba Veteran mabao 3-2 na ushindi wowote Jumapili ijayo utaifanya kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ikiwa kinara wa kundi lake.
  Michuano hiyo ya wiki tatu, itamalizia mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi wiki ijayo, kwa Simba kucheza na Mbagala (saa 11.00 jioni) na Azam kukipiga na Mbagala Kuu (saa 12.30 jioni), zote zikifanyika Julai 30 mwaka huu, huku zile za Julai 31 zikiwahusisha Yanga dhidi ya Binslum (saa 11.00 jioni) na TFF watakaoumana na Chamazi (saa 12.30 jioni).  
  Baada ya mechi hizo za makundi, hatua ya nusu fainali itafuatia kuanzia Agosti 6 mwaka huu kwa washindi wawili wa juu wa kila kundi kupita na kuunda timu nne, ambazo zitatengeneza mechi mbili.
  Mechi ya kwanza itakuwa kati ya mshindi wa Kundi A na mshindi wa pili wa Kundi B huku mshindi wa kwanza wa Kundi B akikutana na msshindi wa pili wa Kundi A, ambapo mechi hizo zitahitimishwa kwa mchezo wa fainali utakaofanyika siku ya Sherehe ya Nane Nane (Agosti 8 mwaka huu).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM VETERANS WAWANIA NUSU FAINALI KOMBE LA FRESCO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top