• HABARI MPYA

    Sunday, July 24, 2016

    AME ALI SASA NJIA MOJA KUELEKEA SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAAM
    SIMBA SC imeendelea na harakati za kuimarisha kikosi chake na sasa ipo kwenye hatua za mwishoni za kumsajili mshambuliaji wa Azam FC, Ame Ali ‘Zungu’.
    Ame Ali amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake Azam FC, lakini Simba SC imepeleka ofa ya kumchukua baada ya mazungumzo ya awali na uongozi wa timu ya Chamazi.
    Vyanzo vya habari kutoka timu zote vimesema kwamba kuna uwezekano mkubwa ndani ya siku mbili hizi, Ame akajiunga na Simba SC baada ya kukamilisha usajili wake kutoka Azam FC, iwe wa moja kwa moja au mkopo. 
    Ame Ali (katikati) akiwa na wachezaji wenzake wa Azam FC
    Mwishoni mwa wiki, Simba ilileta wachezaji wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kiungo Sanga Bahende na mshambuliaji Cedrick Masanga, wote kutoka FC Lupopo ya Lubumbashi.
    Wakongo hao wanafanya idadi ya wachezaji wa kigeni waliokuja kwa majaribio Simba kufika saba, baada ya mabeki Mzimbabwe, Method Mwanjali, Janvier Besala Bokungu, kiungo Mussa Ndusha wote kutoka DRC, washambuliaji Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast na Ndjack Anong Guy Serges kutoka Cameroon.
    Simba SC imeweka kambi mjini Morogoro kujiandaa na msimu mpya na mbali na wachezaji hao wa kigeni, kuna wapya wengine ambao ni pamoja na watatu waliosajiliwa kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, wote viungo Muzamil Yassin, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim na Shizza Kichuya na Jamal Mnyate kutoka Mwadui FC. 
    Wengine ni Moses Chibandu, Said Mussa, Kelvin Falu, Vincent Costa wote wapya pamoja na wa zamani Nahodha Mussa Hassan Mgosi, Juuko Murshid, Vincent Angban, Awadh Juma, Said Ndemla, Peter Mwalyanzi, Peter Manyika, Dennis Richard, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hijja Ugando, Novatus Lufunga, Mwinyi Kazimoto, Danny Lyanga na Ibrahim Hajib.
    Na Masanga na Bahende wanatua wakati Mrundi Laudit Mavugo anayetakiwa na Simba akidaiwa kutimkia Ufaransa kufanya mipango ya kujiunga na klabu ya Tours ya Ligi Daraja la Pili, maarufu kama Ligue 2.
    Mavugo amekwenda Ufaransa wakati tayari Simba SC wamesema wamekwishaingia Mkataba na mchezaji huyo kuanza kuwatumikia kuanzia msimu ujao.
    Bado haijulikani Simba SC itachukua gani kwa Mavugo, kwa kuwa makubaliano yao na mchezaji huyo bado yanafanywa siri ili kuepuka vikwazo kutoka klabu yake, Vital'O.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AME ALI SASA NJIA MOJA KUELEKEA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top