• HABARI MPYA

    Sunday, July 03, 2016

    NI WAKATI WA MALINZI KUJITATHMINI NAMNA ANAVYOIENDESHA SOKA YETU

    SOKA ya Tanzania hatimaye imerejea kwenya zama za migogoro na kutoheshimu misingi ya utawala bora, baada ya muongo mmoja wa utulivu chini ya uongozi wa Leodegar Chilla Tenga.
    Moja kati ya mambo makubwa katika utawala wa Tenga Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo yatamfanya akumbukwe daima ni kukijengea heshima chombo hicho na kuwa moja ya taasisi bora nchini.
    Tenga alifuta kabisa migogoro na kujenga misingi ya utawala bora ndani ya soka ya Tanzania kwa kuhakikisha Katiba zote zilizokuwepo zinabadilishwa.
    Na akafanikiwa kuusimika mfumo wa uendeshwaji klabu kisasa na kwa kiasi kikubwa, pamoja na kuwapo mizizi sugu ya mapenzi ya klabu kongwe nchini Simba na Yanga, lakini wakati wa Tenga hilo maarufu kama Usimba na Uyanga halikuonekana sana.
    Kuna maeneo Tenga alifeli na ilionekana wazi – lakini si katika utawala bora wenye kufuata misingi ya Katiba na sheria.
    Hilo lilizivutia hata taasisi na kampuni nyingine kubwa kuanza kujihusiaha na soka yetu na ndiyo wakati ambao tulishuhudia Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ikiingia Mkataba wa kuzidhamini timu za Simba na Yanga na Taifa Stars (timu ya taifa).
    Awali ya hapo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) nayo iliweka rekodi ya kuwa mdhamini wa kwanza rasmi wa Taifa Stars.
    Tukaondoka kwenye zama za kuendesha timu ya taifa kwa misaada ya wafadhili wenye asili ya Kiasi na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi.
    Tukaondoka kwenye zama za kuziona Simba na Yanga zikijiendesha kwa kutegemea misaada ya wafadhili wenye asili ya Kiasi.
    Taratibu taswira ya soka ya Tanzania ilianza kubadilika – na ndiyo maana ikafika wakati watu wakawa wanajiuliza baada ya utulivu huu, Tenga anashindwaje kuivusha hatua nyingine soka ya nchi hii?
    Na ndiyo hapo baadhi tukatamani mabadiliko, tukiaminia uwezo wa Tenga umeishia katika yale aliyoyafanya, tukiamini anastahili kupokewa kijiti na mtu ambaye labda atatuvusha hatua zaidi kwenda mbele.
    Na huo ndiyo mwanzo wa kumpata Jamal Emil Malinzi, Rais wa sasa wa TFF, ambaye awali alikuwa Katibu wa klabu kongwe nchini, Yanga.
    Sera zake nzuri zilizogonga ukuta Yanga kutokana na mitazamo ya kizamani iliyokuwa imekumbatiwa na wanachama wa klabu hiyo, tuliamini ingesaidia TFF.
    Hata sera alizokuwa ananadi wakati wa kampeni zake za Urais wa TFF, zilikuwa zimebeba matumaini makubwa na zilionyesha ni aina ya mtu ambaye anastahili kumpokea kijiti Tenga.      
    Lakini miaka mitatu baadaye sasa, soka ya Tanzania chini ya Malinzi imerudi kwenye zama za migogoro, malumbano na Usimba na Yanga.
    Heshima ya soka yetu iliyojengwa chini ya utawala wa Tenga imeanza kupotea taratibu.
    Nidhamu imepotea kabisa na sasa si mdau, chama cha wilaya, mkoa au klabu inayoweza kusita kutunishiana msuli na TFF ya Malinzi.
    Sasa umefika wakati Malinzi anaonekana kutumia muda mwingi kupambana na wanachama wake, kwa maana ya klabu na vyama vya wilaya na mikoa – na jiulize muda unaobaki unamtosha kushughulikia maendeleo ya soka ya nchi hii?
    Tumerudi mahala ambapo nchi nyingine zinajua Tanzania kuna migogoro ya kisoka. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) sasa nao wanajua Tanzania kuna migogoro.
    Na mbaya zaidi inafikia viongozi wa klabu wanazikashifu hadi taasisi hizo kubwa, CAF na FIFA tu kutokana na tofauti zao na TFF.
    Tuliwasikia Yanga wakisema klabu yao ni kubwa kuliko CAF na tukawasikia tena wakisema FIFA inanuka rushwa – tu kwa sababu ya tofauti zao na TFF.
    Kama si tofauti zao na TFF, Yanga wangepata sababu gani ya kujiona wakubwa kuliko CAF au kusema FIFA inanuka rushwa hata kama ni kweli?
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi anapaswa kufahamu kwamba mipango yake yote inaweza kufeli, iwapo hatarudisha heshima ndani ya TFF kwa sababu migogoro itamvuruga.
    Malinzi sasa anaonekana kabisa anasita kuchukua hatua hata dhidi ya watu waliofanya makosa kweli ya kimaadili, kwa sababu ya hatua alizowahi kuchukua nyuma kutiliwa shaka.
    Na heshima yake inashuka taratibu mbele ya wadau wa soka kutokana na kwamba anaonekana si mtu wa misimamo haswa. 
    Na huo ndiyo mwanzo wa soka ya Tanzania kupoteza dira – kitu ambacho hatupendi.
    Simba wapo dhidi ya Malinzi kwa muda na sasa Yanga nao wapo dhidi yake – sahau kuhusu wadau wengine mbalimbali kama Kassim Dewji ambao pia wanampinga.
    Naamini wakati umefika sasa Malinzi ajitathmini upya namna anavyoendesha soka ya Tanzania na aamue kubadilika tu. Si kingine. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI WAKATI WA MALINZI KUJITATHMINI NAMNA ANAVYOIENDESHA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top