• HABARI MPYA

    Thursday, July 28, 2016

    NI MIAKA NANE TANGU TUIPOKEE AZAM LIGI KUU, LAKINI WAKONGWE WANASUBIRI!

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jana ilitimiza miaka nane tokea ipande rasmi Ligi Kuu mwaka 2008 tarehe kama ya jana (Julai 27), ambapo ilipanda baada ya kuichapa Majimaji ya Songea mabao 2-0, mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
    Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo yote yalifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ yote yakitokana mipira ya adhabu ndogo, ambapo ushindi huo uliifanya Azam FC kuongoza kituo cha Dodoma kwa kumaliza ikiwa na jumla ya pointi saba.
    Azam FC wakifurahia taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
    Kutoka kulia Khamis Mcha 'Vialli', David Mwantika na Kipre Herman Tchetche wakifurahia ushindi dhidi ya Ruvu Shooting msimu wa 2013 -2014 ambao waliibuka mabingwa

    Pointi hizo saba zilipatikana baada ya Azam FC kuifunga Majimaji (2-0), ikaichapa tena Kijiweni FC ya Mbeya (2-1) na sare bila ya kufungana aliyoipata dhidi ya Mbagala Market ya Mbagala jijini Dar es Salaam (hivi sasa African Lyon).
    Kikosi cha Azam FC kilichocheza siku ya kupanda daraja kiliundwa na kipa Idd Abubakar ambaye ni Kocha Msaidizi wa makipa wa Azam FC hivi sasa, Malika Ndeule, Paulo Nyangwe ‘Mitindo’, Meneja wa timu hiyo hivi sasa Luckson Kakolaki, Boniface Pawasa (C), Adam Ngido ‘Popa’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Steven Nyenge, John Bocco ‘Adebayor’, Kassim Kilungo na James Adriano.
    Mpaka sasa wachezaji walobakia ni wawili tu kutoka kwenye kikosi hicho, nahodha Bocco na Sure Boy, ambao mpaka sasa wametimiza mwaka wa nane wakiwa na Azam FC.
    Wakati huo Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati ilikuwa chini ya makocha Mohamed Seif ‘King’ na Msaidizi wake, Habib Kondo, ambapo mechi hiyo ya mwisho ilishududiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni.
    Ikiwa na miaka nane tu tokea ipande, Azam FC imefanikiwa kuleta upinzani mkali kwa vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, ambapo mwaka huu iliweza kufuzu kwa mara ya tano mfululizo kushiriki michuano mikubwa ya Ngazi ya Klabu Barani Afrika na hii ni mara baada ya kushika nafasi mbili za juu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), lakini kwa mwaka huu ikifuzu kufuatia kuwa washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).
    Ndani ya miaka nane tu Ligi Kuu, Azam FC inayomilikiwa na familia ya Mfanyabiashara Maarufu Afrika Mashariki na Kati, Alhaji Said Salim Bakhresa, ambaye ni mmiliki wa Makampuni ya Bakhresa, imeweza kutwaa mataji mawili makubwa, moja likiwa la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14 ikitwaa kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa mchezo wowote.
    Mechi ya mwisho iliyoipa ubingwa huo Azam FC ilikuwa ni dhidi ya Mbeya City Aprili 13, 2014 walipoifunga mabao 2-1 ndani ya Uwanja wa Sokoine, Mbeya yakifungwa na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba huku John Bocco akiweka rekodi nyingine ukiacha ile ya kuipandisha daraja timu kwa kutupia bao la ushindi likiwa la pili kwenye mchezo huo.
    Taji lingine ni lile la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) walilotwaa Agosti 2 mwaka jana kwa kuwachapa mabingwa wa Kenya Gor Mahia mabao 2-1, Bocco alijiwekea rekodi nyingine tena kwa kufunga bao la kwanza lililowapa nguvu ya kutwaa ubingwa huku Kipre Tchetche akihitimisha kwa kufunga la pili kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo.
    Mbali na mataji hayo makubwa, pia Azam FC ambayo ina kituo cha kukuza vipaji (Academy) kinachofanya vizuri kwa kutoa wachezaji bora nchini, imefanikiwa kutwaa makombe mengine madogo, ubingwa wa Mapinduzi Cup mara mbili (2012 na 2013), Kombe la Hisani lililofanyika mjini Kinshasa, DR Congo (2012) pamoja na ubingwa wa Kombe Maalum la timu nne lililofanyika jijini Ndola Zambia mwaka huu.
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB pamoja na kinywaji safi cha Azam Cola, ilitwaa taji hilo nchini Zambia mbele ya wenyeji Zesco United na Zanaco pamoja na mabingwa wa Zimbabwe msimu uliopita Chicken Inn.
    Mbali na makombe ya timu kubwa, Azam Academy nayo imeitangaza vilivyo Azam FC kwani wao ndio mabingwa wa kihistoria wa iliyokuwa michuano ya vijana ya timu za Ligi Kuu (Uhai Cup) baada ya kutwaa mara nne huku pia ikitwaa ubingwa wa vijana wa Rollingstone mwaka 2014.
    Azam Academy pia imetwaa taji la kwanza la michuano ya Azam Youth Cup lilioanza mwaka huu baada ya kuzishinda timu nne shiriki, Football For Good Academy (Uganda), Ligi Ndogo Academy (Kenya) na Future Stars Acedemy (Arusha).
    Kuhusiana na makocha waliowahi kuinoa Azam FC, mpaka sasa ni watano, ambao ni Mzawa Mohamed Seif ‘King’, Mbrazil Neider Santos, Itamar Amorin, Mwingereza Stewart Hall, Mcameroon Joseph Omog na Zeben Hernandez kutoka Hispania ambaye amekabidhiwa timu hiyo hivi sasa kwa ajili ya msimu ujao (2016-2017).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MIAKA NANE TANGU TUIPOKEE AZAM LIGI KUU, LAKINI WAKONGWE WANASUBIRI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top