• HABARI MPYA

  Friday, July 29, 2016

  MO DEWJI ATANGAZA BONGE LA OFA SIMBA SC, ANATAKA KUZIPOTEZA KABISA AZAM NA YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MFANYABIASHARA Mohamed Gulam Dewji anataka kutumia bajeti ya Sh. Bilioni 5.5 kwa msimu kwa ajili ya Simba SC, ili kuwapiku wapinzani Azam na Yanga.
  Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, amesema hayo leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, ofisini kwake, jengo la Golden Jubilee Towers, Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.  
  Na Rais huyo wa Kapuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) amesema atayafanya hayo iwapo Simba SC watakubali kumuuzia asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20.
  Na amesema akiuziwa asilimia 51 ya hisa na kuwa mmiliki wa Simba, atawawezesha wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo kupewa hisa bure, ambazo wataamua wenyewe kuuza, au kununua hisa zaidi. 
  Mo Dewji akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

  Na o ofa hiyo ya tajiri huyo kijana zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes, inakuja wakati Simba SC itakuwa na Mkutano wake Mkuu wa mwaka Jumapili wiki hii mjini Dar es Salaam.
  “Shabaha yangu ni kuitoa klabu kwenye Bajeti ya Bilioni 1.2 hadi Bilioni 5.5, mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka, lazima tusajili vizuri, tuajiri kocha mzuri. Ukitenga Bilioni 4 kwa mwaka, tayari umewazidi wapinzani Azam na Yanga,”. 
  Na kuhusu Bilioni 1.5 inayobaki, Mo Dewji amesema Simba inatimiza miaka 80 tangu ianzishwe mwaka 1936, lakini haina Uwanja japo wa mazoezi tu.
  “Mimi kama mpenzi wa Simba inaniuma,
  wenzetu (Azam) wameanza juzi, lakini wana Uwanja. Mimi nitaweka Bilioni 1.5 kila mwaka ili kukamilisha ujenzi wa Uwanja ndani ya miaka mitatu ambao utakuwa wa kisasa utakaotupa fursa ya kuanzisha na miradi ya soka ya vijana,”. 
  Amesema lengo lake ni kuifanya Simba itwae ubingwa wa Afrika kwa kushindana na timu kama TP Mazembe zinazotumia Bajeti ya Sh. Bilioni 20 kwa mwaka.
  “Mimi ninaondoka, ninakwenda zangu Singida kupumzika, wao watakuwa na Mkutano Jumapili, wakikubali wasipokubali sina shida. Nitakubali kwa roho safi,”alisema Mo Dewji na kuongeza; “Wabadilishe katiba tusaini mkataba, baada ya hapo kuna taratibu ambazo zinaweza kuchukua miezi sita hadi mwaka, lakini hapa katikati kwa kuwa ntakuwa nimeridhika na mwenendo wa uendeshwaji wa klabu, na mimi pia kama mshabiki nitasaidia kwenye usajili, nasikia wanahangaika kumpata mchezaji mmoja kutoka Ivory Coast, nitawasaidia,”alisema.
  Mo Dewji akizungumza na Waandishi wa Habari leo 
  Mo amesema kwa sasa Simba inazidiwa na Yanga na Azam kwa sababu tu ya kutokuwa na fedha za kutengeneza bajeti kubwa ya uendeshwaji.
  “Kwenye usajili Simba inaweka hela ndogo, Yanga na Azam inaweka kubwa, pia hatuna uwezo wa kumlipa mshahara mzuri mchezaji, ndiyo maana baada ya kutafakari kwa kuwa mimi ni shabiki na mwanachama ningependa kuwekeza Simba ili tubadili mfumo wetu,”alisema.
  Mo Dewji amesema kwa kuwa Simba ina majengo pacha mawili Mtaa wa Msimbazi na kiwanja wa Bunju, atatumia Sh. Bilioni 5 kujenga Uwanja wa kisasa ndani ya miaka mitatu.
  “Shabaha yangu, nikichukua Bilioni 20 tukubaliane hakuna mtu ataruhusiwa kuchukua hiyo fedha. Twende tukaiweke katika akaunti maalum benki kwa miaka mitano tutapata faida ya asilimia 17.5 ambayo ni sawa Sh. Bilioni 3.5,” amesema.
  “Lakini kwa kuwa mimi ni mfanyabiashara, nina uhusiano na wafanyabiashara wenzangu, kama utakumbuka nilipokuwa mdhamini (1999 -2005) niliwaleta pia Simba Cement na benki ya NBC kudhamini Simba,”
  Mo amesema ni muhimu Simba SC kukubali ofa yake, kwa sababu amesikia wadhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wanasita kusaini Mkataba mpya na mpango wa kuishawishi benki ya NMB kudhamini unasuasua.
  “Maana yake bajeti ya klabu itashuka zaidi hadi kurudi kwenye Sh Milioni 500 au 600, hii itakuwa hatari sana kwa klabu. Hatuwezi kushindana siyo tu Afrika, bali hata Tanzania,”amesema.
  Mo Dewji ni mpenzi na mwanachama wa Simba SC, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.
  Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon kwa muda, kabla ya kuiuza kwa mfanyabishara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI ATANGAZA BONGE LA OFA SIMBA SC, ANATAKA KUZIPOTEZA KABISA AZAM NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top