• HABARI MPYA

  Wednesday, July 06, 2016

  YANGA WAIENDEA PEMBA MEDEAMA, USHINDI LAZIMA JULAI 16 TAIFA

  Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC inatarajiwa kuondoka Ijumaa mjini Dar es Salaam kwenda kisiwani Pemba kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wake wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana Julai 16, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga inahitaji ushindi wa kwanza katika mechi za kundi hilo, baada ya kufungwa 1-0 mara mbili dhidi ya MO Bejaia nchini Algeria Juni 19 na TP Mazembe ya DRC mjini Dar es Salaam Juni 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Hans van der Pluijm amesema kuhusiana na maandalizi yake kuelekea mchezo dhidi ya Medeama anahitaji ushindi tu.
  Yanga itamenyana na Medeama ya Ghana Julai 16 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Pluijm alisema kuwa matokeo ya ushindi ambayo yatawapa pointi tatu muhimu ndiyo pekee wanayahitaji ili kufanya hesabu wanazozitegemea kuwavusha na hatimaye kusonga mbele kwenye michuano.
  Pluijm alisema bila kushinda mechi hiyo ya tatu, watakuwa wamejiweka kwenye nafasi finyu ya kusonga mbele na hivyo ndoto za kuwania ubingwa wa mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka barani Afrika zitayeyuka.
  "Soka ni mchezo wa makosa, sifikirii kama tutakosea tena katika mechi hii ya tatu ya kundi letu, najua tutacheza tena nyumbani, ni faida lakini kikuwa tunahitaji kushinda, tukifungwa...itakuwa ni majanga," alisema kocha huyo.
  Mdachi huyo alisema watakapofanikiwa kushinda dhidi ya Medeama, tayari nafasi kwa timu mbili zitakazosonga mbele kutoka kwenye kundi hilo itakuwa wazi licha ya kupoteza michezo iliyotangulia.
  Wakati huo huo kiungo mpya, Mzambia Obrey Chirwa ambaye aliyekwenda kwao kwa ruhusa maaulumu, alirejea nchini jana kwa ajili ya kuungana na wenzake kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Medeama.
  TP Mazembe mabingwa mara tano wa Afrika kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndiyo vinara wa Kundi A wakiwa na pointi sita wakifuatiwa na Mo Bejaia yenye pointi nne, Medeama ina pointi moja na Yanga ambayo haina pointi hata moja inaburuza mkia
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAIENDEA PEMBA MEDEAMA, USHINDI LAZIMA JULAI 16 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top