• HABARI MPYA

    Saturday, July 23, 2016

    SAMATTA: NATAKA MWAKANI NICHEZE LIGI YA MABINGWA ULAYA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Goal’ amesema lengo lake mwakani ni kucheza kwa mara ya kwanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya mwaka huu kuanza kucheza Europa League.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwa simu kutoka Ubelgiji baada ya timu yake kuitoa Buducnost ya Montenegro kwa penalti 4-2 Uwanja wa Pod Goricom mjini Podgorica katika mchezo wa marudiano Raundi ya Pili ya mchujo wa kufuzu hatua ya makundi ya Europ League, Samatta alisema kwamba amefurahi kwa matokeo hayo na sasa anaangalia mbele kuisaidia zaidi Genk ili ifike mbali kwenye michuano hiyo.
    Mbwana Samatta amesema mwakani anataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya

    “Kwa kweli nimejisikia fresh, maana ngoma ilikuwa ngumu na pia ninajisikia vyema, kwani ninazidi kupata uzoefu wa mashindano tofauti pia ni kitu kinachonifanya nionekane sehemu nyingi tofauti,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba SC za Dar es Salaam.
    Timu hizo zilifikia kwenye matuta baada ya sare ya jumla ya 2-2, Genk ikianza kushinda 2-0, mabao ya Neeskens Kebano kwa penalti dakika ya 16 na Samatta dakika ya 79 Alhamisi wiki iliyopita kabla ya Buducnost kulipa kisasi kwa ushindi wa 2-0, mabao ya Radomir Dalovic dakika ya kwanza na Milos Raickovic dakika ya 39.
    Katika mikwaju ya penalti, waliofunga upande wa Genk ni Thomas Buffel, Bryan Heynen, Samatta na Dries Wouters ya mwisho, wakati za Buducnost zilifungwa na Risto Radunovic na Radomir Dalovic, huku Momcilo Raspopovic  na Luka Mirkovic wakikosa.
    Genk ilimaliza mchezo huo pungufu baada ya kungo wake Mghana, Bennard Yao Kumordzi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 na sasa itamenyana na Cork City FC ya Ireland katika Raundi ya Tatu, mechi ya kwanza ikichezwa Julai 28 nyumbani na marudiano Agosti 4 ugenini. Ikumbukwe timu zitakazoshinda zitakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi, ambako sasa vigogo kama Manchester United ya England wataanzia huko.
    Na kuhusu hatua inayofuata, Samatta alisema; “Wapinzani wajao siwafahamu kabisa, lakini nadhani watakuwa wazuri pia, kwani mashindano haya ni ngumu kukutana na timu nyepesi,”alisema.
    Aidha, Samatta aliyeshinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika Januari mwaka huu baada ya kuipa ubingwa wa Afrika TP Mazembe ya DRC  mwaka jana jana na kuibuka mfungaji bora alisema, mipango yake sasa ni kupigania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.
    “Matarajio yetu kama timu ni kuwa na kipindi chenye mafanikio ndani ya msimu huu, nami binafsi kama mimi napenda ndani ya msimu huu niwe na rekodi nzuri za mabao na wastani mzuri wa mechi na kuisaidia timu yangu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani,”alisema
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: NATAKA MWAKANI NICHEZE LIGI YA MABINGWA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top