• HABARI MPYA

    Wednesday, July 27, 2016

    VIONGOZI HOVYO, MIPANGO YA HOVYO HATA MATOKEO NI HOVYO TU!

    RASMI, kuanzia jana mashabiki wa Yanga SC wamekata tamaa ya timu yao kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika mwaka huu.
    Hiyo inafuatia Yanga SC kuendelea kuboronga katika mechi za Kundi A baada ya jana kufungwa mabao 3-1 na wenyeji Medeama FC Uwanja wa Essipong Sports mjini Sekondi-Takoradi, Ghana.
    Huo unakuwa mchezo wa nne mfululizo Yanga inacheza bila kushinda, ikifungwa mara tatu na kutoa sare moja. 
    Yanga ilianza kwa kufungwa na 1-0 na Mo Bejaia nchini Algeria kabla ya kufungwa tena 1-0 na TP Mazembe na kutoka sare ya 1-1 na Medeama mjini Dar es Salaam kabla ya kipigo cha jana.
    Mabao ya Medeama yalifungwa na Daniel Amoah dakika ya saba aliyemalizia kona ya Enock Atta Agyei na Abbas Mohammed mawili dakika ya 23 na 37, wakati la Yanga lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 25 kwa penalti baada ya Mzambia Obrey Chirwa kuangushwa kwenye boksi. 
    Na Yanga ingepigwa 4-1 kama si kipa Deo Munishi ‘Dida’ kupangua mkwaju wa penalti wa Malik Akowuah dakika ya 10.
    Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inaondoka kwenye mbio za kuwania Nusu Fainali na sasa inacheza kukamilisha ratiba. 
    Mazembe inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na MO Bejaia na Medeama ambazo zote kila moja ina pointi tano, wakati Yanga ina pointi moja. 
    Mazembe watakuwa wenyeji wa Bejaia leo Lubumbashi wakihitimisha mechi za mzunguko wa nne.
    Nafasi ya pili sasa iko wazi kwa Bejaia na Medeama – na si ajabu sasa Yanga wakatumika kama mtaji zaidi wa timu nyingine kuvuna pointi.
    Bejaia watakuja Dar es Salaam wakitoka Ghana wakiwa wanahitaji pointi za kuwapeleka Nusu Fainali mbele ya Yanga ambayo itakuwa ikipigania japo kushinda mechi moja ya kundi.
    Tumeiona Yanga hadi jana na hakuna tofauti yoyote na Yanga ile iliyopigana hadi kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi.
    Kinachoonekana, Yanga wameingia kwenye mashindano makubwa kuliko uwezo wao wa sasa – na ni uwezo wa timu kwa ujumla, yaani kuanzia benchi la Ufundi, wachezaji na hata viongozi.
    Uwekezaji wa ndani ya Medeama, MO Bejaia na TP Mazembe huwezi kulinganisha na ubabaishaji unaoendelea Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Yussuf Manji.
    Kama timu haina tu Uwanja wa uhakika wa mazoezi, kuna ajabu gani isiposhinda mechi hata moja Kundi A? 
    Sera za uenedeshaji wa klabu tatu wapinzani wa Yanga katika Kundi A zipo tofauti – uendeshwa wa Medeama si sawa na wa Bejaia wala Mazembe, kila moja ina sera na falsafa zake.
    Na je sera na falsafa za timu ipi utafananisha na za Yanga kati ya MO Bejaia, Medeama na Mazembe?
    Tutakuwa tunakosea sana kuilaumu, au kuishutumu Yanga kwa matokeo waliyoyapata Kundi A Kombe la Shirikisho, kwa sababu ndiyo waliyoyastahili.
    Viongozi wa hovyo, wenye mipango ya hovyo hata matokeo yao kwenye mashindano makubwa kama haya tarajia yatakuwa ya hovyo tu.
    Yanga watarudi tena mwakani kwenye michuano ya Afrika, lakini si ajabu wasifike hatua waliyofika mwaka huu, yaani watatolewa mapema kwa sababu tayari sote tunajua wahenga walisema; “Bahati haiji mara mbili”.
    Kwa staili ya uongozaji wa Manji na aina ya viongozi waliopo madarakani Yanga, kuanzia wa kuchaguliwa hadi wa kuajiriwa, sioni vipi timu hiyo itafanya vizuri kwenye michuano mikubwa ya Afrika zaidi ya hivi. Labda wabadilike.
    Mashabiki wa Yanga kwa sasa wana hasira za matokeo mabaya ya timu yao, kidogo wanaweza kusoma habari na makala chungu kama hizi ili kutaka kujua undani wa matatizo ya timu yao. Ni mengi.
    Lakini kwa matatizo hayo hayo, wakirudi kwenye mashindano yetu yale ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga wataendelea kutesa. 
    Ukweli ni kwamba, Manji ana fedha lakini kama hawezi kuwa na nidhamu, mipango, sera na falsafa nzuri hawezi kuisaidia Yanga kufikia kiwango cha kuitwa klabu kubwa Afrika. 
    Na ndiyo maana ninasema kwa hali halisi ilivyo, Yanga imejitahidi sana hata kwa matokeo waliyoyapata hadi sasa na wanastahili pongezi, kwani walikuwa wa kufungwa kuliko walivyofungwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIONGOZI HOVYO, MIPANGO YA HOVYO HATA MATOKEO NI HOVYO TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top