• HABARI MPYA

  Friday, July 01, 2016

  OMOG ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC NA KUSEMA; “SASA MATAJI YOTE MSIMBAZI”

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog leo amesaini Mkataba wa miaka miwili kufundisha Simba SC na amesema atarejesha furaha ya mataji Msimbazi.
  Omog amesaini mchana wa leo katika hoteli ya Regency, Mikocheni, Dar es Salaam mbele ya Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva na akasema sera yake ni ushindi na mataji.
  “Nimefurahi kusaini Mkataba wa kufanya kazi Simba SC, ni klabu kubwa na ninaamini kwa ushirikiano wa pamoja na uongozi, wanachama na wachezaji tunaweza kufanikiwa,”amesema Omog aliyewasili usiku wa kuamkia leo.
  Rais wa Simba SC, Evans Aveva (katikati) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo kocha Omog baada ya kusaini Mkataba. Kulia ni Katibu Mkuu, Patrick Kehemele
  Omog (katikati) akiupitia Mkataba kabla ya kusaini. Kulia ni Rais Aveva na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch

  Simba inakuwa klabu ya pili kwa Omog kufundisha Tanzania baada ya awali kuwa na Azam FC, aliyoiongoza kwa msimu mmoja na nusu ikishinda mechi 30 kati ya 55 za mashindano yote, sare 14 na kufungwa 11.
  Mwalimu huyo aliyeipa Leopard FC ya Kongo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014, enzi zake alichezea Yaounde na ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, INJS mjini Yaounde, Cameroon. 
  Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou walipata Stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987. 
  Aliporejea nchini mwake, Joseph Marius Omog, alifundisha timu kadhaa kama Fovu ya Baham na Aigle ya Menoua na akazifikisha fainali ya Kombe la Cameroon klabu zote. 
  Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, Simba Wasiofungika chini ya Nahodha Samuel Eto’o haswa kutokana na kujua kwake Kijerumani, kwa sababu kocha huyo alikuwa hazungumzi Kiingereza wala Kifaransa, lugha zinazotumika nchini humo. 
  Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa baada kuondoka kwa Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na matokeo mabaya na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
  Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na AC Leopard ya Kongo, ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe mwaka huo huo na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. 
  Na akafanikiwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe hilo la Afrika mwaka 2012 kwa kuifunga Djoliba ya Mali mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kutengeneza ushindi wa jumla wa 4-3. Mwaka 2014 alijiunga na Azam FC ambayo aliipa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu.  
  Je, mafanikio hayo atayahamishia Simba? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OMOG ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC NA KUSEMA; “SASA MATAJI YOTE MSIMBAZI” Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top