• HABARI MPYA

    Sunday, July 10, 2016

    ANACHOPASWA, SICHO ANACHOFANYA JERRY MURO BAADA YA ADHABU TA TFF

    MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3, baada ya kupatikana na makosa ya kimaadili.
    Jerry alifungiwa baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Julai 7, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.
    Na alifungiwa baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati ya Ogunde.
    Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini akakaidi kulipa hadi siku ya kikao hicho.
    Kwa kosa hilo alihukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
    Katika shitaka hilo, Jerry alidaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    “Alihamasisha mashabiki wa Yanga kufanya vurugu katika mechi dhidi ya Maembe kwa kusema mashabiki wa Simba hawana haki ya kuingia uwanjani, kwa sababu Uwanja umekodiwa na Yanga. Na hili Kamati ilijiridhisha baada ya kusikiliza sauti zake alipokuwa akihojiwa na vituo vya Redio,”kilisema chanzo kutoka kwenye Kamati hiyo.
    Kwa kosa hilo Jerry Muro alifungiwa mwaka mmoja pia na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 ingawa adhabu zote zinakwenda sambamba – maana yake atakuwa pembeni na masuala ya soka kwa mwaka mmoja tu.
    Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni.
    “Kamati ilisikiliza kwa makini taarifa zake alipokuwa anazungumza na vituo vya Redio na kugundua alikuwa sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kilisema chanzo.
    Hata hivyo, Jerry Muro alihukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na ilidaiwa hakutoa taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
    Badala yake, imeelezwa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika mapema leo kabla ya kikao kwa ajili ya kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha makaburi ya wazee wake. 
    Lakini Kamati iliamua kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua. Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF.
    Saa chache baada ya kuvuja kwa taarifa za Kamati juu ya kikao hicho, Jerry Muro tena akaibuka kwenye vyombo vya Habari kuanza kujibu.
    Kwanza akasema hajapata taarifa rasmi, lakini akajibu juu ya kile anachoamini si sahihi katika maamuzi ya Kamati.
    Kimsingi soka inaendeshwa kwa utaratibu na ni utaratibu huo huo uliomfikisha Muro Kamati ya Maadili.
    Uzuri ni kwamba, Kamati ya Maadili imeweka wazi, Muro anaweza kukata Rufaa iwapo hajaridhishwa na hukumu hiyo.
    Na kwa utaratibu wa soka unaonzia ngazi ya chini kabisa – labda klabu, vyama vya wilaya, mikoa hadi taifa, Muro anaweza kusogea ngazi za juu hadi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) iwapo hataridhishwa na Kamati ya Rufaa ya TFF.
    Na kwa kuwa huo ni utaratibu ulio wazi – huwezi kuona sababu ya Muro kujiingiza katika mtego wa kufanya kosa lingine, ambalo linaweza kumfanya apoteze hata haki anazostahili.
    Mfano ni yaliyomtokea Michael Richard Wambura wakati anagombea Urais wa Simba SC mwaka 2014, alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kwa tuhuma za makosa ya kimaadili.
    Lakini akakata rufaa TFF na kushinda hivyo kurejeshwa – hata hivyo, baada ya kurejeshwa akaenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari maneno ambayo yalitafsiriwa kama ya kufanya kampeni kabla ya muda na Kamati ya Uchaguzi ya Simba ikamuengua tena na hata TFF haikuweza kumsaidia tena.
    Wazi sakata la Muro na TFF linafuatiliwa na wadau wengi wa soka – na wapo ambao wanalitazama kishabiki na wengine wanalitazama kwa ufasaha na katika hali ya kawaida.
    Mara nyingi wasio na mihemuko ya kishabiki au maslahi katika masuala huwa hawazungumzi zaidi ya kufuatilia picha inavyoendelea.
    Ila kwa wenye maslahi yao katika hili, yawe ya kishabiki au vyovyote ndiyo mara nyingi hufungua mijadala mipana – lakini Muro anapaswa kutumia akili yake ya kuzaliwa na ya darasani, kama ambavyo yeye mwenyewe hutamba ‘amesoma sana’.
    Hana sababu ya kwenda Redioni au kwenye TV kujibizana na TFF, bali anapaswa kufuatilia hukumu yake na baada ya hapo akate Rufaa. Alamsiki.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ANACHOPASWA, SICHO ANACHOFANYA JERRY MURO BAADA YA ADHABU TA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top