TIMU ya Simba SC imetoa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Petro de Luanda katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa usiku huu Uwanja wa Novemba 11 Jijini Luanda nchini Angola.
Beki wa kati, Pedro Manuel da Mota Pinto alianza kuifungia Petro de Luanda dakika ya 13, kabla ya mshambuliaji Muivory Coast, Alain Anicet Oura kuisawazishia Simba SC dakika ya 81.
Simba SC ilipata pigo la mapema kwenye mchezo huo baada ya beki wake, Shomari Kapombe kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 40 na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Kwa matokeo hayo, Petro de Luanda inafikisha pointi sita katika mchezo wa tano ikibaki nafasi ya tatu kwa kuzidiwa wastani wa mabao na Espérance de Tunis ya Tunisia ambayo ina mechi moja mkononi— na Simba inafikisha pointi mbili katika mchezo wa tano pia na inaendelea kushika mkia.
Kesho vinara wa Kundi D, Stade Malien Mali wenye pointi nane watawakaribisha Espérance de Tunis Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako nchini Mali.
Simba itamalizia nyumbani dhidi ya Stade Malien Februari 14 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam na Espérance de Tunis watamalizia nyumbani pia na Petro de Luanda siku hiyo hiyo Uwanja wa Hammadi Agrebi Jijini Tunis.


.png)
0 comments:
Post a Comment